Kujumuisha Swalaah Akiwa Kazini Sababu Hakuna Sehemu Ya Kuswali

SWALI:

 

Assalam alaykum,

kuna dada angu yupo uingereza anafanya kazi sehemu moja ambayo haina sehemu ya kusali kuanzia saba na nusu mchana mpaka saba ya usiku, swala ya adhuhur inamkuta nyumbani kwa iyo anapata kusali, swala zilobaki hua kazini kwa hiyo anaamua asali safar sala ya laasir na magharib baada ya kusali adhuhur na akirudi anamalizia ishaa, suali langu ni kwamba hivi anavosali inakubalika? Na kama haikubaliki anatakiwa kufanya vipi?


 

JIBU: 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuchanganya Swalah.

Hakika ni vigumu kusema inawezekana kufanya hivyo au haiwezekani bila ya kujua anakofanya kazi na sehemu anayoishi. Ikiwa anafanya kazi katika mji anaoishi itakuwa haifai kwake kuchanganya Swalah na kuswali safari, kwani si msafiri. Kadhalika kuchanganya Swalah ya Alasiri na Magharibi kwa pamoja ni jambo halipo kishari’ah. Huchanganywa Adhuhuri na Alasiri, na Magharibi na ‘Ishaa pamoja. 

Katika hali hiyo inatakiwa yeye awe ni mwenye kuomba ruhusa apewe dakika tano kuswali Swalah ya Alasiri kwa wakati wake na Magharibi kwa wakati wake. Na hizo si nyingi tukifahamu kuwa huwa tunachukua dakika kadhaa za kula na pia kwenda haja. Hivyo kama ni mwenye Niyah ya kutaka kutekeleza Swalah kazini, basi ataweza. Lau kama anaogopa watu wasimwone akiswali au kuomba rukhsa ya kuswali, basi hilo ni tatizo kubwa katika Uislamu wake na inabidi ajitazame tena Uislamu wake. 

Pia anaweza wakati wa Swalah ya Magharibi baadhi ya nyakati akachanganya na ‘Ishaa kwa dharura kama hiyo kwani akiwa anarudi saa sababu na nusu alfajiri, hapo Swalah ya ‘Ishaa nayo itakuwa imeshampita. Swalah ya ‘Ishaa ni hadi katikati ya usiku na si hadi asubuhi kama wanavyoelewa wengi.

Lau atakuwa anatoka mji mwengine basi ataruhusika kuswali Swalah za safari hivyo kuchanganya na kufupisha. Lakini hatoweza kuchanganya Adhuhuri na Alasiri akiwa nyumbani kwani atakuwa hajaanza safari. 

Tunamshauri afanye juhudi za makusudi kabisa za kuweza kutafuta rukhusa kazini za dakika chache za kuweza kutekeleza ‘ibaadah hiyo adhimu. Anaweza hata akagawa mapumziko yake mara mbili akawa anachukua nafasi hiyo kwa kuswali Swalah hizo. Na hilo ni jepesi, linawezekana, na linakubalika makazini sehemu nyingi za Ulaya.

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi: 

 

Vipi Kukidhi Swalah Kama Shida Kuswali Kazini?

 

Hapati Kuswali Kwa Wakati, Kila Siku Anakidhi Swalah

 

 

Swalah Zote Zinanipita Kwa Ajili Ya Kazi Ni Sawa Kuzikidhi?

 

 

Kuakhirisha Na Kujumuisha Swalah

 

 

Vipi Kukidhi Swalah Zilizopita?

 

 

 

Anaweza Kulipa Swalah Ya Magharibi Kila Siku Inayompita?

 

  

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share