Anafanya Kitendo Cha Siri Kisha Anatubu Kisha Anarudia Tena, Hadi Anaacha Kuswali, Vipi Aache Maasi Haya

 

Anafanya Kitendo Cha Siri Kisha Anatubu Kisha Anarudia

Tena, Hadi Anaacha Kuswali, Vipi Aache Maasi Haya

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Assalam Aleykum Enyi ndugu zangu Waislam Kwana kabla sijauliza Swali Langu ningependa Kuwapongeza kwa kufungua Tovuti hii yenye Kuelimisha wanaopenda dini ya Kiislam mi nina Swali ngependa Kuwauliza na nitafurahi mtakavyonjibu

 

Nini Athari ya Alieapa Kwamba Hatorudia Jambo Halafu Akarudia Mara Mbili Lakini Mtu Huyo Huyo Bado Anania Aongoke Lakini Matamanio Ya Mwili Hayamuachi? Na Anataka Msamaha Kutoka Kwa Rabb Wake.  Mfano mimi huwa nina matamanio sana ya kuingiliana Kimwili na msichana nimejitahidi nimeacha lakini nimeshindwa kuacha Musterbation na niliapa kwamba najuta kwa ninayo fanya ee Rabb Niongoze na sitarudia tena lakini nimerudia mara mbili jee nifanye vp kurudia kwangu hunifanya muda mwingine nisi swali Kabisa Nisaidieni ndugu zangu Lakini nahitaji Maghfira kutoka kwa Rabb wangu. Masalaam

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Fahamu ndugu yetu kuwa Allaah Aliyetukuka ni Msamehevu sana, Naye Anasamehe kila jambo kama Alivyosema:

 

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu. [Az-Zumar: 53].

 

Kwa hiyo, mwanzo usikate tama na ni lazima uwe na azma yenye nguvu. Ukiwa na sifa hizo pamoja na kumuomba Allaah Aliyetukuka basi yatakusaidia kabisa katika kujiondoa na madhambi hayo. Huenda pia una marafiki wabaya ambao wanaokushawishi kuliendea hilo ovu ambalo limekatazwa na Allaah Aliyetukuka. Ikiwa unaweza kutimiza masharti haya, basi msamaha wako kutoka kwa Allaah Aliyetukuka una dhamana:

 

1.     Kujiondoa katika maasiya hayo.

2.     Ajute sana katika kufanya kosa hilo.

3.     Aazimie kutolirudia tena kosa hilo.

 

Uchu huo wa matamanio huenda ukawa unakuja kwa sababu huna mke. Kwa hiyo, unatakiwa ufanye juhudi za kutafuta mke ili uweze kukidhi mahitaji yako ya kimwili kwa njia ya halali. Kisha pia usiwe ni mwenye kuapa apa kila wakati, bali weka nia nzuri kabisa wala usiape kwani kuapa kunahitajia kafara ikiwa hujatekeleza kiapo chako.

 

Ili kupunguza matamanio yako inabidi pia uwe ni mwenye kufunga kama alivyoagiza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kufanya hivyo kutafanya matamanio yako yapungue kwa kiasi kikubwa. Na kufanya kosa la kujichua isikupelekee kuacha Swalah kwa hali yoyote ile. Shikamana na Swalah kwa hali zote na huku unamnyenyekea Allaah Aliyetukuka ili Akuondolee tatizo hilo.

 

Yaonyesha kuwa yamini uliyoweka si ya upuuzi bali ni ya kweli kweli. Kwa ajili hiyo kuonyesha kuwa kweli unataka kurudi kwa Allaah Aliyetukuka inatakiwa na inafaa utoe kafara iliyolezewa katika Aayah iliyo chini. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

لَا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا عَقَّدتُّمُ الْأَيْمَانَ ۖ فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ أَوْ تَحْرِيرُ رَقَبَةٍ ۖ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ ۚ ذَٰلِكَ كَفَّارَةُ أَيْمَانِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ ۚ وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٨٩﴾

Allaah Hatokuchukulieni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini Atakuchukulieni kwa (kuvunja) viapo mlivyoapa kwa niyyah mlioifunga thabiti. Basi kafara yake ni kulisha maskini kumi chakula cha wastani mnachowalisha ahli zenu, au kuwavisha nguo, au kuacha huru mtumwa. Lakini asiyeweza kupata (katika hayo), basi afunge Swiyaam siku tatu. Hiyo ndio kafara ya viapo vyenu mnapoapa. Na hifadhini yamini zenu. Hivyo ndivyo Allaah Anavokubainishieni Aayaat (na hukmu) Zake ili mpate kushukuru. [Al-Maaidah: 89].

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share