Mume Anawasikiliza Sana Wazazi Wake Na Kuna Mvutano Baina Ya Mke Na Wakwe

 

Mume Anawasikiliza Sana Wazazi Wake Na Kuna Mvutano Baina Ya Mke Na Wakwe

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam Alaikum,

 

Allah awajaze kila la kheri katika kazi hii munaoifanya.nami nafurahi sana kupata elimu kutoka kwa mtandao huu.

 

Swali langu ni hili:mume humwamrisha mke wake afanye kama wazazi wanavyo taka. Mume huyu hana rai inaotoka kwake, anaogopa sije akawaudhi wazazi wake na huku mke nae hataki kufuata kwa kuwa anaona jambo hilo si sawa. Inakuwa mvutano kila siku katika ndoa yao. Kwa mfano mke anataka mtu fulani akaoshe gari. Huku wazee nao wanataka mtu mwengine akaoshe gari. Mke atamweleza mumewe kuwa huyu atasafisha gari vizuri lakini mume nae hatomsikiza. Atafanya kama anavyoamrishwa na wazazi wake. Mke kama huyu afanyeje ili asilete mvutano.

shukran

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Baada ya kusoma swali la muulizaji hatuoni kwa nini kuwe na mivutano. Mivutano baina ya mume na mke inawezekana kuwepo tu ikiwa mume anamuamrisha mkewe amuasi Allaah Aliyetukuka au awache ya halali au kumuamrisha kufanya ya haramu.

 

 

Inavyotakikana ni kuwepo na hali nzuri kabisa ya wanandoa kwa kuweza kushirikiana na kushauriana katika mambo yao. Na pindi wanapofanya hivyo basi wahakikishe wanafanya juhudi kuyatekeleza hayo kwa njia iliyo nzuri. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ 

Na jambo lao hushauriana baina yao.. [Ash-Shuwraa: 38].

 

 

Hata hivyo, ikiwa ni mambo ya kuosha gari, hatuoni kama ni ams-ala ya kukukera na kukushughulisha hivyo, ni bora ili kuepusha kuvutana na mumeo ni kuamua kumuachia shughuli hiyo mumeo ili muweze kuishi pamoja kwa hali ambayo ni nzuri kabisa. Ikiwa kijana anayetumwa na mama mkwe wako anaimudu hiyo kazi wacha iwe hivyo na ujira wako kwa Allaah Aliyetukuka utakuwa mkubwa kwa kudumisha uelewano na utulivu ndani ya nyumba.

 

 

Ikiwa kuna matatizo makubwa kuliko hilo unaweza kufuata mfumo ufuatao:

 

1.     kuzungumza na mumeo wakati wa faragha yenu kwa upole, ulaini, na maneno matamu ili msaidiane katika kudumisha wema.

 

2.     Ikiwa hakuna natija iliyopatikana basi itabidi uitishe kikao baina yenu na wawakilishi wenu wenye busara wa kuweza kutatua tatizo ikiwa ni wazazi wenu nyote wawili au jamaa zenu.

 

3.  Ikiwa tatizo halikutatulika basi itabidi uende kwa Qaadhi au Shaykh mwaminifu ili mtatuliwe hilo.

 

Katika kila hali ikiwa hamtoweza kusikilizana na mume kwa mambo ambayo ni madogo huenda yakawa makubwa na mkashindwa kuishi pamoja. Mume ana makosa ikiwa hawezi kukusikiliza hata kwa jambo ambalo ni dogo lililo sawa. Inabidi apate ushauri na nasaha wa kuweza kudumisha utiifu kwa mama na vile vile kuyapeleka maisha ya nyumbani kwako kwa njia iliyo bora.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share