Maamuuma Lazima Wasome Suwratul-Faatihah Au Kisomo Cha Imaam Kinawatosheleza Wote?

 

Maamuuma Lazima Wasome Suwratul-Faatihah

Au Kisomo Cha Imaam Kinawatosheleza Wote?

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalamu alaykum

Ama baada ya kumshukuru Allah (sw) na kumtakia mema kipenzi cha umma huu mtume wetu Muhammad (saw) juu ya ya alizake na maswahaba zake. Ustadh napenda kuuliuza swali moja juu ya ibada ya swala, kuna hoja ya baadhi ya watu husema hakuna haja ya maamuma kusoma Suratil fatihah mara baada ya imamu kusoma sura hiyo na kuisoma sura yoyote ktk quran, kwa madai kua inaposomwa Qur`an muisikilize. Na watu wengine husema swala haiwezi ikakamilika mpaka ipatikane suratil fatihah hata kwa maamuma ila tu pale ambapo amechelewa rakaa itahisabiwa kwake (suratil fatiha) kama aliosomewa na imamu wake na rakaa inayo fuata ita mlazimu aisome

 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.  

 

 

Kwanza tunapenda kukutanabahisha kosa la kufupisha Thanaa, Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), na Maamkizi ya Kiislamu. Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate faida na mafunzo sahihi:

 

Al-Lajnah Ad-Daaimah: Haijuzu Kufupisha Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Katika Maandishi

 

Imaam Ibn Baaz: Kufupisha Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Kwa Mfumo Wowote Haijuzu

 

Hukmu Ya Kufupisha Thanaa (Kumtukuza Allaah) Na Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Na Maamkizi Ya Kiislam

 

Ufafanuzi Wa Kiburi Na Mas-ala Ya Bid’ah Katika Jibu La “Hukmu Ya Kufupisha Thanaa”

 

 

Ama kuhusu swali lako ni kwamba zipo kauli tatu za ‘Ulamaa kuhusu mas-ala haya:

 

 

1- Hasomi Maamuma katika Swalaah ya siri wala dhahiri: Hii ni kauli ya Abuu Haniyfah na wafuasi wake. Na hoja zao ni:  “Aliye nyuma ya Imaam, naye (Imaam) akasoma basi hicho kitakuwa ni kisomo chake (Maamuma)” [Ahmad na Ibn Maajah.

 

Lakini baadhi ya ‘Ulamaa wamesema Hadiyth hii ni dhaifu ingawa wengine wamesema ni sahihi).

 

Na pia kwao kusoma Suwratul-Faatihah si wajibu kabisa, kwa hivyo haitokuwa lazima kwa Maamuma. Soma zaidi kuhusu maelezo ya Hadiyth hiyo na rai zingine kwenye kiungo kifuatacho:

 

Kufutwa Kisomo Nyuma Ya Imaam Katika Swalaah Za Sauti, Na Kuwajibika Katika Swalaah Za Kimya

 

 

2- Maamuma atasoma katika Swalaah za siri wala si za dhahiri: Na kauli hii ndio Madh-hab ya Jamhuri: Az-Zuhriy, Maalik, Ibn Mubaarak, Ash-Shaafi‘iy katika kauli yake ya zamani, Muhammad mwanafunzi wa Abuu Haniyfah, Ahmad na amechagua kauli hii Shaykhul-Islaam, Ibn Taymiyyah. Na hoja zao ni kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَإِذَا قُرِئَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُوا لَهُ وَأَنصِتُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٢٠٤﴾

Na inaposomwa Qur-aan, basi isikilizeni kwa makini na bakieni kimya (mzingatie) ili mpate kurehemewa. [Al-A‘raaf 7: 204]

 

 

Na Hadiyth, “Hakika Imaam amewekwa ili apate kufuatwa, anapopiga takbiyr, nanyi pigeni Takbiyr (na anaposoma nyamazeni)” [Muslim, Abuu Daawuwd na An-Nasaa’iy].

 

Waliobobea katika elimu ya Hadiyth wamedhoofisha nyongeza iliyo katika mabano kwa Hadiyth iliyo juu. Na pia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakataza watu kusoma nyuma yake. Kwa hivyo, watu wakawa hawasomi kwa kisomo cha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Swalaah za jahra pindi waliposikia maneno hayo kutoka kwake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). [Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah]. Wakasema baadhi ya ‘Ulamaa: Hadiyth hii inafuta kisomo nyuma ya Imaam katika Swalaah ya jahri (ya sauti).

 

 

3- Anasoma katika Swalaah za siri na dhahiri: Na hii ni rai ya Imaam ash-Shaafi‘iy katika kauli yake mpya na wafuasi wake, Ibn Hazm na wakachagua rai hiyo ash-Shawkaaniy na Ibn ‘Uthaymiyn. Na dalili zao ni:   “Hapana Swalaah kwa asiyesoma Suwratul-Faatihah” [al-Bukhaariy na Muslim]

 

Pia, “Yeyote mwenye kuswali bila kusoma Mama wa Qur-aan (Al-Faatihah) haikutimia. Abuu Hurayrah akaulizwa: ‘Sisi tunakuwa nyuma ya Imaam’. Akasema: ‘Isome kwa nafasi yako…’” [Muslim, Abu Daawuwd, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah].

 

Na Hadiyth yenye kueleza uhususia uliotajwa, kwani Aayah na Hadiyth zilizotumika ni za kijumla kwa rai ya pili. Hadiyth hii ni kutoka kwa ‘Ubaadah bin asw-Swaamit (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa alisema: Tulikuwa nyuma ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye Swalaah ya Alfajiri, ambamo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kukawa na uzito katika kisomo chake. Alipomaliza, akasema: “Huenda mkawa mnasoma nyuma ya Imaam wenu?’ Tukasema: ‘Ndio, ee Rasuli wa Allaah!’ Akasema: ‘Msifanye ila kwa ufunguzi wa Kitabu (al-Faatihah), kwani hakuna Swalaah kwa asiyeisoma (hiyo Suwrah)’” [Abu Daawuwd na at-Tirmidhiy].

 

Kwa hivyo, masuala hayo yana tofauti baina ya ‘Ulamaa ingawa wengi wameonelea kusoma nyuma ya Imaam katika Swalaah ya sauti ndio sahihi zaidi, na hakuna shaka katika Swalaah za kimya.

 

Pia utapata faida zaidi kwenye kitabu hiki:

 

Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share