Zawaaj (Ndoa) Ya Al-Misysaar - Nini Hukmu Yake?

SWALI

 

Assalam alaykum warahmatu llahi wabarakatuhu,

 

Tafadhali ningeomba kutoka kwa masheikh wetu wa al hidaaya, nifafanuliwe nini maana ya "zawaj misyar". 

 

Nilivyo fahamishwa ni hivi:

Ni ndoa ambayo haina mambo mengi kama ndoa ya kawaida. Mwanamke huwa labda ana umri mkubwa na bado hajaolewa abadan na labda ana kazi yake nzuri na mapato mazuri kwa hivyo anajiangalia mwenyewe kimaisha, au ana familia inayojiweza kimaisha. Khususi kwa mwanamume anayesafiri kila wakati aidha kwa kazi au jambo lingine lolote, anakuwa na mke wake wa kwanza nyumbani, halafu anaowa mwengine mahali anakosafiri (au pia kutoka sehemu anayoishi) humueka kwao (kwa familia ya mke au peke yake na kujiangalia mwenyewe) huwa ndoa hii haina masarifu mengi wala conditions, mwanamke anajiangalia mwenyewe kimaisha. Mume anaweza kumtembelea wakati wowote ule hata baada ya mwaka, almuhim ni amemuowa kisheria na watu wanajua.

 

Jee hii ndoa inakubalika kisheria kiislamu. Wassalam alaykum warahmatu llahi wabarakatuhu.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndoa ya Misyaar.

Zawaaj al-Misyaar (ni aina ya ndoa) ambayo inagawanyika sehemu mbili. Nazo ni kama zifuatazo:

 

1)  Zawaaj al-Misyaar inamaanisha kufungwa ndoa baina ya mume na mke. Mkataba unatimiza masharti yote ya ndoa ya kawaida kama kuwepo kwa walii wa msichana, mashahidi wawili waadilifu, kuridhia kuolewa kwa msichana na kukubali kwa mume. Hata hivyo, ama kuhusu haki ya nyumba na uangalizi wa kifedha, mume hana jukumu la mke, kwa kuwa mkewe ataishi nyumbani kwao au nyumba yake, naye huwa anakuja kama mume. Ziada ya hayo, anajishughulikia kwa mahitaji yake.

 

2)  Aina ya pili ya Zawaaj al-Misyaar ni mkataba ambapo ana jukumu la kumkimu mkewe kifedha, hata hivyo, hatompatia mgao wa sawa kuhusiana na kulala kwake kwa zamu. Aina hii ya Zawaaj al-Misyaar ndio iliyo maarufu zaidi kwa kuwa mume anataka kuiweka ndoa yake kuwa siri ili mkewe asiwe ni mwenye kujua lakini inatimiza mahitaji yote ya ndoa ya kawaida.

 

Ama kuhusu aina ya kwanza ya Zawaaj al-Misyaar, tunafikiria kuwa ni matakwa ya mwanamke kutaka kujihifadhi na zinaa na pia kuwa na Niyah ya kupata mtoto au watoto ambako kunampelekea katika ndoa hii. Hivyo, aina zote mbili zinakubalika na ni halali. Ama kule kukubali kuacha baadhi ya haki ya mmoja wa wakeze mume katika ndoa aina hii haina utata wowote maadamu tafanywa kwa ridhaa na kutakuwa na maslahi kabla au baada ya mkataba wa ndoa hiyo.

 

Hakika, Zawaaj al-Misyaar inawapatia wanandoa baadhi ya faida kama kulinda na kuhifadhi heshima na utwahirifu mbali na kuepusha na yale malengo ya ufisadi, uharibifu, hasa kwa waseja. Hata hivyo, ndoa hii ina matatizo yake kama kutofautiana na kukosana kuhusu urithi na haki nyinginezo, ambazo zinaweza kuibuka baada ya kifo cha mume. Ili kuondoa baadhi ya matatizo hayo inatakiwa mume aweke wazi kuwa ana mke mwengine ili akifa, wao, yaani mke na watoto wapate fungu lao la urithi. Jambo hili limewafanya wanavyuoni wengine kama Shaykh Muhammad bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn, Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy na ma-Ustadh wa al-Azhar kuikataza Zawaaj al-Misyaar, kwani inakinzana na roho ya ndoa katika Uislamu na ina athari kubwa kwa mwanamke, familia na jamii kwa ujumla. Lakini, wanavyuoni wengi wameikubali kwani ina masharti yote ya ndoa ya halali na pia wakati wowote mke ana haki ya kudai haki zake zote kama mke katika ndoa ya halali.

 

 

Na ndoa hii haiwezi kabisa kufananishwa na ndoa ya muda ‘Mut’ah’ ambayo wanaiofanya Mashia yenye kukosa masharti ya ndoa na yenye malengo ya kujistarehesha kimwili tu. Na wale wanaotyaka kufananisha baina ya Misyaar na Mut’ah, lengo lao ni kutafuta sababu penginepo ili kuhalalisha makosa yao.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share