Kumkosea Aliyekwishafariki - Afanyeje Kurekebisha Makosa? Je Amtolee Sadaka?

SWALI:

 

ASALAM ALEYKUM. SWALI LANGU NI MIMI NATAKA KULETA TOBA KOSA NILILOMKOSEA MTU NA MOJA KWA MOJA LINAINGIA KUANIMEMKOSEA ALLAH VILEVILE. JE? NAWEZA KULETA TOBA KWA, ALLAH BILA YA KUMUELEZEA YULE MTU NILIE MKOSEA .MAKOSA NILIO MKOSEA KWA KUOGOPA FITNA?  

ASSALAM ALEYKU WARAHMATULLAHI WABARAKATU, SWALI, KUNA MWENZANGU NILIMKOSA MAKOSA MAKUBWA. NA KWA BAHATI MWENZANGU AMESHAFIKA MBELE YA HAKKI, NA YEYE KWA UPANDE WAKE ALINIKOSEA LAKINI SIO KAMA MIMI, MAKOSA MAKUBWA NILIFANYA MIMI, NA SASA NAJUTA MAJUTO MAKUBWA, SASA KWA SABABU MIMI BADO NIPO HAI, MIMI NIMEMSAMEH KWA KILA HALI SASA, YEYE HATUKUWAHI KUSAMEHEYANA, WAKATI WA UHAI WAKE,  SASA NIFANYE NINI? NA JE NAWEZA KUMTOLEA SADAKA, IKAWA NIFIDIA YA MAKOSA YANGU? NA NIKATIA NIA THAWABU ZA SADAKA HIO ZIMWENDEE YEE. NAWEZA KUPATA SALAMA, KWA ALLAH? GHADHABU ZA ALLAH, NAZIOGOPA NA SIZIWEZI NAOMBA NASAHA ZENU


 

JIBU: 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kuomba msamaha kwa kosa ulilomkosea mwanaadamu mwenzio.

Hakika ni kuwa toba ina masharti yake na ni lazima yatimie yote ili upate samehewa. Ikiwa umemkosea mwanaadamu masharti yake ni 4, kama yafuatavyo:

 

1.     Kujiondoa katika maasiya.

2.     Kujuta kufanya maasiya hayo.

3.     Kuweka azma ya nguvu kuwa hutarudia tena kosa hilo.

4.     Na kuomba msamaha kwa uliyemkosea.

 

Ikiwa uliyemkosea bado yuko hai utakuwa huna budi ila kumwomba msamaha. Hii ni kwa ajili tusiwe ni wenye kuwakosea watu bure bure hivyo kukufanya ufikirie mara dufu kabla ya kumkosea mwanaadamu mwenzio.

Lakini ikiwa kwa kuhofia kumuomba msamaha aliye hai kutazua matatizo zaidi na balaa, basi ni vizuri kumuomba Allaah msamaha na pia kumuombea mazuri huyo uliyemkosea na kumfanyia wema ikiwezekana. 

Ikiwa amekufa kabla ya kuomba msamaha kwake itabidi uwe unamuombea du’aa kila uchao kwani du’aa zinakuwa ni zenye kuwafikia waliokwenda mbele yetu kaburini. Pia unaweza kutoa Swadaqah kwa niaba yake na pengine kuisaidia familia yake kwa njia moja au nyingine kutegemea uwezo wako.

Na InshaAllaah Allaah Aliyetukuka Atakusamehe kwani Yeye ni Mwingi wa Kusamehe.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share