Mlio Wa Simu Wa Qur-aan Akisikia Asiye Muislamu Inafaa?

 

Mlio Wa Simu Wa Qur-aan Akisikia Asiye Muislamu Inafaa?

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalam Alaykum:

 

Swali langu ni kwamba, Kuna milio ya simu unapompigia mtu unaisikia wakati unamsubiri apokee (caller tune). Je kama Mkisto anakupigia na inakua anaisikia je ni sawa au? Nahitaji ufafanuzi wenu.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hakika ni kuwa Muislamu hafai kuweka mlio wa simu kuwa wa Aayah au Suwrah ya Qur-aan kwani Qur-aan haikuteremshwa kwa lengo hilo. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ  

Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na batili). [Al-Baqarah: 185]

 

 

Na kisha Qur-aan haifai kusomwa katika sehemu fulani mojawapo ikiwa ni chooni. Mfano umeingia chooni na ikaanza kulia itabidi uizime lakini hasara tayari itakuwa imepatikana. Pia ikianza kulia nawe uishike, hata kabla ya kumalizika Aayah itakuwa ni utovu wa adabu.

 

Bonyeza kiungo kifautacho upate jibu lenye maelezo zaidi:

 

Kuweka Milio Ya Miziki Kwenye Simu Za Mkononi Au Qur-aan Inayosomwa Au Adhaana

 

Ama sauti ya Qur-aan kusikika na asiye Muislamu haina tatizo kabisa. Ikiwa asiye Muislamu anataka kujua kuhusu Uislamu licha ya kusikiliza hata kuisoma kwa kupatiwa tafsiri kwa lugha anayoielewa ndio bora na lengo.

 

Kwa hiyo, jambo hilo halina tatizo katika shari’ah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share