Muislamu Kuwekewa Kiungo Cha Asiyekuwa Muislamu Baada Ya Kufa - Organ Transplant

SWALI:

Assalaamu Aleykum Warahmatul-laahi Ta'ala Wabarakaatuh.

Shukrani zote anastahili Allah (subhanahu wata'ala) mola wa viumbe vyote. Na rehma na amani zimshukie nabii wetu Muhammad (Salla laahu Aleihi Wasallam). Mwanzo kabisa natoa pongezi zangu za dhati kwa maustwaadhi wetu wa alhidaaya na wanachama wote wa hii website kwa kutuma maswali yao yenye kuwaelimisha wao na sisi tunaoitembelea hii website kutafuta faida. Mungu awajaalie Husnal khaatim indal maut, Amiin. Sheikh nilitaka kuuliza swali ambalo limenitatiza sana, swali lenyewe ni hili;

{A} je transplant ya kubalika katika dini hii yetu ya kiislaam?

{B} je kama yakubalika, inafaa mtu kusaini karatasi ili pindi atakapoaga dunia vile viungo/organ vyake vitolewe ili apewe mtahaji wa vile viungo? Na kwa Allah (subhanahu wa ta'ala) nini hukmu ya mtu huyu aliyedonate?

{C} Na kama yakubalika tena, yafaa muislamu akiwa nahaja sana na kiungo flani kutiwa kiungo cha mtu aliyekuwa mkristo?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa maswali yako kuhusu kutoa viungo kwa ajili ya kumsaidia muhitaji.

Hakika ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia sana tuwe ni wenye kufanya dawa kwani hakuna ugonjwa usiokuwa na dawa. Na mara nyingine dawa inakuwa ni kutolewa kiungo ambacho kimeharibika kabisa na kutiwa kilicho kizuri.

 

Kwa minajili hiyo Uislamu unatazama na kupatia kipaumbele uzima na afya ya mwanaadamu na hata ikafanya ni dharura kwa mwanaadamu kuwa na haki ya kuishi. Kwa hiyo, kukitokea haja ya mtu kufanyiwa transplant basi Uislamu hauna pingamizi bali utakubali hilo kwa moyo mkunjufu kabisa.

 

Uislamu hivyo hivyo umemkirimu mwanaadamu akiwa hai na anapokufa pia kwa kiasi ambacho pindi Muislamu anapoaga dunia kuna mambo ambayo anafaa kufanyiwa. Mambo hayo yote ni kwa maslahi ya aliyefariki na kwa kule kukirimiwa hafai kufanyiwa mambo kama ya kumkata isipokuwa kunapokuwa na dharura au kumfanyia lolote ambalo litamteremsha hadhi na kumkosea.

 

Hivyo, hakuna tatizo kwa mtu kukubali kwa kutia saini makaratasi kuwa akifa viungo fulani vyake vimsaidie mtu mwengine ambaye ni muhitaji ili kumuokoa na maradhi aliyonayo.

 

Ama Muislamu kupatiwa kiungo na asiyekuwa Muislamu au kinyume chake yote yakubalika kishari’ah bila ya tatizo lolote lile.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share