Kufanya Biashara Ya Kuuza DVD Na Picha Zenye Maasi

SWALI:

Asalaam Alaykum Warahmatul Laahi Wabarakatu ama baad

Ni mpenzi wa makala yenu na jitihada zenu za ki-daawa, lakini ninayo

masikitiko yangu kuhusu kucheleweshwa majibu yangu mara nyingi ninapouliza maswali huwa sijibiwi sijui kama nimekoseeni na majibu yangu ni ya msingi kabisa, lakini hata hivyo nakutakieni kila la kheri na afya na mzidi

kuwaelimisha waislaam popote pale walipo na Inshaala Allaa atakuzidishieni

neema zaidi kwa kazi zenu nzuri mnazofanya, ila tu swali langu kwa hii leo

nauliza kama ifuatavyo.

Mimi biashara yangu ya kuuza vitu vingi tu, ila kuna biashara moja ya

kuuza DVDs movies na ambazo ni comedy, wrestlers, catoons na wildlife

movies, lakini mara nyingine nauza hizi za action movies ambazo zina lugha

chafu na mara nyingine zina mambo ya kubusiana na mengineyo sasa ninaweza kuendelea na biashara hii.

 

Jazakat Laah Kher.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukurani kwa swali lako la kuhusu kuuza DVDs’ na picha zenye maasi. Hakika biashara kama hiyo haifai na inapasa ujiepushe nayo kwani hazina manufaa au mafunzo ya kumfaa Muislamu na Akhera yake. Juu ya hivyo zina mambo ya haraam ndani yake, hivyo basi itakuwa kila anayezitazama atajichumia dhambi, na dhambi hizo zitarudi kukurundikia wewe uliyesababisha. Na chumo lako litakuwa ni la haraam.

 

Hata hizo zingine ulizotaja zote pia ni masuala ya kupumbaza na kuburudisha na yasiyo na manufaa yoyote katika Diyn wala kumzidishia Muislamu Iymaan.

 

Tunakushauri utafute biashara nyingine isiyo na utata ambapo utapata rizki yako ya halaal na pia utamridhisha Mola wako. Na kama unataka kuuza video au biashara yako ndio hiyo basi ni bora uuze video za mafunzo ya Diyn.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share