Mume Anayedai Kujua Dini Anaishi Naye Bila Nikaah Akidai Kuwa Inatosheleza Baba Wa Mke Kupokea Mahari Na Sasa Mja Mzito

SWALI:

 

Asalam alaikum

Mimi naomba kuuliza swali ambalo nadhani ni la ajabu lakini natumai mutanipa ufaafanuzi nielewe. mimi nimeolewa lakini kabla ya kuolewa posa yangu ilikua ni ya utata sana hadi ikapita kama mwaka mmoja mzima kwa subra, mume wangu alhamdullilahi ni mtu aliye shika dini na mwenye elimu ndio sababu ya kukubali kuolewa na yeye ili nami nipate faida kwake lakini mushkil wangu ni kuwa hatukufanya nikah akidai kua si lazima kufanya nikah madhali baba amekubali, mahari imekubalika na mimi mwenyewe nimekubali.....kulingana na ilmu yake anasema kua ana ushahidi kua nikah si lazima kwa wanandoa. Kabla sijakutana naye nilimwambia kua ni lazima tufanye nikah hata kama si lazima ili kuepukana na mushkil, mpaka sasa hatujafanya nikah na nimejaliwa kushika mimba yake sasa ina miezi 6. Swali langu ni je ni sawa tunavyofanya ama ni zinaa kwani sitaki kuingia kwenye dhambi ya zina tena, inshaalah naomba munieleze ili nisiwe na wasiwasi. Shukran. 

 

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kufunga Nikaah na mume unayempenda.

Hakika ni ajabu kwa mtu unayesema ana elimu ya dini lakini akashindwa kufahamu muongozo wa Uislamu kuhusu ndoa. Uislamu ni nidhamu katika kila jambo lake, kubwa au dogo. Na ndoa haiko nje ya nidhamu hiyo na hivyo ikawekewa masharti ili wanaume na wanawake wasiwe ni wenye kuchukuana tu au kuketi bila ndoa ya halali. Na jambo hilo ndio imetofautisha baina ya ndoa ya Kiislamu na ‘njoo tukae pamoja’.

 

Masharti ya kusihi ndoa ya Kiislamu ni kama yafuatayo:

 

1.     Kukubali kwa mume kuoa na mke kuolewa. Bila idhini hiyo hakuna ndoa baina ya mume na mke.

 

 

2.     Idhini ya walii – baba au jamaa ya karibu ya mke aliyepatiwa jukumu la kutoa idhini. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hapana ndoa bila ya walii” (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na al-Haakim).

 

3.     Ni lazima kuwe na mashahidi wawili waadilifu wakiwa zaidi ya hao ni bora zaidi. Na amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hapana ndoa isipokuwa kwa walii na mashahidi wawili waadilifu” (ad-Daraqutwniy na al-Bayhaqiy).

 

4.     Kuwe na Khutbah, ambayo inatakiwa ifungwe na baba mzazi wa msichana. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia sana tuitangaze Nikaah zetu ili kila mmoja ajulikane kuwa ni wa watu sasa. Tamko la ndoa: Nimekuoza fulani binti fulani au nimekuozesha binti yangu fulani...

 

 

5.     Mume kulipa mahari aliyotaka msichana. Na mahari ni wajibu kwa kauli ya Aliyetukuka: “Na wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni kipawa”, lakini hata hivyo, ikiwa mke ataachia kwa radhi zake, Allaah Aliyetukuka Anaendelea: “Lakini wakikutunukieni kitu katika mahari, kwa radhi yao, basi kileni kiwashuke kwa raha” (an-Nisaa’ [4]: 4). Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuhusu mahari: “Tafuta japokuwa pete ya chuma” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Masharti hayo yaliyo juu yakikamilika basi ndoa hiyo inakuwa ni ya Kiislamu na mume na mke ni wa halali kukaa pamoja. Ikiwa baadhi yake hayakufanyika basi inakuwa wewe na mumeo mumekaa pamoja nje ya shari’ah ya Kiislamu, hivyo kuchukuliwa kuwa mnazini tu.

 

Inafaa ujiepushe na utata huo ambao tayari umeingia ndani yake. Na ni ajabu kuwa baba yako amekubali wewe ukae na aliyekuposa katika hali kama hiyo isiyo ya kishari’ah!

 

Rejea haraka katika haki na jiepushe na hayo maisha mnayoishi hivi sasa yasiyo ya Kiislam. Na fahamu kuwa huyo mwanaume hajui dini na ni katika wajanja tu wanaotaka kupata mahitajia yao kiwepesi na kwa njia ya mkato. Na isije ikawa ni wale wanaoamini ndoa ya muda ambayo haina walii wala mashahidi na kama ni hivyo, basi usije kushangaa baada ya masiku ukatupwa tu na akaendwa kuchukuliwa mwengine kwa njia kama hiyo hiyo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share