Fadhila Za Kusuluhisha Waliokhasimiana -2

 

Fadhila Za Kusuluhisha Waliokhasimiana - 2

 

Alhidaaya.com

 

 

Tukiendelea na fadhila za kusuluhisha waliogombana wakakhasimiana, na iwapo baada ya kusoma mada hii tutazithamini fadhila hizi, basi kila mmoja wetu atakimbilia kufanya hima ya kupatanisha ndugu zetu wa Kiislamu waliokhasimiana. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Amelichukia jambo hili kwani linavunja asili ya undugu wa Kiislamu kama Anavyosema : 

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ ..﴿١٠﴾

 Hakika Waumini ni ndugu, basi suluhisheni baina ya ndugu zenu. [Al-Hujuraat: 10]

 

Na kwa jinsi jambo hili lilivyochukiza hadi kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anakataa kupokea amali za watu waliokhasimiana mpaka wapatane, na hawasamehe watu hao:  

 عن أبي هريرة رضي الله عنه قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((تُعرض الأعمال في كل أثنين وخميس فيغفر الله لكل أمريء لايشرك بالله شيئاً، إلا إمرءاً بينه وبين أخيه شحناء فيقول: اتركوا هذين حتى يصطلحا)) رواه مسلم

Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba kasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Amali njema (vitendo vyema) hutandazwa kila Jumatatu na Alkhamiys, kisha Allaah Humghufuria kila mtu asiyemshiriki kitu Allaah, isipokuwa mtu aliyekuwa baina yake na baina ya ndugu yake uhasama, Husema: Waacheni hawa wawili mpaka wapatane)) [Muslim]

 

Kwa hiyo ni hatari kubwa kwa waliogombana kuwa wanapoteza umri wao bure kutenda mema na hali kumbe havipokelewi vitendo hivyo hadi  wapatane.

 

 

Njia za kupatanisha Watu

 

1-Kwanza tia nia kuwa unafanya kupata Radhi na ujira mkubwa kutoka kwa Allaah na muombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akuwafikie jambo hili. 

 

2-Msikilize kila mmoja malalamiko yake. 

 

3-Ukishajua sababu ya ugomvi, watajie hatari ya kuhasimikiana kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) 

 

4-Tafuta wakati na sehemu munaasib kwa wote wawili.

 

5-Ikibidi kusema uongo, inafaa katika jambo hili kwa kutaka kumridhisha mmojawao ili kuleta suluhisho kama alivyoruhusu Nabiy(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth:

 

((لَيْسَ الْكَذابُ الَّذِي يُصْلِحُ بَيْنَ النَّاسِ فَيَنْمِي خيرا أو يقول خيرا))  رواه البخاري ومسلم

 "Si muongo yule anayesuluhusha watu kwa kusema uongo, kwani anaarifu mema au anasema mema [kwa lengo la kusuluhisha]"  [Al-Bukhariy na Muslim]

 

6-Fanya uadilifu, usipendelee hata kama mmoja ni jamaa yako wa karibu au unampenda zaidi.  Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):  

.فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ

 Basi suluhisheni baina yao kwa uadilifu, na timizeni haki. Hakika Allaah Anapenda wanaotimiza haki. [Al-Hujuraat: 9]

 

Na Anasema tena Allaah  Subhaanahu wa Ta'aalaa : 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاءَ لِلَّـهِ وَلَوْ عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَوِ الْوَالِدَيْنِ وَالْأَقْرَبِينَ ۚ إِن يَكُنْ غَنِيًّا أَوْ فَقِيرًا فَاللَّـهُ أَوْلَىٰ بِهِمَا ۖ فَلَا تَتَّبِعُوا الْهَوَىٰ أَن تَعْدِلُوا ۚ وَإِن تَلْوُوا أَوْ تُعْرِضُوا فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا ﴿١٣٥﴾

Enyi walioamini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu mtoapo ushahidi kwa ajili ya Allaah japokuwa ni dhidi ya nafsi zenu au wazazi wawili, au jamaa wa karibu. Akiwa tajiri au maskini Allaah Anawastahikia zaidi. Basi msifuate hawaa mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa au mkikanusha basi hakika Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [An-Nisaa: 135]

 

 

7-Wakishapatana In shaa Allaah  omba du'aa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Awaendeleze masikilizano na mapenzi baina yao na muombe pia Akutakabalie juhudi yako.

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atunufaishe kwa yale tunayojifunza na Atuajaalie miongoni mwa wale wanaosikiliza kauli (nyingi) wakafuata zile zilizo njema. Aamiyn.

 

 

 

 

 

 

Share