Mume Anashindwa Kurudisha Amana Ya Mke Aliyeachana Naye – Aombe Du’aa Gani Kuhusu Dhulma Aliyomfanyia?

 

SWALI LA KWANZA:

 

Bismilahi Arahmani Arahim. Asalaam alaikum warahmatullahi wabarakatu,

Kuna mtu na mkewe, yule mke kampa mumewe hela ili amuekee (amuhifadhie) yaani ni kila mwezi huyo mume anapewa amana hiyo amuekee huyo mkewe kwa muda wa miaka, mpaka zikatimia maelfu kadhaa. Kisha mke na mume wakaachana baada ya miaka 6. Mke kadai haki zake zile alizo mpatia mumewe ili umuekee hakulipwa, na akatumana kwa watu ili wamtetee adai haki zake alizo muamini kumpa mtalaka wake amuekee. Lakini Mume mwenyewe hajakataa kama ana deni or ana haki za watu, lakini kulipa ni masumbuano na misukosuko. Jengine ni, Mume huyo-huyo katika miaka hiyo 6 walioishi hakumuangali mkewe kinyumba wala hakumpa chochote kama, matumizi, chakula, mavazi na mengineo haki za mke. Dada anauliza suali jee kuna hukumu gani ya kisheria ya dini yetu kuhusu Mume huyo walioachana, na kuna dua gani za kudhulumiwa kwa Mke kutokana na mtalaka wake na malipo yake ni nini, kutokana kwa Quraan na hadithi? Tafadhali naomba majibu nitumiwe Inshaallah, pamoja na aya za Quraan na Hadithi na dua ya kudhulumiwa. Shukran

 

SWALI LA PILI:

 

Bismilahi arahmani arahim.

Asalaam alaikum warahmatulahi wabarakatu. Jee ikiwa mwanamke amempa mtalaka wake pesa amuekee kila mwezi kabla hawajaachana kwa muda wa miaka sita. Kisha walipo achana mume anamsumbua kumlipa mtalaka wake haki zake. Jee hukumu ya huyo Mume ni nini?

 

 


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 

.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumdai mtalaka wako pesa ambazo anasumbua kuzilipa.

 

 

Hii ni mojawapo ya dhulma ambayo wanawake wanafanyiwa katika jamii yetu. Inaonekana kama waume wameshindwa kuwa waaminifu kwa wake zao kwa wanachoamiwa kwa kiasi ambacho hata baada ya talaka wanapata usumbufu kutoka kwa watalaka wao.

 

Hii ni katika zile alama za unafiki kwa upande wa mwanamme, kwani alama ya mnafiki ni yule ambaye anapoaminiwa hufanya khiyana. Kisha hii dhulma itakuwa ni giza siku ya Qiyaamah, sijui mume atakimbilia wapi Siku hiyo. Yaonyesha kuwa mume amesahau kuwa deni halisamehewi na Waislamu wanatakiwa wasimswalie ikiwa ana deni anapokufa mpaka warithi wake watoe ahadi ya kulilipa. Na deni hilo litakwenda kumuweka pabaya ilihali mdai anaweza thawabu nyingi kutoka kwa mumeo huyo kwa ajili ya hiyo.

 

Na hiyo mara nyingi hutokea kwa wanawake kwa kutojali kufuata maagizo ya Uislamu pindi wanapopata posa. Wazazi na wasichana wao huona kuwa hiyo ni kheri na hivyo kukubali mara moja bila ya kumchunguza.

 

Ama kuhusu du’aa hakuna du’aa maalumu lakini unaweza kuomba yoyote kwa lugha yoyote lakini hatari yake ni kuwa du’aa hiyo hairudishwi na Allaah Aliyetukuka. Hiyo ni ile iliyozungumziwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuwa du’aa ya mwenye kudhulumiwa haina pazia kwa Allaah Aliyetukuka. Kumuombea du’aa ni kama kumlaani.

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  ((ثَلَاثَةٌ لَا تُرَدُّ دَعْوَتُهُمْ,  الْإِمَامُ الْعَادِلُ وَالصَّائِمُ حَتَّى يُفْطِرَ وَدَعْوَةُ الْمَظْلُومِ يَرْفَعُهَا اللَّهُ دُونَ الْغَمَامِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَتُفْتَحُ لَهَا أَبْوَابُ السَّمَاءِ وَيَقُولُ بِعِزَّتِي لَأَنْصُرَنَّكِ وَلَوْ بَعْدَ حِينٍ))

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah  (رضي الله عنه) amesema: Mtume (صلى الله عليه  وسلم) amesema: (([Watu] Watatu hairudishwi Du'aa zao; Imaam muadilifu, mwenye Swawm mpaka afuturu, na Du'aa ya aliyedhulumiwa, Anainyanyua Allaah bila ya mawingu Siku ya Qiyaamah and inafunguliwa milango ya mbingu na Anasema: Kwa Utukufu Wangu, Nitakunusuru japo baada ya muda)) [Ibn Maajah, Ahmad]

 

Sisi tunaona kuwa utumie njia kwanza za kupitia kwa watu wake ili mume alipe deni hilo na ikiwa inaonekana haizai matunda inatakiwa utumie njia za kisheria kwa kuwaona viongozi wa Kiislamu hapo ulipo ili upate haki yako. Haifai kwako kuacha haki yako kwani kufanya hivyo kunawapatia wanaume wengine kuwa na ujasiri kuwadhulumu wanawake wengine.

 

Ama mume wakati alipokuwa amekuoa alikufanyia dhulma ya kutokupa chakula ni madhambi juu yake kwa kufanya hivyo na atakwenda kulipwa mbele Siku ya Qiyaamah kwa hayo. Hata hivyo ilikuwa ukamshitaki kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake, lakini kama ada ya wanawake wanaachia na wanakuja kujuta baadaye.

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Amtie fahamu mume huyo na aweze kurudisha amana hiyo yako.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share