Skip navigation.
Home kabah

Jinsi Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Sallam) Alivyokuwa Akisherehekea Mazazi Yake

 

 

Tawakkal Juma Husayn

 

 

“Allaahumma Swallii ‘Alaa Muhammadin Wa’alaa Aali Muhammadin Kamaa Swallayta ‘Alaa Ibraahiyma Wa’ala Aali Ibraahiyma Wabaarik ‘Alaa Muhammadin Wa’ala Aali Muhammadin Kamaa Baarakta ‘Alaa Ibraahiyma Wa’ala Aali Ibraahiyma Innaka Hamiydun Majiydun”.

 

 

Hii ndiyo Swalahh ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambako kumethibiti kuwa na fadhila na malipo makubwa sana. Kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ‘Ibaadah iliyothibiti kishari’ah tena yenye thawabu lukuki. Tena kuna wakati ni lazima kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni maneno ya kizushi yatamkwayo na baadhi ya watu wenye chuki ambazo tunaweza kuziita chuki binafsi kuwa kuna watu hawamswalii Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au hawapendi kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tena wakiwakejeli kama Mawahabi! Na miongoni mwa madai yao ni kuwa wao hupinga Maulidi. Wakati yakisemwa hayo moja kati ya wanazuoni wao wakubwa naye si mwengine bali ni Ibnu Qayyimul Jawziyah ametunga kitabu kizima kikielezea juu ya Swalah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akikiita Jilaaul Afhaam fiy Swalaati khayril anaam.

 

 

 

Kwa kuwa kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ‘Ibaadah Ibnul Qayyim ametaja ndani ya kitabu chake hicho sehemu 48 ambazo mtu anatakiwa amswalie Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Ni ukweli kuwa wanaotetea kuwa wanampenda Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawazijui sehemu hizo za kishari’ah ambazo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatakiwa aswaliwe. Ndani ya sehemu hizo 48 ambazo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatakiwa kishari’ah aswaliwe Maulidi hayako!!!!

 

 

 

Ndugu yangu katika Uislamu unaposema jambo fulani ni ‘Ibaadah maana yake ni sawa na kusema Allaah na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Wake wameamrisha jambo hilo lifanywe, hapa kuna hatari ya kumzulia Allaah na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Wake. Hatari inakuwa kubwa zaidi pale wanapotokea watu wakatetea tena kwa nguvu zaidi na kuleta dalili za Aayah na Hadiyth kuhalalisha uzushi huo. Ndugu zangu katika Iymaan Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

“Atakayenizulia uongo kwa makusudi basi na ajiandalie makazi yake motoni.” Al-Bukhaariy

 

 

 

Muislam yampasa azingatie yafuatayo:

 

 

  1. Kusherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Maulidi kama kufanywako na watu siku hizi hakukufanywa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wala Maswahaba zake wala Taabiina, wala Taabii Taabiina. Kwa hiyo hapa unazungumza kupita bila kusomwa Maulidi kitambo kisichopungua miaka 400.

 

 

 

  1. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaweza kusherehekea Maulidi au mazazi yake katika wakati wake bila kipingamizi tena Swahaba zake kama akina ‘Uthmaan Bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) wangechinja ngamia wengi tu kwa ajili ya mnasaba huo kama ungekuwa unafaa kishari’ah. Kama walivyokuwa wakifanya kuchinja wakati wa Hijja. Kule Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutokulifanya yeye wala Swahaba zake, wakati walikuwa wanaweza kulifanya jambo hilo kishari’ah linakuwa ni uzushi au bid’ah ambayo Muislam anatakiwa aliepuke. Kwa mantiki hii Sunnah ni kinyume cha taarifu hii yaani jambo lolote lile ambalo lilikuwa linawezekana kufanyika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bila kipingamizi kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akalifanya na Swahaba zake, jambo hilo ni Sunnah na Waislamu wanatakiwa walifanye. Pia ni katika Sunnah jambo lolote lile ambalo lilikuwa linawezakana kufanyika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kisha pakapatikana  sababu au kipingamizi ikawa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kashindwa kulifanya lakini Swahaba zake wakalifanya jambo hilo baada ya sababu kuondoka, jambo hilo nalo ni katika Sunna na Waislamu wanatakiwa walifanye mfano ni  kuswali Swalah ya Tarawehe kwa jamaa ambako Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichelea isije Tarawehe ikafaradhishwa na hivyo kuwa uzito kwa Waislamu. Kwa kuwa jambo la kufaradhishwa lilikuwa linapitia kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa njia ya wahyi; kuondoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kufaraki kuliondoa kizuizi kile.

 

 

 

  1. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunga siku ya Jumatatu ya kila wiki. Alipoulizwa kwa nini anafanya hivyo alijibu kuwa; hiyo ni siku aliyozaliwa, na ndiyo siku aliyopewa Utume na ndiyo siku aliyotemshiwa ndani yake Qur-aan. Kwa mujibu wa Hadiyth hii Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisherehekea Maulidi au  mazazi yake kwa kufunga, hivyo na sisi hatuna budi kumuiga Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kusherehekea kuzaliwa kwake kwa kufunga kwani yeye kwetu ni kiigizo chema. Pamoja na kuwa siku ya Jumatatu ndiyo siku aliyozaliwa, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kataja matukio mengine mawili kuhusiana na siku hii yaani kupewa kwake Utume na kutemshiwa Qur-aan. Sababu hizi tatu zinaweza kupatikana ndani ya siku ya Jumatatu wala haziwezi kupatikana vyote abadani ndani ya tarehe 12 ya mwezi wa Rabiy’ul Awwal. Kisha wanachuoni wote wamekubaliana kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kazaliwa ndani ya siku ya Jumatatu lakini wametofautina juu ya tarehe ya kuzaliwa kwake. Jingine ni kuwa ukitazama vitabu vyote hutokuta kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya jambo lolote lile maalumu katika tarehe ya kuzaliwa kwake ambayo ilikuwa ikimpitikia akiwa ndani ya Utume kwa muda usiopungua miaka 23. Swali la kujiuliza hapa ni kuwa kama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisherehekea siku ya kuzaliwa kwake kwa kufunga wewe na mimi tumepatia wapi suala hili la kusherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kukusanyika na kusoma Maulidi?

 

 

 

Fudhwayl bn ‘Iyaadh (Allaah Amrehemu) alisema;

“Allaah Haikubali ‘amali yoyote ile ya mja isipokuwa ile ambayo iliyotakata na iliyo sawa. ‘Amali iliyotakata kishari’ah ni ile ambayo imefanywa kwa ajili ya Allaah peke Yake (Ikhilaasw) na iliyo sawa ni ile ambayo imefanywa kwa kuangalia na kuiga vile Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akiifanya yaani Al-Mutaba’atu”.

 

 

 

Muislam wa kweli hapati tabu anapokuwa na msingi kama huu ambao kwa hakika ni msingi madhubuti miongoni mwa misingi inayompelekea kung’amua ukweli wa mambo. Acha wale ambao wamekuwa wakilivalia njuga jambo hili la Maulidi kwa msingi wa kauli yao mashuhuri kuwa tuliwakuta baba zetu wakifanya hivyo.

 

 

 

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amezungumza kuwa;

“Mtu anayetafuta elimu pasina kuuliza ushahidi wa hayo anayofundishwa mfano wake ni kama akusanyaye kuni usiku hukusanya na majoka yakawa yanamng’ata hali ya kuwa hajui.”

 

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuacha katika mchana ambao usiku wake ni sawa na mchana huu. Yaani katuachia hoja zilizo wazi sana ambazo hapotei isipokuwa mwenye kuangamia.

 

 

 

Kanuni muhimu ya Uswuul Fiqh inasema hivi:

“Katika Uislamu ‘Ibaadah yoyote ile ni haramu kuifanya isipokuwa pale itakapokuja dalili kuwa hiyo ni ‘Ibaadah inayofaa kufanywa kishari’ah”.

 

 

 

Ni katika mantiki hii watu kama Imamu ash-Shaafi’iy wanasema kuwa “Atakayepelekwa na akili yake kuona kuwa je kuna ubaya gani kulifanya hili au lile atakuwa anajitungia Shari’ah yake mwenyewe kinyume na Shari’ah ya Allaah na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wake.”

 

 

Ibn Maajishuun naye akasema:

“Atakayezua katika Uislamu ‘Ibaadah ambayo anaiona kuwa ni nzuri au haina ubaya wowote, kwa kufanya hivi atakuwa anasema kwa lisaanul haal japo hadhihirishi kauli yake kuwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya khiana asifikishe baadhi ya mambo.”

Akiendelea akasema Ibn Maajishuun;

“Mwenyezi Mungu Amesema siku ya hijja ya mwisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Leo hii nimweakamilishia dini yenu” Suratul Maaidah: 3

 

kwa hiyo kile ambacho hakikuwa siku hiyo ni katika dini hakiwezi leo kuwa katika dini”.

 

 

 

Tunaposema kuwa asli katika ‘Ibaadah zote ni kuwa kishari’ah hazifai kufanya mpaka tuwe tumeruhusiwa au tumeamrishwa na Shari’ah kuzifanya, na hili ni jambo lililokubalika kwa wanachuoni wote kuwa hakuna kufanya ‘Ibaadah yoyote ile iwayo mpaka uwe umeamrishwa au umeruhusiwa na shari’ah.

 

 

 

Ukweli huu unatupelekea tuwaulize wanaosoma Maulidi, kuwa Maulidi kama Maulidi ni ‘Ibaadah?

 

 

Achana na dhana ya kusema kuwa kwenye Maulidi kuna kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndani yake na hata kusoma Qur-aan. Hiyo si hoja kwani kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndiyo ni ‘Ibaadah lakini hapo si mahala pake na ni hivyo hivyo kusoma Qur-aan hapo si mahala pake. Tazama kuwa Qur-aan ni dhikri iliyokuwa bora kuliko zote lakini niambieni nini hukumu ya mtu kusoma Qur-aan anapokuwa amesujudu wakati wa kuswali.

 

 

 

 

Al-Mutaaba’atu au kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama Sharti muhimu la kukubaliwa ‘Ibaadah ya mtu ili kutimie ni lazima mambo sita yapatikane:

 

 

 

  1. Ibaadah ni lazima iwe imejengwa katika sababu iliyothibiti Kishari’ah. Kwa mfano Tahajudi au kisimamo cha usiku ni ‘Ibaadah tukufu, lakini ikiwa mtu atasimama kisimamo cha usiku siku ya tarehe 27 Rajab kwa hoja kuwa anafanya hivyo kwa kuwa hiyo ni tarehe ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda katika ile safari ya Israa na Mi’iraaj. Tahajudi hiyo itakuwa ni bid’ah na ni Baatwil kwani itakuwa imejengwa katika sababu ambayo haikuthibiti kishari’ah.

 

 

 

  1. Ibaadah ni lazima iwe imejengwa katika msingi wa kiwango ambacho imekadiriwa kishari’ah. Kwa mfano huwezi kusema kuwa wewe ni Mnyenyekevu sana na hivyo ukaamua kuswali Swalah ya Asubuhi rakaa nne badala ya mbili. Swalah yako hiyo ni Baatwil na inakutia katika madhambi.

 

 

 

  1. Ibaadah ni lazima pia iende katika namna ambayo aliifanya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ‘Ibaadah hiyo. Kwa mfano huwezi kutawadha kwa kuanzia miguuni kuja mikononi kisha ukasema unatawadha kishari’ah.

 

 

 

  1. Ibaadah ni lazima iwe katika wakati muafaka iliyopangiwa na Shari’ah. Kwa mfano huwezi kuchinja kwa ajili ya Hijja katika mwezi wa Rabiy’ul Awwal. Ni lazima uchinje katika yale masiku ya kuchinja ya Dhul Hijjah ndipo kuchinja kwako kukubalike.

 

 

 

  1. Ibaadah pia ni lazima iwe katika aina ya kitu ambacho kimekubalika kishari’ah. Kwa mfano huwezi kuchinja farasi kama udh-hiyah hata kama una farasi mia moja. Bali ni lazima uchinje ng’ombe, mbuzi, kondoo au ngamia.

 

 

 

  1. Ibaadah ni lazima iwe katika pahala ilipopangiwa kishari’ah. Kwa mfano huwezi kukaa itikafu nyumbani kwako ukasema unakaa itikafu ya kishari’ah. Kimsingi utachukuliwa kuwa unajipumzisha tu hapo nyumbani kwako kwani itikafu haiwi isipokuwa Msikitini.

 

 

 

 

Miongoni mwa Hadiyth zilizo wazi kabisa kuhusiana na suala hili ni ile isemayo Kullu bid’atin dhwalaalatin wa kullu dhwalaatin fiy nnaar” yaani;Kila uzushi ni upotevu na kila upotevu mahala pake ni motoni”.

 

 

 

Kuna wajanja ambao hudai kuwa kullu hapo maana yake ni baadhi na huuliza kwa kejeli Kullu iliyoko hapa kwenye Hadiyth hii ni Kullu ya namna gani? Kulliyah au Ba’adhiyah? Kabla sijalitolea ufafanuzi hili kwa kuchukulia Kullu kama Ba’adhiyah au baadhi katika hadithi hii maana ya hadithi sasa itakuwa: “Baadhi ya bid’a au uzushi ni upotevu na baadhi ya upotevu ni motoni”!

 

 

 

Awali ya yote hakuna aliyesema kuwa Hadiythi hii ina ulakini au si sahihi. Kwa hiyo wote tunakubaliana kuwa Hadiythi hii ni sahihi. Ikiwa ni hivyo basi inapasa pia tujue Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anakusudia nini aliposema Kullu bid’atin dhwalatun. Kwa ufahamu wa kawaida dhahiri ya Hadiythi hii inaonyesha kuwa kila bid’ah ni upotevu. Hivyo inawezekana kuwa jambo fulani si bid’ah kwa hiyo si upotevu au ni bid’ah lazima itakuwa ni upotevu isipokuwa watu wanachanganya na kutokujua upotevu wake na ubaya wake na hili ndilo linalotukumba sana hapa.

 

 

 

Katika lugha ya Kiarabu maneno yanapokusanya vitu vitatu; Ukamilifu wa nasaha, ukamilifu wa mapenzi na huruma, na ukamilifu wa Fasaha yanakuwa yanakusudia kinachokusudiwa katika Taabiri hiyo!

 

 

 

Katika Hadiyth hii mambo haya matatu yanapatikana kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema maneno haya katika katika Nasaha, ufasaha na huruma na kwa mapenzi makubwa aliyo nayo juu ya ummah wake. Tatizo kubwa sana mara nyingine linakuwa ni kuelewa kinachokusudiwa. Ukiisoma vizuri Hadiyth hii ya “Kullu bid’atin dhwalaalatun, wakullu dhwalaatin fii nnaar” utaona kuwa kinachokudiwa ni ujumla wa bid’ah. Maadamu, jambo fulani ni bid’ah basi litakuwa dhwaahalah au upotevu kwa mujibu wa Hadiyth hii ambayo sote tunakubaliana kuwa ni sahihi.

 

 

 

Siku zote tunakubaliana kuwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni fasaha kuliko watu wote katika Ummah huu na hata mara nyingine husemwa yeye pekee ndiye aliyeweza kutamka herufi dhwaad vizuri!. Katika fasaha yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) siku zote alikuwa akiweka wazi pale ambapo kasema hivi na watu wanaweza kuelewa vile.

 

Laa sivyo wana Uswuul wanayo kanuni inayosema; “Tarkul istifswaal fiy Maqaamil ihtimaal yunazzalu manzilata ‘umuumi fil maqaal” kwa maana ya kuwa kuacha kufafanua katika pahala ambapo watu wanaweza kuelewa hivi au vile kunachukuliwa kuwa kinachokusudiwa ni kila kinachotajwa katika kauli hiyo.

Kwa maana nyingine Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kauli hii alikuwa havui kuwa kuna kullu Ba‘adhiyah na kullu kulliyah au bid’atun hasanatun na bid’atun sayyiatun. Na hivi ndivyo walivyofahamu mabingwa wa lugha ya Kiarabu ambao pia ni mabingwa wa Shari’ah ya Kiislamu kama akina Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan, ‘Aliy na wengineo (Radhiya Allaahu ‘anhum). Inapokuja kullu katika Taabiri ya Kiarabu huwa inagusa kila kitu isipokuwa pale kitakapokuja cha kuivua na hakikuja katika Hadiyth hii cha kuivua ila matamanio ya nafsi zetu. Kusema kuwa kullu bid’atin, kuwa kullu  hapo ni ba‘adhiyah itatulazimu tuseme pia ile wakullu dhwalaatin fiy nnaar nayo pia ni ba’adhiyah kwa kuwa hiyo ina ‘atwifishwa katika ile ya kwanza; yaani tukisema kullu bid’atin dhwalaalatun kisha tukasema kullu hapo ni ba’adhiyah ni kama kusema ba’adhu bid’atin hasanatun waba’adhun aakhari sayy’atun na ni hivyo hivyo tutasema kwa upotofu kuwa kuna upotofu mzuri au mwema na upotofu mbaya. Sijui kama kuna aliyewahi kusema hivyo!

 

Jingine ni kuwa kinachowafanya watu waseme kuwa kullu hapo ni ba‘adhiyah ni kuwa hawajui kuwa bid’ah ni nini na hili ndilo linalowapelekea hata kufikia kuviita vipaza sauti kuwa ni bid’ah!

 

 

 

Kuna wanaofikia hata kudai kuwa vipaza sauti navyo ni bid’ah. Hawa tunawaambia kuwa katika Uislamu vipaza sauti n.k. ni maendeleo ya kiteknolojia ya zama hizi ambayo yanamuwezesha mwanaadamu Muislam akiwemo kuendesha vizuri maisha yake na hata ‘Ibaadah zake na hivi ni vitu vyenye asili katika shari’ah bali vinaitwa wasaail na haviitwi bid’ah!.

 

 

 

Mfano: ilivyo ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitaka Muadhini aadhini kwa sauti ya juu ili watu wengi iwezekanavyo waweze kusikia Adhana. Sasa katika zama hizi tuna vipaza sauti ambavyo kwa kweli havibadilishi sauti na maneno ya Muadhini bali vinachofanya ni kuikuza ili watu wengi zaidi wasikie wito wa kuwaitia jambo jema la Swalah n.k. Na hili ni jambo ambalo alikuwa akilitaka sana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Vitu hivi sio bid’ah katika shari’ah ya Kiislamu, japo kilugha vinaweza kuitwa bid’ah kwa maana ya kuwa vimevumbuliwa katika wakati wa sasa na havikuwa vimevumbuliwa wakati uliopita.

 

 

 

Jingine ni kuwa hudaiwa kuwa ‘Umar bin al-Khattwwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwahi kusema Ni’imatul bid’ah haadhihi” yaani bora ya bid’ah ni hii akimaanisha kitendo cha kuwakusanya watu kuswali Swalah ya Tarawehe chini ya Imaam mmoja kitu ambacho Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakufanya. Hili limekwishajibiwa katika maelezo yangu juu ya Sunnah kuwa jambo hili lina asli katika Uislamu na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliacha kuswali Tarawehe kwa Jama’ah kwa kuogopa isije kufaradhwishwa na hivyo kuwa uzito kwa Waislamu.

 

 

 

Ni kweli kuwa ‘Umar bin al-Khattwwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) katumia bid’ah kilugha hapa wala si kishari’ah. Yaani Bid’atun man’tuqaan Sunnatun maf’huuman. Neno hili pia limetumika kilugha katika Suratul-Ahqaaf, Aayah ya 9. Laa sivyo hakuna mwenye rukhsa kutanguliza neno mbele ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tena sote tunajua ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alivyokuwa mkali katika shari’ah za Mwenyezi Mungu hadi pamesemwa kisa ambacho japo katika usahihi wake kuna walakini au fiyhi nadhwar kuwa mwanamke mmoja aliwahi kumwambia ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) mbele ya watu pindi alipotaka kuweka kiwango maalumu cha mahari kuwa amepata wapi hilo wakati Allaah Amesema wapewe hata kama ni Qintwaar yaani mali nyingi sana. ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema kuwa amekosea ‘Umar na mwanamke kapatia. Hichi ni kisa maarufu kwa watu wengi, hivi mtu kama huyu anawezaje akafanya jambo la kizushi kisha akasema Ni’imatul bid’ah haadhihi na akawa anakusudia kimaana ile bid’ah aliyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Kullu bid’atin dhwalaalatun!

 

 

 

Ama ile Hadiyth Man sanna fiyl Islaam” maana yake ni “Sanna tanfiydhan la ibitida’an wala tashriy‘an” yaani kahuisha jambo ambalo lilikuwepo lakini likawa limesahauliwa na anayekusudiwa hapo ni mtu yeyote lakini sharti awe Muislam. Sunnatan hasanatan hapo maana yake mwendo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) uliokuwa umesahaulika na hili linarandana na sababu ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kusema maneno hayo katika ule ugeni uliokuja Madiynah ukiwa katika dhu’uful haal ambao Maswahaba walishindana katika kuwasaidia.

 

 

 

Wabillaahit Tawfiyq