Vipi Kugawa Urithi Kwa ndugu Au Mtoto Aliye Mgonjwa Wa Akili?

 

 SWALI:

 

Asalam aleikum warahmatullahi wa barakatu.

 

Napenda kuwashukuru ndugu zangu wa alhidaaya kwa kazi yenu kubwa mnayoifanya inshaallah Allah atawalipa.

 

Napenda kuuliza swali langu kuhusu ugawaji wa urithi. Baba yetu amefariki miaka mingi nyuma. Na ameacha mali nyingi haikugaiwa hapo mwanzoni, sasa inataka kugaiwa. Nasi tuko ndugu wa kiume na wa kike. Ndugu yetu mmoja ana ugonjwa wa akili, hakuoa wala kuzaa, na serikali ya   inamuangalia kihali na mali - jee hii sehemu yake tuifanye nini? Tugawane sisi ndugu au tuitoe sadaka au tufanye kitu cha kheri kwa jina lake au la wazee wetu?

 

Tutashukuru kwa Ufafanuzi wenu. Ahsanteni.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu sehemu ya mirathi ya ndugu yenu ambaye ana upungufu wa akili. Ama kuhusu hilo Allaah Aliyetukuka Ametupatia muongozo wa kihakika pale Aliposema: “Wala msiwape wasio na akili mali yenu ambayo Allaah Ameyajaalia yawe ni kiamu yenu. Walisheni katika hayo na muwavike, na mseme nao maneno mazuri” (an-Nisaa’ [4]: 5).

 

Kwa hiyo, mnachohitajika ni kuyatunza mali ya ndugu yenu huyo kwani ugonjwa wa akili wakati mwingine huondoka na mtu akarudi kuwa na akili timamu kabisa. Yatizameni kwa vizuri mali yake, kwa pengine kuyafanyia biashara, na kutoka mali yake hiyo kumtimizia mahitaji yake mengine. Na mhakikishe kuwa lau yatakuwa ni mali yanapaswa kutolewa Zakaah hilo lifanywe. Ikiwa atakuwa ni mwenye kuaga bila kutumia ndio nyinyi mtakaokuwa warithi wake.

 

Ni maombi yetu kwa Allaah Aliyetukuka Ampatie ponyo na arudi kama wengine walio na akili timamu na siha nzuri.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share