Mume Amemuacha Baada Ya Kuzaa Anadai Sababu Anadharau Wazazi Wake

SWALI:

 

Assalam Aleykum.

 

Shukran sana kwa kupata nafasi kama hii ya kuweza kuuliza na kujibiwa katika sheria za kiislam.

 

SWALI: Mimi ni mwanamke wa kiislam, mume wangu alisafiri nje ya nchi siku ya 5 tu baada ya mimi kujifungua. Kwa hio basi aliniacha me nikiwa katika arobaini na mtoto akiwa na siku 5. Tulikua tukiwasiliana mara kwa mara. Tarehe 18 mwezi huu saa tatu usiku alimpigia simu baba yangu na kumwambia kua mimi na yeye basi tena. Baba yangu alimuuliza kwa nini akasema kua sababu ni nyingi sana ila sababu kuu ni kua mimi simpeki mtoto mara kwa mara kwao, pia nawadharau wazee wake kitu ambacho kwangu si cha kweli. Na amesema yeye hupata taarifa zangu zote kwa sababu anapiga simu kwao na kuuliza.

 

Ndugu zangu wa kiislam je mnanishauri nifanyeje na yeye hataki kuskia hata maneno ya wazee wangu? Na jee natakiwa kukaa eda? Shukran.

 

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kupewa talaka na mumeo.

Hakika ni masikitiko makubwa kuwa mume amechukua hatua kama hiyo nzito bila ya kuketi nyote pamoja na kujadili hayo. Kwa kuwa sasa ushaachwa inafaa uanze kuhesabu siku zako za eda.

 

Wakati huu wa eda mnaweza kurudiana bila ya Nikaah wala mahari mapya. Mambo ambayo yanaweza kufanyika kwa sasa ni kama yafuatayo:

 

1.      Ni nyinyi kutafuta njia ya kuweza kuwasiliana naye na kumuelezea hali halisi ya mambo yalivyo.

 

2.      Ikiwa hilo linaonekana halitoi natija basi ni wazazi wako waende kwa wazazi wa mume wajaribu wazungumze nao. Au pia muwatume watu ambao wanaweza kuelewana na wazazi wa mumeo ili wawakinaishe na kuwapatia maelezo sahihi ya kutaka suluhu na ndoa kuendelea.

 

 

Ikiwa yote yatashindikana, na eda yako ikimalizika utakuwa tayari kuolewa na mume mwengine. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Amlainishe mumeo na wazazi wake waweze kufahamu na kurudi na kurekebisha mambo kwa haraka iwezekanvyo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share