Mume Hapendi Kulala Chumba Kimoja Na Mke, Je Mke Astahimili Au Afanyeje?

SWALI:


Asalaam alaikum

Mimi nina swali langu naomba mnisaidie nina mume wangu na katika ndoa yetu kuna matatizo kwa muda mrefu tangu tuoane ni miaka 8, kuna tatizo limeanza zamani kuwa mume wangu yeye hapendi kulala chumba kimoja na mimi inafika miezi 2 or 3 bila kuwa pamoja sasa kidini hii itakuaje ndoa yangu? Nikimwambia anatoa ukali anasema nimuache sasa mimi nataka kujuwa nimestahmili mpaka sasa je ndoa hii bado inaswihi?

Salaam alaikum.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mume kutopenda kulala chumba kimoja nawe (mkewe).

Kusoma tu hili swali lako inaonyesha kuwa mume wako ana matatizo ambayo ameshindwa kuyatatua na hataki kukuambia wewe. Hakika ni kuwa katika sheria yetu ya Kiislamu haifai kwa mume kulala kando na mkewe. Na hata wakati ambapo mke ana makosa na sheria imemruhusu kujitenga ne mkewe lakini inafaa iwe kwenye kitanda kile kile lakini asifanye naye mapenzi.

 

Hata hivyo, kulingana na maelezo yako inaonyesha mumeo ana matatizo na hataki kuyatatua lakini wewe usivunjike moyo inatakiwa umshauri ili apate tiba. Inatakiwa mwanzo umshauri aende kwa Shaykh apate ushauri nasaha kwa yale aliyo nayo.

 

Kawaida mke anamjua mumewe kwa aliyo nayo na mengineyo. Ikiwa amekataa kuchukua ushauri wako inatakiwa uzungumze naye kwa wakati unaofaa, akiwa ametulia na kisha kwa upole, hekima na njia nzuri. Huenda kwa hilo akarudi nyuma na kurudi aliyokuwa akifanya hapo awali. Ikiwa hukufanikiwa katika hilo itabidi uitishe kikao baina yako wewe, yeye (mumeo), wazazi au wawakilishi wako na wake. Na katika kikao hicho unatakiwa uwe wazi kabisa kwa yale unayoyapata kutoka kwa mumeo ili mpate suluhisho kwa tatizo hilo. Ikiwa kwa njia hiyo pia hukufaulu itabidi upeleke kesi yako mbele kwa Qaadhi au Shaykh mwenye elimu, muadilifu na mcha Mungu ili awasuluhishe kwa mliyo nayo. Hapa ndio kilele cha kadhiya yenu na hapo itajulikana hali halisi. Ikiwa mume kweli anakutaka basi atajirekebisha au ataamua kuwa hakutaki, kwa hivyo akupe talaka.

 

Ujue kuwa mpaka sasa wewe ni mke wake, unatoka tu katika unyumba ikiwa mume atatamka kuwa amekupa talaka au hakutaki tena.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share