Mzazi Wake Hataki Anioe Naye Ananipenda Sana Yuko Tayari kunioa Kwa Siri

 

SWALI:

 

Assalam-aleikum,

Ndugu zangu waislam nina swala linalo nisumbuwa akili kwa kweli sina raha. Ninaye mpenzi wangu wa siku nyingi aliye tayari kuniowa hata sasa ila shida wazazi wake. Kunaye mchumba aliyechaguliwa na babake ila hamtaki kadri ya kiwango hawaongei na babake akinihakikishia hawezi niacha hata kuniowa kwa siri aweza niowa hata babake akimfanya nini.

JE, NIFANYE NINI? NAOMBA MAONI KUTOKA KWENU...NAJIONA KAMA MIMI NDO NI CHANZO CHA KUGOMBANISHA WATU HAWA.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mzazi kutotaka mtoto wake akuoe.

 

Maelezo yako yanasikitisha kuona kuwa bado kuna Waislamuu wengi hawajui shari’ah ya dini yao. Umetaja kuwa una mpenzi na hali hajakuoa!! Vipi msichana wa Kiislamu au mvulana awe na mapenzi na asiye Mahram wake?

 

Hakika ni kuwa hili ni suala la mapenzi limekuwa tatizo sugu katika jamii yetu ya Waislamu leo kote ulimwenguni. Uislamu umeweka vikwazo vikubwa kwamba mwanamme na mwanamke ambao si Mahram wasiwe ni wenye kukutana. Ikiwa hali ni hiyo vipi msichana atakuwa na mpenzi ilhali yeye hajaruhusiwa kufanya hivyo kishari’ah na kufanya kwake hilo ni kupata dhambi mbele ya Allaah Aliyetukuka.

 

Kisha dada yetu tazama sana kuwa tumeusiwa sana na Dini yetu kuwa tuwe ni wenye kuwatii wazazi wetu wakiwa wako baada ya kutiiwa Allaah Aliyetukuka. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na Mola wako Ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa heshima” (A-Israa’ [17]: 23).

 

Ucha Mungu wa mtu huonekana kwake kwa kufuata maagizo ya Allaah Aliyetukuka na kuepukana na makatazo Yake. Na kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuagizia na kutunasihi dada zetu waolewe na wenye Dini hatuna budi nasi kufuata maagizo hayo. Kukosa kufanya hivyo basi mtu hufikiwa na matatizo mengi sana katika maisha yake.

 

Kuhusu hilo, Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

Msifanye wito wa Mtume baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi. Hakika Allaah Anawajua miongoni mwenu wanaoondoka kwa uficho. Basi na watahadhari wanaokhalifu amri Yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu kali” (An-Nuur [24]: 63).

 

Ikiwa mtu amekwenda kinyume na amri ya Allaah Aliyetukuka kwa kutomheshimu mzazi ambaye ameamriwa amheshimu au amtii. Je, anaweza kumtii mtu mwengine ambaye mafungamano yake ni ya kindoa peke yake? Kila mtu ana baba na mama mmoja tu ambao hawezi kuwabadilisha wala kuwakataa lakini mke anaweza kuwa na zaidi ya mmoja au hata kumuacha. Mtu ambaye anaweza kugombana na baba hadi ya kuwa hazungumzi naye ni hatari kwake hapa duniani na kesho Akhera.

 

Suala la ndoa si la kumfanya mwanamme au mwanamke kugombana na mzazi wake. Suala la ndoa ni la khiyari ya mwenye kuoa, lakini hata hivyo mzee anafaa ashirikishwe katika shughuli hizo kwani nasaha zao ni muhimu. Wakati ikitokea kuwa mnapishana na mzazi kwa kuwa yeye anataka uoe msichana fulani nawe wataka mwengine, inatakiwa utumie mbinu ya kuweza kumkinaisha mzee wewe mwenyewe au kutumia jamaa wengine au wanachuoni kuhusu hilo. Ikiwa bado anaendelea kubisha mwanamme hahitaji idhini ya walii, anayehitajia idhini hiyo ni msichana. Hivyo, mwanamme anweza kuoa bila kuvutana na mzazi wake kwani kugombana naye ni makosa makubwa katika Uislamu.

 

 

 

Jambo jingine ni kuwa hakuna ndoa ya siri katika Uislamu kwani katika ndoa ni lazima kuwe na mashahidi waadilifu kwa uchache wawili.

 

Bonyeza viungo vifautavyo upate maelezo zaidi:

 

Ndoa Ya Siri Inafaa Ikiwa Wazazi Hawataki?

 

Ndoa Ya Siri Inafaa?

 

 

 

Na wewe kama msichana unayeolewa ni lazima walii wako akubaliane na ndoa hiyo. Hata hivyo, kuna maswali kadhaa ya kujiuliza:

 

1.     Je, una hakika huyu ndiye mume unayemtaka kwa kuwa tu anakupenda?

2.     Je, unamtaka mwanamme huyu akuoe kwa kuwa ameshika Dini, au ni mtu mwenye pesa au ni mtu mwenye uzuri au ni kwa sababu gani?

3.     Je, wewe umemridhia hata kule kugombana kwake na baba yake?

 

Ukiyajijibu maswali hayo utakuwa umefikia hali ya kuweza kuamua unalotaka na unakoelekea. Hata hivyo, tungependa sana uzingatie Dini yake kabla ya kuingia katika mahusiano ya kindoa. Pia anza kutaka ushauri kutoka kwa Allaah Aliyetukuka kwa kuswali Swalah ya Istikhaarah. Ikiwa kwa kufanya hivyo utaona ishara ya kuwa uepukane na ndoa na huyo mwanamme basi fanya hivyo. Na wala usivunjike moyo ikiwa kwa sababu moja au nyingine kwa kuwa hamkuweza kuoana, kwani Allaah Aliyetukuka ndiye Mwenye kupanga na huenda ukawa umeondolewa balaa kubwa sana. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui” (Al-Baqarah [2]: 216).

 

 

 

 

Na usivunjike moyo, kwani kuvunjika moyo ni sifa ambayo si ya Kiislamu na ukiacha jambo kwa ajili ya Allaah Aliyetukuka Atakupatia badali iliyo njema zaidi kuliko hiyo ya awali. Allaah Aliyetukuka Anaeleza katika Qur-aan:

...Hakika hawakati tamaa na faraji ya Allaah isipokuwa watu makafiri” (Yuusuf [12]: 87).

Na tena: “Na anayemcha Allaah, Humtengezea njia ya kutokea” (At-Tahriym [65]: 2).

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akufanikishe kuweza kupata lililo na kheri nawe hapa duniani na Kesho Akhera.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share