Mashairi: Malezi Ni Msingi Duniani Na Akhera

 Malezi Ni Msingi Duniani Na Akhera

                ‘Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Salaam pwani na bara, ziwafikie wapenzi,

Malezi si masikhara, inahitaji ujuzi,

Lazima uwe imara, mwangalifu si mpuuzi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

Duniani na akhera, ndio msingi malezi,

Inahitaji subira, na kufanya uchunguzi,

Uchunguze mazingira, fanya na upelelezi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

Sikiliza mihadhara, dini yako uienzi,

Ni ngao ilio bora, Mungu Ndie Mkombozi,

Uepushwe na madhara, kulea wana ni kazi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

Duniani ni amana, mikononi mwa wazazi,

Waleleke kiungwana, dini iwe ni mzizi,

Zuri na baya kuona, waelezwe waziwazi.

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

Mwana mpe jina zuri, chagua kwa uchaguzi,

Sana ujitahadhari, majina ya sikuhizi,

Lisiwe lenye dosari, kama jina la machizi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

Kuanzia utotoni, wana wape mazoezi,

Kuswali misikitini, wasiseme hawawezi,

Wasome na Qur-ani, waelewe ya Mwenyezi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

Nguo zile za heshima, ziwe ndio ni mavazi,

Sio zile za shutuma, zile nguo za kishenzi,

Binadamu si mnyama, anaetembea wazi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

 

Watazame marafiki, wakienda matembezi,

Wasiwe ni wanafiki, wahuni na majambazi,

Upate kuyadiriki, nyumbani uwe mlinzi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

Baba na mama nyumbani, wao ni wasimamizi,

Wanapotoka shuleni, fanya sana ukaguzi,

Vijana na wanandani, chunga bila ubaguzi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

Uwafundishe adabu, waseme bila mapozi,

Waambiwe ni aibu, kuitana kwa miruzi,

Na nywele si chekibobu, wapelekwe kwa kinyozi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

Wasichana na hijaabu, hakika hawachukizi,

Waambiwe ni wajibu, wasifanye pingamizi,

Wakivaa na dhahabu, nje wasijibarizi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

Wavae za kusitiri, wasivae dengrizi,

Mwisho wake ni hatari, kama hawasikilizi,

Kama watatakabari, mwisho ni maangamizi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

Wasikie mawaidha, wajifunze wanafunzi,

Mawaidha yana ladha, wapate ufafanuzi,

Uwafanyie orodha, ya masomo kila mwezi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

Akhera utaulizwa, yalikwendaje malezi,

Kama hayakwenda sawa, utalia kwa machozi,

Na kujibu utashindwa, upigwe na bumbuazi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

Na akhera Kwa Jalali, ni mwisho wa uamuzi,

Ukilea kwa halali, peponi ndio makazi,

Thawabu kama jabali, utapewa na pongezi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

Shairi hapa ni mwisho, hapa natia kitanzi,

Ona kuzima koleo, sio mwisho wa uhunzi,

Inanitosha kwa leo, sasa ninapiga mbizi,

Ndio msingi Malezi, duniani na akhera.

 

 

 

 

Share