Kuunganisha Swalaah ya Adhuhuri Na Alasiri Bila Ya Sababu Inafaa?

 

SWALI:

 

Assalam alaikum warahmatu llah wabarakatuh,

 

Ktk sahihi Muslim hadith ya 705 (Babu swalat lmusafir) na ktk sahihi lbukhar Babu ta-akhru swalat dhuhr ila l-asr Hadiyth ya 528, zasema Mtume swalla llahu alaih wasallam alikusanya adhuhr na al-asr, maghrib na al'ishaa bila khofu wala safari wala mvua, alipoulizwa akasema ili isiwawee taabu umati wangu. Tukiamuwa fanyia kazi Hadiyth hizi, kwa kuzikusanya swala hizo kila siku ili isituwee taabu itakuwa makosa?

ma'asalam


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuunganisha Swalah bila ya sababu yoyote.

Hakika tumetafuta namba za Hadiyth na milango uliyoitaja lakini hazipo huko; inawezekana umekosea kunukuu.

 

Ama Hadiyth ya kwanza iliyopo katika Muslim tumeipata kuwa ni Hadiyth namba 1628 na pia 1629, katika mabano ikandikwa 705 (Baab al-Jam’ baynasw Swalaatayn Fil Hadhwr – Mlango wa kuunganisha Swalah mbili kwa Mkaazi). Ama mlango ulioutaja, Baab Swalaatul Musaafir, ni kabla ya ule ulioutaka uko kabla ya ule ulioukusudia. Ama Hadiyth katika al-Bukhaariy hiyo uliyoitaja ni Baab Man Tarakal ‘Aswr (Mlango wa Mwenye Kuacha Alasiri).

 

Hadiyth hizo ulizozitaja katika Muslim na nyenginezo zenye maana sawa na hiyo ni Hadiyth zilizo sahihi kabisa. Na ni hakika kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya hivyo katika maisha yake hapa duniani bila ya udhuru wa safari wala kuwa na mvua. Hata hivyo, hebu tujiulize alifanya jambo hilo la kuchanganisha Swalah kwa muda gani? Je, alifanya kila siku katika uhai wake? Hilo halijapatikana katika uhai wake bali alifanya hivyo mara chache sana katika uhai wake.

 

Kwa hiyo, Hadiyth hizo zinatuelezea tu ruhusa kuwa twaweza kuunganisha Swalah mara moja moja na sio kila siku. Lau ingekuwa huo ndio mtindo wa shari’ah, au ndio alioutaka yeye kwetu, basi angeundeleza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe. Pia Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) wangekuwa wamefahamu hivyo pamoja na Salaf wangelitekeleza hilo kimatendo lakini kutofanya hivyo ni kuwa suala la kuchanganisha Swalah kama wafanyavyo Mashia halifai kufanywa kila siku. Na Allaah Aliyetukuka pamoja na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wametufahamisha kuhusu Swalah tano ambazo zatakiwa kuswaliwa kwa nyakati zake.

 

Imaam an-Nawawiy katika kuisherehesha Swahiyh Muslim ametuambia kuwa hiyo haikuwa ada wala desturi na kawaida ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bali aliifanya mara chache sana. Na wakati alipofanya hivyo alikuwa mgonjwa. Pia imethibiti wakati mwengine akichanganya kwa sababu ya mvua.

Ama hilo wanalolifanya Mashia kila siku maisha yao yote wanahitaji kulitolea ushahidi ikiwa Mtume au Maswahaba zake walifanya hivyo maisha yao yote! Na hakutokuwa na dalili zaidi ya hiyo iliyoelezwa na muulizaji na hivyo tutapata kuwa ufahamu wa kimakosa wa nuswuus na watu kutafuta uwepesi na kuchukua fursa ya kuendekeza matamanio yao, ndio kukawa na matumizi mabaya na kinyume juu ya Aayah na Hadiyth kama hizo. Suala hili kwa kiasi Fulani linafanana na ufahamu mbovu wa ile Aayah ya wudhuu ya 6 ya Suratul Maaidah ambayo Mashia wanaitumia kwa kupangusa miguu wakati wa wudhuu badala ya kuosha kama ilivyofahamika na Mtume na Maswahaba zake na Waislam wote.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Kuakhirisha Na Kujumuisha Swalah

Kuswali Kabla Ya Wakati

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share