Mume Anagawa Kidogo Kwa Mke Mdogo Na Kwa Mke Mkubwa Anagawa Zaidi – Nini Hukmu Yake?

SWALI:

 

Assalam alleykum, nashukuru kwa kupata fursa hii niliyojaaliwa na Allah s.w mimi nina swali langu moja linalo nitatiza nimeolewa mke wa 2 mume wangu hugawa kidogo sana kwangu na kingi hupeleka kwa bi mkubwa katika kila agawapo je kwa kufanya hivyo mume yu sahihi? Au yuakosea nini hukmu yake katika hilo?

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 



 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mume kugawa kidogo kwako kama mke mdogo na kingi kwa mke mkubwa.

Hakika ni kuwa kila kitu katika Uislamu kina mfumo, utaratibu na nidhamu yake. Na uke wenza pia una nidhamu, mpangilio na utaratibu wake muruwa kabisa ila kila kitu kiende katika njia inayotakiwa.

 

Uislamu umeweka masharti ya kukubaliwa mume aoe mke wa pili. Miongoni mwayo ni:

 

1.    Awe ni muweza wa kufanya uadilifu baina ya wakeze: Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Aliyetukuka: “Basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wanne. na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu” (an-Nisaa’ [4]: 3).

 

 

2.    Ajiamini katika nafsi yake kuwa hatafitinika wala kupoteza haki zao: Hakika Amesema Aliyetukuka: “Enyi mlioamini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu wamo maadui zenu. Basi tahadharini nao” (at-Taghaabun [64]: 14).

 

3. Awe na uwezo wa kuwatimizia mahitaji yao ya kimwili, hivyo kuwaepusha na uasherati na kuwabakisha katika utwaharifu.

 

 

4.  Awe na uwezo kwa wasaa wake kuwapatia mahitaji yao yote, kama kuwalisha, kuwavisha, kuwapatia malazi na matibabu: Huu ni wajibu mkubwa wa mume na awe muadilifu pia kwa hayo ili kusiwe na utesi wa aina yoyote. Allaah Aliyetukuka Anausia: “Na wajizuilie na machafu wale wasiopata cha kuolea, mpaka Allaah Awatajirishe kwa fadhila Yake” (an-Nuur [24]: 33).

 

 

5.   Pia haifai kwa mume kuwakusanya wake zake wote katika nyumba moja pasi na idhini ya wakeze: Amesema Aliyetukuka: “Enyi mlioamini! Msiingie nyumba za Nabii ila mpewe ruhusa kwenda kula, sio kungojea kiwive” (al-Ahzaab [33]: 53). Na Ametaja hapa Aliyetukuka nyumba kwa wingi na sio moja.

 

Baada hayo yaliyo tangulia hapo juu, tunaweza kusema kuwa swali la muulizaji wetu haliko wazi kama inavyohitajika. Haliko wazi kwa kuwa hakutaja idadi ya watu katika nyumba ya mke mkubwa na mdogo. Inawezekana kuwa nyumba ya mke mkubwa ina watu wengi zaidi kuliko yako (mke mdogo). Ikiwa nyumba moja ina watu kumi na nyingine watatu haiwezekani kuwa vyakula vigaiwe sawa. Hii ni kuwa akipeleka nyumba ya mke mkubwa kilo 3 ya mchele kwako ataleta kilo moja. Huu ndio uadilifu kwa mgao baina ya wake.

 

Lakini ikiwa kwa idadi hiyo kule anapeleka kilo 3 na kwako nusu kilo hiyo itakuwa ni dhuluma kwako. Dhuluma imekatazwa kwa Dini ya Kiislamu. Hivyo, ikiwa anafanya hivyo itabidi uzungumze naye ajirekebishe, kwani akitojirekebisha kwa mujibu wa Hadiyth ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Siku ya Qiyaamah atafikishwa mbele ya Allaah Aliyetukuka ilhali upande mmoja wake umeinama.

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akupe usahali na ikiwa kweli mume hafanyi uadilifu Amrudishe katika njia ya sawa ya kutekeleza uadilifu huo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share