Mke Akitaka Talaka, Alipwe Nini?

 

SWALI:

 

A, alaikum jina issa mussa swali langu ni kama mke wangu akitaka talaka ana haki ya kupata mahari yake kani mm nilioa mwaka 2008 mwezi wa 8 na tunaishi mbali kidogo sijamuona mke wangu toka nimuoe  kwa sababu ya kisheria mm siruhusiwi kusafiri na mke wangu ana haki ya kusafiri na anakazania kumuona mama yake ambaye hayuko karibu naye anasema hajamuona mama yake naomba mnisaindie kwani mke wangu ni msilamu lakini hajue ndini ya Kiislamu.

 

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mke kutaka talaka.  Hakika hili na matatizo mengine ya kinyumba ni matatizo sugu sana katika jamii yetu. Mwanamme na mwanamke pia wanaingia katika ndoa bila kujua majukumu yao wala yanayohitajika kufanywa wanapokuwa wanandoa. Haya huleta matatizo na shida nyingi hata mara nyingine kumalizikia katika talaka.

 

Kwa ajili hiyo, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) alituuisia sana tuoe wanawake wenye Dini laa sivyo tutapata matatizo mengi. Tatizo ulilo nalo kwa sasa ni kwa ajili yako kupuuza agizo hilo na nasiha hiyo nzuri na nyeti kutoka kwa Mtume wetu. Lau ungekuwa umeichukua tahadhari hii basi hungekuwa na tatizo wala taabu hizi unazokabiliana nazo kwa sasa.

 

Ikiwa mke anataka talaka inategemea anataka talaka kwa sababu gani. Ikiwa anataka kujivua kutokana nawe, bila ya wewe kuwa na makosa itabidi yeye akulipe mahari uliyompatia wakati wa ndoa yenu. Hata hivyo, akiomba talaka kupitia kwa Qaadhi kwa sababu ya makosa uliyonayo wewe basi Qaadhi ataweza kuwaachisha baada ya kusikiliza pande zote mbili. Na katika hali hiyo, hutarudishiwa mahari uliyotoa wakati wa ndoa.

 

 

Na jambo la ajabu sana kwa mtu kuoa kisha kukaa mbali na mkewe. Mume anatakiwa akae na mkewe pale ambapo anaishi mume huyo. Na ilikuwa muhimu sana kwa mume kabla ya kuoa aijulishe familia ya mke pamoja na mke mwenyewe kuwa hatoweza kukaa kwao kwani yeyea anaishi nchi nyingine kwa hivyo itabidi mke asafiri kwenda kwa mumewe. Hupatikana matatizo mengi kwa mke kukaa mbali na mumewe na kinyume chake, kwani tashwishi na fitna inakuwa kubwa.

 

Ulipoona kuwa wewe huruhusiwi kabisa kusafiri ilikuwa uliweke wazi hilo. Na kwa kuwa mke anatakiwa akae kwa mumewe, na kishari’ah baada ya ndoa ana haki zaidi juu yake kuliko mama, hivyo, inabidi kutumwe watu wajuzi wa Dini wamueleweshe hayo ili arudi katika utiifu wa mume na kukaa naye.

 

Kukusaidia katika tatizo hilo itabidi ima wewe mwenyewe usafiri ukamchukue mkeo, na akiwa atakataa, itabidi utume watu ambao wanaweza kuzungumza naye na kumuelewesha kuhusu mas-ala hayo Kidini ili apate kurudi nyuma na kufuata kanuni hizo.

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

 

Kujivua Mwanamke Katika Ndoa (Khul'u) Na Hukumu Zake

 

Mut’ah (Kiliwazo, Kustarehea, Kitoka Nyumba, Masurufu) Ya Kumpa Mke Anayeachwa

 

Je, Inafaa Mume Na Mke Kuishi Mbali Kwa Muda Mrefu?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share