Anapokuwa Safarini Mke Wa Pili Hataki Kuwasiliana Naye, Na, Anamjibu Ujeuri, Je, Amuache Kwa Tabia Yake Hiyo?

SWALI:

 

A.w.w. Mimi na wake 2. Napokua safarini napata ugumu mno kuwasiliana na mke wa 2, kila napoitaji kuwasiliana nae basi ataki kuniongelesha, ata navyotuma ujumbe kupia marafiki ataki. Napokua safirini nawaweka wote nyumba moja, kadhalika napoaga aoneshi ushiriiano mzuri nami kama mwenzie. Nini uislamu unazungumzia kuh.mke behaviour kwa mume juu ya utiifu na nini nifanye kwani inaudhi kiasi nafikiria kumuacha, siku nyingine kumuongeresha anaeza kuja juu, ila swala la tendo la ndoa aina tatizo. Naomba fatuha nimfikishie, mimi ni mgeni kwenye dini yetu hii.

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mke kuwa mjeuri kwako.

 

Matatizo na shida za kuoa mke mmoja au wawili zinatokea kwa mume kufanya uchaguzi mbaya kwa mwendani wake katika maisha yake.

 

Hata hivyo, kukitokea tatizo au matatizo ya kindoa hutakiwi wewe kama mume kufanya haraka kutoa talaka. Kuhusu hilo Allaah Aliyetukuka Amesema:

Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Allaah Ametia kheri nyingi ndani yake” (an-Nisaa [4]: 19).

 

Unaweza kufanya yafuatayo kabla ya kuchukua hatua yoyote ile.

 

1.     Huenda kuwa mke wako hajui wajibu wake kwako. Kwa hivyo, fanya juhudi umpeleke katika Madrasah ya sawa ili aweze kupata mafunzo ya Dini yamwezeshe kuishi Kiislamu.

 

2.     Jaribu kuzungumza naye kuhusu mas-ala ya kidini kwa kumletea vitabu vya Dini, VCD, DVD, CD na kaseti za mawaidha kuhusu maudhui tofauti za Kiislamu (Nyingi zipo tayari ALHIDAAYA hapa Mawaidha, Swahili Video). Unaweza kutumia watu wake wa karibu ili wazungumze naye. Mas-ala ya kushauriana ni muhimu sana katika Uislamu, na ikiwa pengine makosa ni yako basi fanya juhudi kujirekebisha katika makosa hayo yako.

 

3.     Ikiwa hajajirekebisha basi itabidi uitishe mkutano baina yako wewe, mkeo, wazazi wake na wazazi wako. Wakikosekana, unaweza kuwaita wazee wengine wazoefu katika mas-ala ya upatanishi na wenye kutaka maslahi ya ndoa kubakia.

 

4.     Ikiwa hadi hapo hamkupata suluhu ya mkeo kujirekebisha basi itabidi mwende kwa Qaadhi ili aweze kuwapatanisha au kwa Shaykh mzoefu, mcha Mngu, mwenye elimu na muadilifu ili awasikilize.

 

Hata hivyo, kw aupande mwengine huenda ikawa kosa ni lako. Na lau kadhiya hiyo tutakuwa tumeielewa vyema basi utatuondoshea utata wowote ule.

Tulivyoelewa ni kuwa mke/wake zako wanaishi nyumba mbali mbali ila tu wakati unasafiri unamchukua mke mdogo unampeleka kwaenye nyumba ya mke mkubwa. Hilo ni kosa kisheria kufanya hivyo bila ya ruhusa ya mkeo. Kwa hiyo, nasaha yetu ya kwanza kwako ni kuwa jaribu unapoondoka umwache kila mke kwake isipokuwa wanaporidhia kukaa pamoja. Twatumai kuwa kwa kufanya hilo utaondosha tatizo hilo na pengine ikawa si dharura kufuata utaratibu tuliouandika hapo juu na unaweza kufuata utaratibu wowote mwengine unaokubaliana na shari’ah.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Mke Mjeuri Juu Ya Kwamba Anapewa Raha Na Mahitajio Yote Na Mume

 

Mke Mjeuri Sana - Anamwambia Mtoto Wangu Kuwa Nimeshakufa, Nifanye Nini?

 

 

 

Twakutakia kila la kheri na kutatua tatizo hilo kwa njia nyepesi kabisa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share