Mtoto Wao Amelawiti Mtoto Mwengine, Wamfanye Nini?

 

 

SWALI:

 

Assalam aleikum

Nalileta suali langu kwenu nikitarajia ufafanuzi.

Nina kijana alipofika umri wa 15yrs nikamuona hana raghba ya masomo ya kiengereza. Nikaamua bila kumpotezea wakati afadhali nimpeleke hifdhil quran! La kunihuzunisha ni kua baada ya mwaka na nusu -niliitwa nilipofika nikapewa khabari yakuhuzunisha!!! Niliambiwa kua mtoto wako ameshikwa na kitendo cha qaumulut. Tukajaribu kujadiliana mbele yao ikapatikana kua alikipata hapo mahali mda tuu alipoanza masomo yahifdhil quran. Nimehuzunishwa sana kupata hii khabari na kunikosesha raha.

 

Mwanipa fikra gani ama ushauri gani kwa huyu mtoto??? Kwani nilimdhihirishia kua lau kungekua na hukmu ya kiislaam wallahi ninge mhukumu!! Mwaeza nipa fikra ama ushauri!??? Shukran!


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu liwati.

Tufahamu kuwa liwati ni katika madhambi makubwa yaliyokatazwa na Uislamu kwa kauli za wazi kabisa. Ni nasaha kwa kila mmoja wetu anapotaka kumpeleka mtoto kwenye Madrasah basi achague Madrassah za Sunnah za watu wenye kuaminika maadili yao na elimu yao, kwani Madrasah nyingine hawaoni umuhimu mkubwa wa uasherati aina hiyo kwa kuweka waalimu wasio na maadili na wenye tabia chafu ambao wamevaa vazi la watu wa dini na hali ni waharibifu wa maadili. Na Madrasah kama hizo waalimu wenyewe ndio wanaowafanya watoto kitendo cha liwati.

 

Kwa hiyo ni muhimu kuwa na tahadhari kubwa sana kuhusu hilo. Na inaonyesha ni hiko kisa cha mtoto wako ambacho umekipata lakini visa hivyo vinaweza kuwa ni vingi. Suali ni kuwa je, waalimu wenyewe wamechukua hatua gani? Ikiwa wao hawajachukua hatua inaonyesha kulikubali jambo hilo katika sehemu hiyo ya kielimu.

 

Kwa kila njia, hata kama waalimu hawakuchukua hatua wazazi ni lazima wachukue hatua. Na hatua ni kama zifuatazo:

 

1.     Kumtoa Madrasah hiyo na kumtafutia nyingine yenye misimamo ya Sunnah baada ya kuichunguza na kuiona kuwa iko sawa. Ni muhimu kumbadilishia mazingira ya masomo na sehemu. Na ukimpeleka Madrasah nyingine isiwe ni kuhifadhi tu bali kuwe na masomo mengine kama , ‘Aqiydah na Tawhiyd, Qur-aan na tafsiri yake, Hadiyth, Fiqh, Siyrah, Lugha na masomo mengineyo.

 

2.     Ni muhimu mtoto azungumziwe kuhusu mas-ala ya Imani, kutii amri za Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na katika hilo aelezewe madhara ya kujiweka katika madhambi kama hayo hapa duniani na kesho Akhera. Na Muislamu katika Qur-aan ameagiziwa asikaribie zinaa, liwati itakuwa ni mbaya zaidi.

 

 

3.     Ni muhimu huyo mtoto apatiwe nasiha za nguvu kuhusu suala hilo huenda akawa ameathirika na mazingira aliyoingia.

 

Kisha suala la kuwa alionekana akifanya kitendo hicho ni upande mmoja. Je, mtoto mwenyewe amekiri kuwa amefanya kweli? Na waliomuona ni wangapi katika hao walioshuhudia? Suala la zinaa na liwati ni suala gumu, na shari’ah haikubali mpaka kuwa na mashahidi wanne walioona kihakika kitendo hicho kikifanyika, la sivyo katika shari’ah yule aliyekuja ndio mwenye kuadhibiwa. Na suala hilo haliwezi kupatikana katika Madrasah isipokuwa kunapokuwa na uzembe aina fulani hapo au kuna wataalamu tayari wa hilo.

 

Na kukiwa na shari’ah ya Kiislamu, si wewe utakayemhukumu bali ni Khalifa au Qadhi wa mji wako au sehemu mnayoishi. Na mtu hawezi kuhukumiwa mpaka kuwe na ushahidi wa kutosha kuhusu tuhma hiyo.

 

Kwa hivi sasa fanyeni juhudi za kumpatia nasiha, na InshaAllaah, atakuwa ni mwenye kuacha ikiwa kweli alitumbukia katika kitendo hicho.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share