Nani Wa Kuulizwa Juu Ya Kuzorota Hali Ya Ummah?

 

Nani Wa Kuulizwa Juu Ya Kuzorota Hali Ya Ummah?

 

Alhidaaya.com

 

Makala hii ni muhimu sana katika zama kama hizi ummah wetu wa Kiislam umezorota na Dini yetu ya Kiislam inaweka aibu kwa jinsi imevyozorota. Lengo la muandishi ni kutaka ujumbe huu umfikie kila Muislam, mkubwa, mdogo, shaykh, maamuma, tajiri, maskini na Waislamu wengine wote ili kila mmoja wetu ajihisi kuwa yeye ni sababu mojawapo ya kuzorotesha hali ya ummah huu.

 

 

Hali ya ummah wa Kiislam umebeba kila sampuli ya udhalili na kasoro, ummah wa Kiislam umekuwa ni ummah wenye kutia aibu na kusikitisha, ummah wa Kiislam umekuwa ni ummah wenye kila aina ya uharibifu na dharau kutokana na kuzorota kwake.

 

 

Ikiwa mtu atachunguza kila aina ya kasoro na udhaifu basi kasoro na udhaifu huo atautoa katika ummah wetu huu wa Kiislam. Yeyote ambae atakayeangalia majumba yanayovunjwa ni yakina nani, basi bila shaka ukubali usikubali ni majumba ya Kiislam. Ukiangalia damu nyingi zinazomwagwa ni za kina nani, bila shaka ni damu za Waislam. Ukiangalia akhlaaq kuharibiwa, basi ni akhlaaq za Waislam. Ukiangalia jamii zenye malumbano, kusengenya na kufitiniana, utakuta ni jamii za Kiislam, na kila sampuli zingine za udhaifu basi utakuta ni majumba na jamii za Kiislam. Na sidhani kama kuna mwenye kupinga hili au kuna ambaye haoni hali hii, sote tunajua kuwa hali hii imetusibu na sidhani kuwa kuna ambaye kishajifikiria siku moja ni jinsi gani ya kutatua tatizo kama hili kadiri na uwezo ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliyomuwezesha.

 

 

Baada ya kuona kasoro na udhaifu wote huu, swali linalojitokeza ni ”Nani mwenye kuulizwa juu ya kuzorota hali ya ummah?” Mas-uliyah ni ya nani? Tumlaumu nani kutokana na hali hii?

 

 

·    Iwapo utamuuliza Muislam yeyote swali kama hili, bila shaka utapata majibu kama yafuatayo. Baadhi yetu tunadai na kuamini kuwa, hali ya kuzorota kwa ummah huu majukumu ni viongozi wa Kiarabu, kwa kuwa wao ndio viongozi, wao ndio wenye dola za Kiislam, wao ndio wenye hili na lile.

 

·     Baadhi yetu wengine tunadai kuwa hali ya kuzorota kwa ummah huu, majukumu ni ya ’ulamaa na Mashaykh kwa kuwa wao ndio warithi wa Rusuli na Manabii.

 

·    Baadhi yetu wengine tunadai kuwa hali ya kuzorota kwa ummah huu, lawama ni kwa matajiri wa Kiislam kwani wao ndio wenye kuweza kuusaidia ummah huu kutokana na mali zao.

 

·    Na baadhi ya Waislam wengine humlaumu huu na yule kwa sababu hii na ile, basi kwa kifupi ni kuwa kila Muislam humlaumu mwenzake na kila mmoja wao hutoa sababu hii na ile.

 

Kinachouma na kusikitisha sana, ni kuwa humpati Muislam yeyote isipokuwa utamsikia akisifia hali ya kuzorota kwa ummah huu akisema hili na lile na kwa sababu hii na ile. Linalostaajabisha ni kuwa mtu huyo atasifia hali ya kuharibika kwa ummah huu kana kwamba yeye si miongoni mwa Waislam hao.

 

 

Ndugu zangu Waislam, ubishi huu na lawama hizi hazitotufikisha popote wala kusaida lolote, kinyume cha kutafuta njia au suluhu ya kutatua janga kama hili tumekaa na kurushiana lawama. Wa kukuuliza kama Muislam, wewe umefanya au kuchangia nini katika ummah huu? Wewe umetanguliza nini kuusaidia ummah huu? Jua ya kwamba, kadiri unavyozidi kusifia hali ya udhaifu ya ummah huu ndio kuzidi kuuponda ummah huu na kuurudisha nyuma, na huenda ukawa miongoni mwa wale wanaoupiga vita ummah huu na kuuponda kwa kashfa zako pasina kujua ulifanyalo.

 

 

Hebu turudi katika suluhisho la ummah huu kwa kutumia Qur-aan na Sunnah na tumuulize kipenzi chetu Muhammad (Swala Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) swali hili ambalo kila umoja wetu anajitahidi kujitoa katika jukumu kama hili na kumtupia kosa huyu na yule kana kwamba yeye hahusiki.

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi sallam) Anajibu swali hili kwa kusema katika Hadiyth yake mashuhuri:

 

"Ee! Jueni ya kwamba nyie nyote ni wachunga na kila mmoja ataulizwa alichokichunga, kiongozi wa watu ni mchunga na ataulizwa kwa alichokichunga, na mwanamme ni mchunga wa familia yake na ataulizwa kwa alichokichunga, mwanamke ni mchunga wa nyumba ya mume wake na watoto wake naye ataulizwa alichokichunga, na mtumwa ni mchunga wa mali ya bwana wake naye ataulizwa kuhusu uchungaji wake" Imepokewa na [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Natumai kuwa Nabiy (Swala Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth hii hakutumia lugha ngumu sana isiyoeleweka. Kajibia swali hili wazi kabisa na kila yule mwenye akili na kuzingatia ameelewa wajibu wake ni upi katika Dini/ummah huu bila ya kuhitaji kufasiriwa.

 

 

Kama Nabiy (Swala Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anavyotwambia kuwa sote ni wachungaji, na kila mmoja wetu ataulizwa kwa kila kile alichokichunga. Hajasema kuwa mchungaji ni viongozi wa Kiarabu, wa Kiafrika, Shaykh, tajiri,… isipokuwa kaweka wazi jibu kwa kusema kuwa mimi na wewe sote ni wachungaji na sote tutahojiwa kwa kila kile tulichokichunga.

 

 

Kwa hiyo, ndugu yangu Muislam, tambua ya kwamba. Kuzorota kwa hali ya ummah huu majukumu ni yako wewe na mimi, na sote wawili tumeshiriki kuuponda ummah huu. Usishangae nikikwambia ya kuwa wewe nami tumeshiriki kuzorotesha ummah huu, kwa kuwa mimi nitakuuliza swali wewe kama Muislam, kuzorota au kuharibika kwa ummah si watu kuacha maamrisho (Twa'aa) ya Allaah na kumtii Shaytwaan ndiko kunapelekea kuharibika kwa hali ya ummah? Ikiwa jibu ndio, hao wanaokwenda kinyume na maamrisho ya Allaah si wanatoka katika majumba yetu na tunaowalea ni sisi wenyewe? Itakuweje yule uliyemlea chini ya misingi ya Qur-aan na Sunnah na malezi ya Nabiy wetu Muhammad (Swala Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aje kutokea kuwa mvuta bangi/sigara, au mlaji mirungi? Aje kutokea kuwa mkosefu wa adabu? Aje kutokea kuwa tapeli? Aje kutokea kuwa na tabia na maadili ya kinaswara kiyahudi au kikafiri kwa ujumla?

 

 

Hapa unaona moja kwa moja kuwa lile jukumu lenu ambalo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alilowapatia baba na mama kama viongozi katika nyumba, hamkujua umuhimu wake na madhara yake, ndio haya leo unaona ummah wetu umezorota. Lengo kubwa wazazi mmeacha majukumu yenu na kuthamanisha vingine zaidi ya malezi ya mtoto. Iweje leo wewe ndio wa kwanza katika kulaumu na kusifia hali ya udhaifu ya ummah wa Kiislam hali ya kuwa nyumba yako mwenyewe imekushinda kwa kuishi kama iamrishavyo Qur-aan? Unataka Mashaykh na Maustaadh waje kurekebisha hadi nyumbani kwako kwa mke na watoto wako? Jua ya kwamba udhaifu wa imani yako wewe na familia yako ndio umesababisha kuzorotesha kwa hali ya ummah huu na kuurudisha nyuma.

 

 

Kabla ya kutaka Qur-aan ije kutawala katika jamii ingelipaswa kwanza mtu atawale kwake kwa mkewe na familia yake.

 

 

Suluhu la ummah huu haliwezi kupatikana katu endapo Waislam tutaendelea kuwa kama tulivyo hivi leo, kinachotakikana ni kila Muislam ahisi kwanza yale majungu ya kuwa na yeye ni miongoni mwa waliyozorotesha ummah huu, kisha baada ya hapo ndugu yangu Muislam jiamini ya kwamba mimi naweza kuleta mabadiliko katika ummah huu. La kufuatia baada ya hapo ni Waislam tushikamane na kuleta mabadiliko kwanza katika majumba yetu kabla ya kutoka nje. Kisha mabadiliko katika jamii.

 

 

Kwa mfano mimi na wewe tuna familia, kisha kila mmoja wetu aanze kuirekebisha nafsi yake, baada ya hapo aende kurekebisha ahli zake nyumbani. Tuchukue wewe una familia ya watu 15 na mimi nina familia ya watu 15, AlhamduliLlaah wote 30  wakaelekea kwenye njia sahihi wakatengemaa na kuwa sawa, na baadhi yao wakaenda kwa marafiki zao na kuwafanyia haijatengemaa au imeshatengemaa? Jibu ni kuwa imeshatengemaa kwani hao thalathini ndio watakaokwenda na kutengeneza wengine, kisha hao wengine ndio wende na kuwaweka sawa wengine zaidi. Kadiri ya watakavyoongezeka na kwenda wanafanyiana da’awah ndio mujtamaa utakavyokuwa na nguvu na kutengemaa.  Acha fikra mbovu ya kufikiria kuwa mi peke yangu naweza kuleta mabadiliko kwenye jamii, ndio unaweza ikiwa utaamua kufanya mabadiliko na kujua umuhimu wa unachokifanya.

 

 

Suluhu Na Mafanikio Ya Ummah Huu. 

 

Baada ya kusoma kwa makini na kuelewa kuwa uzoroteshaji wa hali ya ummah huu, chanzo ni mimi na wewe, kwa hiyo kinachofuatia sasa ni vipi tutasimamisha ummah huu juu? Vipi mimi na wewe tunaweza kuleta mabadiliko katika ummah huu? Tukishakuwa na niyah na lengo hilo, swali la kufuatia  ni hili ”tuanzie wapi?”.

 

 

Mimi na wewe tunaweza kuuokoa ummah huu na kuleta mabadiliko makubwa ikiwa tutaamua kufanya hivyo na tutafanya hivyo kwa ikhlaasw. Ummah huu tunaweza kuufanya kama Allaah Alivyotubainishia ndani ya Qur-aan na kuurudisha kama ulivyokuwa zama za Swahaba, ummah wa nguvu uliokuwa ukitikisa kama Allaah Anavyosema ndani ya katika aayah Qur-aan 48:29, Ummah Bora 3:110, Ummah wa wasitani 2:143 na sifa kem kem za kuonyesha utukufu na ubora wa ummah huu wa Muhammad (Swalla Allaahu Alayhi Wasalam), kwa masikitiko makubwa imekuwa kinyume chake ummah wetu huu hauna nguvu wala hautikisi tena na umezorota na chanzo ni mimi nawe kwani Allaah Hana sifa ya kudanganya (Na’udhu biLlaahi min dhaalika), sikiliza Anavyosema ndani ya Qur-aan:

 

وَلَا تَهِنُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَنتُمُ الْأَعْلَوْنَ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٣٩﴾ 

Na wala msilegee na wala msihuzunike na ilhali nyinyi mko juu mkiwa ni Waumini. [Aal- ‘Imraan :139]

  

Ukisoma Aayah hii utaona Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) Anasema kuwa ”kwani nyinyi ndio wa juu mkiwa ni Waumini” kwa hiyo, sharti hapa ya sisi kuwa juu na kushinda, vipi sisi ikiwa tutakuwa Waumini wa kweli, yaani turudi katika mafunzo ya Allaah na tushikamane na yale Aliyo Amrisha na kuacha yale Aliyokataza. Hapo tutakuwa juu na kuutawala ulimwengu huu na kufaulu kuanzia hapa duniani na huko Aakhirah (Aamiyn).

 

 

Jambo la pili, ni kuwa, tunahitaji Waislamu watakaojitolea kwa ajili ya Allaah katika kutenda na si kuongea tu na kulaumu kama tunavyofanya wengi wetu. Ikiwa tutajitolea na kuamua kutenda na kumtegemea Allaah pekee basi tutaleta mabadiliko makuwa sana katika ummah huu na utakuwa juu siku zote.

 

 

Jambo la tatu, ni Waislamu tuwe tuwe kitu kimoja na tushikamane, Aayah za kuhimiza umoja wa Waislam na kuepukana mafarikiano ni nyingi sana katika Qur-aan. Kwa hiyo, ikiwa tutakuwa kitu kimoja na tukawa na kauli moja basi tutaweza kusonga mbele. Na iwe ni umoja wa kweli, umoja wa ’Aqiydah moja na wa kuifuata hii Dini kama tulivyoipokea kwa Nabiy wetu na Swahaba zake na wema waliotangulia, na si umoja wa jina lakini ’Aqiydah tofauti na wengine wana mapenzi na walioileta Dini hii kwetu na wengine wana chuki nao; wengine huombea radhi, wengine hulaani na wenye visasi; wengine hukubali Aayah za Allaah na mafunzo ya Nabiy kama yalivyotufikia na wengine hupindisha na kugeuza na kubadilisha maana ili iendane na matamanio ya nafsi zao na itikadi zao. Umoja huo hauwezi kufanikiwa. Bali umoja unaotakikana ni umoja wa Kalimah na ’Aqiydah sahihi iliyosalimika ya wema waliotangulia.

 

 

Na mwisho, Waislam tupendane, tuhurumiane, tusaidiane na tupeane nguvu/moyo kwa kila yule mwenye kujitolea na kufanya jambo jema lenye faida na jamii yetu ya Kiislam. Tumpe nguvu na kujiunga na kila yule mwenye niyah ya kuleta mabadiliko katika jamii ya Kiislam. Badala ya kumponda na kumvunja nguvu.

 

 

Namalizia kwa kukariri mara nyingine kuwa, wewe na mimi tutaulizwa hali ya kuzorota kwa ummah huu kadiri na ule uwezo ambao Allaah Kakuwezesha, Kadiri na kile cheo ambacho Allaah Alikuruzuku.

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu Wa Ta'alaa) Atujalie kuwa miongoni mwa wale watakaotenda kwa manufaa ya jamii na ikhlaasw ya hali ya juu katika kuleta mabadiliko katika ummah huu.

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) Atujalie kuwa miongoni mwa wale wenye kuweza kuleta mabadiliko ya hali ya juu. Wale wenye kuishi na kufikiria mbinu gani za kutumia katika kuleta mabadiliko, wale wenye kuishi kwa ajili ya manufa ya jamii ya Kiislam. (Aamiyn Yaa Rabal 'Aalamiyn).

 

Share