04-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu 'Anhu) - 1

 

 

 

1. Abu Bakr As-Swiddiyq Aliyebashiriwa Pepo.

 

 

Linapotajwa jina la As-Swiddiyq tunapata tafakuri ya watu wenye mwenendo na maadili mema. Moyo utachangamka na kuvutiwa na As-Swiddiyq (mkweli).

 

Abu Bakr As-Swiddiyq alikuwa rafiki wa Mjumbe wa Allaah Muhammad tokea ujana wake mpaka alipozeeka. Alikuwa mwenza mwaminifu wakati wa raha na wakati wa shida. Alikuwa akiitwa ‘mwaminifu’ ambaye alimwamini Mtume wakati wengine wakimpa mgongo (wakimkana). Imani yake ilikuwa thabiti, na alifahamika kwa umbuji wa lugha na kwa kuamiliana vizuri na watu. Alifahamika sana kwa ukarimu wake; na utajiri wake ulikuwa wa jamii ya waumini.

 

Ilikuwa heshima kwake kwa Allaah kuteremsha aya hii;

“Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume , basi Allaah Alikwishamnusuru walipomtoa waliokufuru, naye ni wa pili katika wawili walipo kuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: Usihuzunike. Hakika Allaah yu pamoja nasi. Allaah Akamteremshia utulivu Wake, na Akamuunga mkono kwa majeshi msioyaona, na akalifanya neno la waliokufuru kuwa chini, na Neno la Allaah kuwa ndilo juu. Na Allaah ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima.” (9: 40).

 

Kisa cha Hijrah na siku walizokaa pangoni ni mfano wa somo lililoonesha usuhuba unavyoweza kuwa na nguvu.

 

Alikuwa kiumbe wa Allaah aliyependwa sana na Mjumbe wa Allaah na alielezewa kama ifuatavyo:

“Alikuwa dhaifu kimwili lakini mwenye nguvu katika mambo ya Allaah , alikuwa mnyofu katika nafsi yake lakini aliyetukuka mbele za Allaah . Alitukuzwa mbele za watu, na alifadhilishwa katika mioyo yao.”

 

Wanyonge waliimarishwa kwa ushawishi wake. Abu Bakr alikuwa chimbuko la matumaini wakati wa hali ngumu. Alikuwa kimbilio na mhimili wa Waislamu wakati akiishi nao. Alidharau maisha ya dunia, na akajiweka mbali na jambo lolote ambalo halikuwamo katika mafundisho ya Mtume Alikuwa msomi mashuhuri wa dini ambaye alibadilishana mawazo na watu na alikuwa mcheshi. Alikuwa na imani thabiti kuliko watu wote, alikuwa na imani safi na alikuwa mkweli sana. Alikuwa rahimu kwa kila mtu, hasa kwa Waislamu. Kulipokuwa na kukengeuka dhidi ya Uislamu alilia; na Uislamu uliposhambuliwa aliunguruma kama simba tayari kuihami dini na watu aliowapenda sana. Endapo aliyedhalilishwa ni mwanamke au mtoto au mnyonge, alikuwa wa kwanza kukusanya watu kwenda kwenye mapambano.

 

Hebu fikiri, hadhi ya Uislamu ingekuwaje kama asingewahofisha wasaliti? Ujasiri wake na ulezi wake alivifanya kuwa umoja na nguvu. Alikuwa Zaydi ya mtu wa kawaida.

 

Huyu ndiye Abu Bakr aliyekuwa mbora wa Waislamu baada ya kurejea katika Uislamu, na alibakia hivyo mpaka Allaah Alipomukhitari (Alipotwaa roho yake).

 

Ni muhali kudhukuru mema yote na uadilifu wa Abu Bakr ndani ya kurasa chache. Kwa hiyo inatosheleza kutaja sifa chache kwa matarajio ya kuwa zitawahamasisha wale wanaotafuta ukweli.

 

 

Jina Lake na Nasaba Yake

 

 

Jina lake ni ‘Abdullaah bin Abu Quhaafah, ‘Uthmaan bin ‘Aamir bin ‘Amr bin Ka’b bin Sa’d bin Taim bin Murrah bin Ka’b. Nasaba yake inakutana na ile ya Mjumbe wa Allaah kwa Murrah.

Lakabu yake ilikuwa ‘Atiyq (aliyeokolewa Motoni). Watu wana maoni tofauti kuhusiana na jina lake. Baadhi wanasema kuwa ni kwa sababu ya vitendo vyake na majadiliano na watu kwa tabia iliyotukuka. ‘Wengine wanasema ni kwa sababu ya nasaba yake sharifu, kwa kuwa hakuwa na dosari au alikuwa nazo chache. Inasemekana kuwa lakabu hiyo alipewa na Mtume .

’Aaishah alisema: “WaLlaahi, nilipokuwa chumbani mwangu na Mjumbe wa Allaah na Maswahaba wake walikuwa uani, tulitenganishwa na pazia. Abu Bakr aliingia ndani na Mtume alisema, ”Yeyote atakaye kuridhishwa kwa kumwangalia mtu aliyeokolewa na Moto, amuangalie Abu Bakr.”

 

‘Abdullaah ni jina alilopewa na wazazi wake lakini jina ‘Atiyq ndilo liliolokuwa likitumika sana. Katika baadhi ya masimulizi katika zama za jahiliya alikuwa akijulikana kama ‘Abdul Ka’bah lakini aliposilimu aliitwa, ‘Abdullaah. ’’Abdullaah bin Az-Zubayr alisema

“Jina la Abu Bakr lilikuwa ‘Abdullaah. Mtume alimwambia: ‘Umeokolewa na Moto’ Kwa sababu hiyo aliitwa “Atiyq.”

 

Mama yake aliitwa Saalima bint Sakhr bin ‘Amr bin Ka’b. Lakabu yake ilikuwa Ummul-Khayr (Mama wa Kheri) na alikuwa binamu ya baba yake.

 

 

Umbile Lake

 

 

Abu Bakr alikuwa na hali nzuri ya wastani, mwembemba, mgongo ulipinda kidogo, na alikuwa na uso mwembemba na macho makubwa yaliyoingia ndani. Paji la uso wake lilijitokeza kidogo, na alitia nywele zake hinna iliyochanganywa Katam.

 

 

Kuzaliwa  Kwake

 

 

Abu Bakr alizaliwa miaka miwili na miezi kadhaa baada ya kuzaliwa Mtume katika mji wa Makkah. Aliishi hapo mpaka alipokuwa kijana (barobaro). Hakuondoka mpaka alipoanza biashara, na kisha alihamia Madina pamoja na Mtume Alikuwa mmoja wa matajiri wa Makkah na alifahamika kwa ukarimu wake, heshima na tabia njema. Alikuwa akipendwa na watu wa jahiliya na alikuwa msimamizi wa diya na madeni.

 

Hali ilikuwa hivyo kwa sababu Maquraysh hawakuwa na mfalme wa kuwatawala. Kila kabila ilikuwa na kiongozi ambaye alitawalia mambo yao. Mathalan Banu Hashim walikuwa na jukumu la kuwapa mahujaji chakula na maji. Banu 'Abdid-Daar walikuwa na jukumu la kuangalia mambo mengine yaliyohusu utunzaji wa Ka’bah (Nyumba ya Allaah Hapana mtu aliyeruhusiwa kuingia ndani ya Ka’abah bila ruhusa ya Banu ‘Abdud-Daar.

 

Kuibeba bendera wakati wa vita lilikuwa jukumu lao pamoja na Darun–Nadwah (mahala Maquraysh wakikutana kujadili masuala muhimu).

 

Abu Bakr alijishughulisha sana na biashara zake. Akiutumia vizuri muda wake na hakupoteza muda wake kufanya mambo yasiyo na maana. Ambapo wengine wakinywa pombe au wakijishughulisha na ufisadi, uzinzi na madhambi mengine. Abu Bakr alikuwa mwanaume aliyejipambanua kwa daraja na hadhi.

Abu Bakr aliona faraja kuwa na kijana kama yeye ambaye alikuwa na maadili mema. Mtu ambaye aliyeacha kuabudia masanamu, asiye kunywa pombe na ambaye hakupoteza ujana wake katika ufedhuli. Kijana huyo alikuwa Muhammad bin ‘Abdillaah bin ‘Abdul-Muttwalib ambaye Abu Bakr alimwona kuwa rafiki bora. Vivyo hivyo Muhammad aliona kwa Abu Bakr yaliyomfanya awe karibu naye na kumpenda. Jamii ilipendezewa na usuhuba wao. Abu Bakr aliutumia muda wake na mapumziko kujifunza koo za makabila ya Kiarabu mpaka akawa mjuzi wa tawi hili la elimu mpaka akawa bingwa wa nyanja hii.

 

 

Kurejea Kwake Kwenye Uislamu

 

 

Haishangazi Abu Bakr kuwa mtu wa kwanza kusilimu, na pia sio ajabu kuwa alikuwa wa kwanza kumwamini Mjumbe wa Allaah .

Kuna mambo mawili yaliyomfanya Abu Bakr kuharakisha kuukubali Uislamu.

  • Kupenda mambo mazuri, na
  • Urafiki wake na Mjumbe wa Allaah .

Abu Bakr alikuwa na wema wa asili ambao uliwafanya watu kutenda mema. Alijiepusha na yale mambo ambayo yangechafua hadhi yake.

 

Moyo wake ulikuwa sawa na ardhi yenye rutuba ambayo inatoa matunda mengi. Maji yalitononeshwa na busara za Uislamu ambazo aliamua kuzifuata. Uislamu ukifanya hulka yake kuwa nzuri. Kamilifu, ya ukweli, ya haki na imara. Ukarimu wake katika njia ya Allaah haukuwa na mfano. Kwa ufupi, kila tabia na mwenendo mzuri unajumuishwa katika hiba yake.

 

Mvuto mwingine uliomsukuma Abu Bakr kufuata njia ya Uislam ni urafiki wake na Mjumbe wa Allaah Muhammad. Haina maana aliamini kwa kumpendezesha rafiki yake.

 

Hapana! Hakuamini kwa sababu ya urafiki wao bali ni kutokana aliyojifunza na yaliyompendeza kwa Mtume ndiyo yaliyomkurubisha katika Uislamu na Allaah.  Aliuona Uislamu kwa uwazi, kwa sababu aliiona tabia njema ya Mtume Urafiki wake na Mtume haukuwa katika nje na wakati huo huo waliheshimiana na kusaidiana. Alimpenda Mtume na alimuona kuwa ni mshauri wake mkuu. Walipishana miaka miwili katika umri wao, na hili lilifanya wafahamiana bila kuwepo ushindani au ubandia. Naye Abu Bakr alikuwa na muda wa kumjua Mtume pia. Alifarijika kumwona kuwa ni mkweli na mwaminifu. Kwa hiyo alimtambua kuwa ni Mtume na hakuona dosari yoyote kwake. Aliona ni mfano uliokuwa unatembea katika yote aliyokuwa akihubiri kuhusu Uislamu. Kutokana na sababu hiyo haikuwa ajabu kwa Abu Bakr kuwa mtu wa kwanza kumwamini Muhammad na kumuunga mkono.

 

Muhammad alipotoa ujumbe kwa Abu Bakr akimwalika yeye na watu wengine kuyaacha masanamu yao, Abu Bakr hakusita, na alikuwa mtu wa mwanzo kusilimu. Mtume Muhammad rafikiye alifurahi sana.

 

Mjumbe wa Allaah akizungumzia kurejea kwa Abu Bakr kwenye Uislamu, alisema,

 

“Sijapata kumlingania mtu kwenye Uislamu na asiwe na wasiwasi, Abu Bakr alikuwa wa mwanzo kutokuwa na wasiwasi.”

Kuna Hadiyth nyingi zinazothibitisha ya kuwa Abu Bakr alikuwa wa mwanzo kati ya wanaume huru kumwamini Mtume kama ilivyo. Khadija alikuwa mwanamke wa mwanzo kumwamini. ‘Aliy bin Abi Twaalib  akiwa miongoni mwa vijana, na Zayd bin Haarithah miongoni mwa watumwa wa mwanzo kuingia katika Uislamu.

 

Kusilimu kwa Abu Bakr kuliunufaisha Uislamu, kwa sababu alikuwa mtu maarufu sana hapo Makkah ambaye alikuwa tajiri na aliyependwa sana na watu. Alikuwa muhubiri mzuri wa Uislamu kwa sababu watu walimheshimu, na walivutiwa sana na tabia yake. Kwa hakika maswahaba wengi walirejea katika Uislamu kupitia kwake.

Baadhi yao ni: Az-Zubayr bin Al-’Awwaam, ‘Uthmaan bin ‘Affaan, Talha bin ‘Ubaydullaah, Sa’d bin Abi Waqqaas na ‘Abdur-Rahmani bin ‘Awf . Kwa njia hii, kurejea kwa Abu Bakr katika Uislamu kuliwaleta watu wengi katika Uislamu. Waislamu lazima wawe wema na waamiliane kwa uzuri na watu wengine kama njia ya kuwavuta watu wazuri, na kunyanyapaa watu waovu kunasaidia kuepusha uovu. Ni kama fumbo la mti wenye matunda mengi ambao mizizi yake ni imara katika ardhi na matawi yake yanafikia juu mawinguni. Unazaa matunda wakati wote katika mwaka. Kinyume na hivi, ni mshikamano wa watenda maovu ambao ni kama fumbo la mti mwovu ambao hauzai chochote isipokuwa matunda mabaya yasiyolika.

 

 

As-Swiddiyq (Msema Kweli)

 

 

Alipewa jina la As-Swiddiyq (msema kweli) kwa sababu ya kutokuwa na wasiwasi wa kumwamini Mjumbe wa Allaah . Ibn Is-haaq alisema kwa mamlaka ya Al-Hasan Al-Baswriy na Qataadah, Alijulikana kwa jina hilo kwa mara ya mwanzo asubuhi ya Israa (safari kutoka Makkah mpaka Quds [Jerusalem]) kisha Mi’iraaj (kurufaishwa mbinguni). Kwa mamlaka ya Bi ’Aaishah aliyesema: “Makafiri walimwendea Abu Bakr na kumwambia, Rafiki yako amefikwa na jambo gani? Anadai ya kuwa usiku uliopita alikwenda (Quds) Jerusalem (na akarejea usiku ule ule)” Akauliza? Amesema hivyo? Wakasema, ‘Ndiyo’. Abu Bakr akawambia: Amesema kweli, na ninaamini ufunuo atakao kuja nao kutoka mbinguni. Kwa hiyo kutokana na msimamo huo aliitwa As-Swiddiyq.”

 

Kuna Hadiyth nyingi zinazothibitisha kuwa Jibriyl na Mtume walimpa jina hili. Kwa mamlaka ya Abu Hurayrah aliyesema: “Mjumbe wa Allaah alipofika Dhi Tuwa wakati akirejea kutoka Mi’iraaj safari ya Usiku, alimwambia malaika Jibriyl: “Ewe Jibriyl! Watu wangu hawatoniamini.’ Alimwambia,”Abu Bakr anakuamini, Yeye ni As-Swiddiyq.”

 

Kuna Hadiyth nyingine inayothibitisha kuwa Jibriyl ndiye aliyempa jina hili. Kwa mamlaka ya An-Naazil bin Sawah ambaye alisema:

 

“Tulimwambia ‘Aliy ‘Ewe Khalifa wa Waumini! Tueleze juu ya Abu Bakr alisema: “Huyu ni mtu aliyepewa As-Swiddiyq kwa ulimi wa Jibriyl na Muhammad. Alikuwa Khalifa wa Mjumbe wa Allaah aliyemchagua kwa ajili ya dini yetu, hivyo tunaridhika naye kwa maisha yetu ya dunia.”

 

Kwa mamlaka ya Hakam bin Sa’d ambaye alisema: “Nilimsikia ‘Aliy akiapa ya kuwa jina la ‘As-Swiddiyq, (Abu Bakr) alipewa na Allaah :

 

 

Kurejea Kwa Baba Yake Katika Uislamu

 

 

Baba yake alikuwa ‘Uthmaan bin ‘Aamir akijulikana kama Abu Quhaafah. Alirejea kwenye Uislamu siku Makkah ilipokombolewa na akala kiapo cha utii kwa Mjumbe wa Allaah na kipindi cha Ukhalifa wa Abu Bakr Alifariki dunia wakati wa Ukhalifa wa ‘Umar

 

Sasa tumsikilize Asmaa bint Abi Bakr akitusimulia juu ya kurejea baba yake kwenye Uislamu.

 

“Mjumbe wa Allaah aliposimama Dhi–Tuwa, Abu Quhaafah alimwambia binti yake mdogo kabisa,’Ewe binti! Nisindikize safari yangu ya Abu Qubays kwa kuwa alikuwa kipofu kwa hiyo binti alimsindikiza. Alimwambia ‘Ewe binti, unaona nini? Alijibu: “Naona mkusanyiko wa watu wengi. Akamwambia, ‘Hawa ni farasi. Akajibu, ‘Namwona mtu akienda mbele na nyuma.’ Akasema, Huyu ndiye anayewaongoza na anakuwa mbele yao.’ Kisha akasema:  ‘WaLlaahi wametawanyika”, Akasema: ‘WaLlaahi! Wapanda farasi wameendelea na safari. Alirejea naye nyumbani wakiwa njiani, mpanda farasi alikutana naye, na alipomwona msichana amevaa kidani cha fedha, alikichukua.

 

Asmaa alisema: “Mjumbe wa Allaah alipoingia Makkah na kisha kuingia katika nyumba ya Allaah , Abu Bakr alimjia akimwongoza baba yake. Mjumbe wa Allaah alipomwona Abu Bakr akamwambia; ‘Ingekuwa vema kama ungelimwacha nyumbani mpaka nije kwake. Abu Bakr alijibu; “Ewe Mjumbe wa Allaah! “Analazimika kuja kwake kuliko wewe kwenda kwake.” Kisha Abu Bakr alimkalisha mbele ya Mjumbe wa Allaah Mjumbe wa Allaah alikigusa kifua chake kisha akamwambia, ‘Rejea katika Uislamu’ na alirejea katika Uislamu.

 

 

Kurejea Kwa Mama Yake Katika Uislamu

 

 

Mama yake akiitwa Salma bint Sakhr. Alikuwa miongoni mwa Waislamu wa mwanzo, na alikufa katika hali nzuri ya Uislamu. ’Aaishahh anasimulia kisa kifuatacho: “Maswahaba wa Mjumbe wa Allaah ambao idadi yao ilikuwa 39, walijumuika katika nyumba ya Darul-Arqam. Abu Bakr alimsisitizia Mjumbe wa Allaah ajitokeze mbele ya watu. Mjumbe wa Allaah alisema:

“Kwa hakika sisi ni wachache ewe Abu Bakr” Aliendelea kumchagiza mpaka Mjumbe wa Allaah alikubali na Waislamu walitawanyika Msikitini (Nyumba ya Allaah ).

 

Abu Bakr alisimama na alianza kuwaasa watu na Mjumbe wa Allaah alikuwa amekaa. Kwa hiyo, Abu Bakr alikuwa mtu wa kwanza kuwalingania watu katika dini ya Allaah na Mjumbe Wake hadharani. Makafiri walikasirika na kuwashambulia Waislamu. Abu Bakr alipigwa vibaya. Mwovu na fedhuli, ‘Utbah bin Abi Rabi’ah alimpiga kwa kobadhi mpaka Abu Bakr akajeruhiwa sana kiasi cha kushindwa kutofautishwa kati ya pua na uso. Banu Taym, jamaa zake Abu Bakr, walikuja kuwazuia makafiri kuendelea kumpiga. Walimpeleka Abu Bakr nyumbani, na wakarejea Msikitini huku wakiapa: ‘WaLlaahi, iwapo Abu Bakr atafariki dunia, tutamwua ‘Utbah.’

 

Walirejea nyumbani kwa Abu Bakr na Abu Quhaafah alimsemesha Abu Bakr mpaka akajibu. Aliporejewa na fahamu, alisema: ”Mjumbe wa ‘Allaah amefanya nini?”

Walimlaumu na kumkaripia.Waliondoka na kumwambia mama yake Ummul-Khayr amlishe na ampe kinywaji.

 

 

Abu Bakr aliendelea kuuliza: ‘Mjumbe wa Allaah amefanya nini?’ Mama yake akamwambia: ‘WaLlaahi sijui alichofanywa rafiki yako?’ Abu Bakr akamwambia, ‘Nenda kwa Umm Jamiyl bint Al-Khattwaab na umuulizie habari zake.’ Alipofika kwa Umm Jamiyl, alimwambia; ‘Kwa hakika, Abu Bakr anakuuliza juu ya Muhammad bin ‘Abdillaah.’ Umm Jamiyl alijibu ‘Simjui Abu Bakr wala Muhammad bin ‘Abdillaah, lakini kama unataka niende kwa mwanao, nitafuatana nawe.’ Alisema, ‘Ndiyo.’ Kwa hiyo Umm Jamiyl alifuatana naye na walimkuta Abu Bakr anakaribia kukata roho. Umm Jamiyl aliangua kilio na kusema: hakika watu waliokuumiza ni waasi, na namwomba Allaah Mlezi Akulipizie kisasi.’ Abu Bakr aliendelea kuuliza: ’Mjumbe wa Allaah anafanya nini?’ Alijibu: ‘Mamako huyu hapa anakusikiliza’. Abu Bakr akamwambia: ‘Usimhofie’ Akajibu, ‘Afya yake ni njema’. Akauliza tena, ‘Yuko wapi?’ Alijibu, ‘Katika nyumba ya Al-Arqam.’ Akasema: ‘WaLlaahi sitoonja chakula wala maji mpaka niende alipo’. Walimwambia asubiri mpaka watu watulie. Kulipotulia, alitoka akimwegemea mama yake na Umm Jamiyl. Alipoingia kwa Mjumbe wa Allaah alimbusu, na Mjumbe wa Allaah alifurahi sana.

 

Abu Bakr alimwambia: ‘Ningependa baba yangu na mama yangu watolewe muhanga, mimi sina tatizo isipokuwa yule mwovu (‘Utbah) amejeruhi uso wangu. Huyu ni mama yangu, maridhia kwa wazazi wake, nawe umetukuzwa (umebarikiwa). Kwa hiyo mkaribishe kwa Allaah, na umwombee kwa Allaah Amwokoe na adhabu ya Moto. Mtume alimkaribisha katika Uislamu naye aliupokea Uislamu.

 

Walikaa na Mjumbe wa Allaah kwa mwezi mmoja, na jumla yao walikuwa wanaume 39. Hamzah naye alirejea katika Uislamu siku ambayo “Abu Bakr alipigwa.

 

 

Kuhajiri

 

 

Mateso ya makafiri yaliposhitadi, Mjumbe wa Allaah aliwapa ruksa ‘Waislamu kuhajiri. Abu Bakr alipoomba ruksa ya kuondoka, Mjumbe wa Allaah alimwambia:

“Usifanye haraka. Inaweza kuwa Allaah atakuchagulia mwenza.” Abu Bakr alitarajia ya kuwa mwenza atakuwa Mjumbe wa Allaah mwenyewe, kwa hiyo alinunua vipando viwili kwa madhumuni hayo.

 

‘Aaishah anasema: “Mtume alikuwa akija kwenye nyumba ya baba yangu mapema asubuhi au jioni. Siku ile aliyeruhusiwa na Allaah kuhajiri, alitujia mchana. Abu Bakr aliondoka alipokaa juu ya kitanda na kumpisha Mtume Hapakuwa na mtu nyumbani isipokuwa Asmaa na mimi. Mtume alimwambia Abu Bakr ‘Waondoshe uliokuwa nao.’ Alisema, ‘Ewe Mjumbe wa Allaah! Hawa ni mabinti zangu. Kuna jambo gani?’ Mjumbe wa Allaah alijibu: ‘Allaah Ameniruhusu nihajiri’. Abu Bakr akasema: ‘Je, nifuatane nawe?’ Ewe Mjumbe wa Allaah? Alijibu ‘Ndiyo’. WaLlaahi sijapata kumwona mtu akitoa machozi kwa furaha kama nilipomwona baba yangu siku ile akitokwa na machozi ya furaha.”

 

 

Hijra

 

 

Mtume na Abu Bakr walimkodi ‘Abdullaah bin Urayqit ambaye alikuwa kafiri, kuwaongoza katika safari yao. Walimpa vipando viwili avichunge mpaka wakati utakapowadia. Hapana aliyeijua safari yao isipokuwa ‘Aliy bi Abi Twaalib, Abu Bakr As-Swiddiyq na familia ya Abu Bakr

 

Mtume na Abu Bakr walianza safari yao. Waliingia katika pango linaloitwa Thawr jirani ya Makkah. Kutokana na mapenzi yake kwa Mtume Abu Bakr alikuwa wa kwanza kuingia pangoni isije kuwa kulikuwa na mnyama pori mle ndani, alimkinga Mtume ili asimhatarishe maisha yake.

 

Abu Bakr alimtaka mwanae ‘Abdullaah asikilize waliyokuwa wakiyasema watu, na aje kwake kuwaelezea waliyokuwa wakijadili watu kuhusu kadhia hii. Alimtaka ‘Aamir bin Fuhayrah, mtumwa wake, awachunge kondoo wale mchana na jioni awapeleke pangoni kwa sababu mbili:

1.  Kuwakamua na kunywa maziwa yao.

2.  Kufuta nyoyo za ‘Abdullaah anapokuja kuwapasha habari.

 

Baada ya siku tatu watu walikata tamaa ya kuwatafuta. Mwongozaji (‘Abdullaah bin Urayqit) alikwenda pangoni na farasi watatu.

Asmaa bint Abi Bakr aliwaletea chakula. Wakati mmoja aliposahau Al-Isam (mkanda wa kubebea chakula) alichukua mkanda wake na kuukata. Alipewa lakabu ya Dhatun–Nitwaqayn (mwenye mikanda miwili) baada ya tukio hilo.

 

Makafiri walipopoteza matumaini ya kumkamata Mjumbe wa Allaah na Maswahaba zake, walitangaza zawadi nono ya ngamia 100 kwa yeyote atakayemshika. Waliangalia nyayo lakini walichanganyikiwa. Mmoja ya watu hodari wa kufuatilia nyayo alikuwa Suraaqah bin Malik.

 

Kwa msaada wake waliweza kupanda mlima alipokuwa Mtume na Maswahaba wake. Walipita mlango wa pango mara nyingi bila kutambua ya kuwa ndani mlikuwa na watu kwa sababu Allaah aliwafisha utambuzi na uoni wao ili kumhifadhi Mjumbe wa Allaah . Abu Bakr alimwambia Mtume: “WaLlaahi, kama mmoja wao angeangalia chini ya miguu yake, angetuona.”

Mtume alimwambia:

“Unafikiria nini juu ya (watu) wawili na Allaah ni watatu wao? Katika mapokezi mengine ya Muhammad bin Sinaan, iliyosimuliwa na Anas kuwa Abu Bakr alisema:

“Nilimwambia Mtume nilipokuwa pangoni, kama mmoja wao angeangalia chini ya miguu yake, angetuona.”Alisema, ‘Ewe Abu Bakr! Unafikiria nini juu ya (watu) wawili ambapo watatu wao ni Allaah?”

 

Watu wa Al-Madiynah walipopata habari ya kuwa Mtume alikuwa anaondoka Makkah, walimsubiri kwa hamu. Wakati mwingine ilikuwa asubuhi wakati jua lilikuwa kali. Siku ambayo Mjumbe wa Allaah alipowasili Al-Madiynah, mtu wa kwanza kumwona alikuwa Ya’aquub ambaye alijua kuwa watu wa Madiynah walikuwa wakimsubiri, alisema kwa sauti.

 

“Enyi Answaar! Yule mliyekuwa mkimsubiri amewasili: Kwa hiyo walitoka nje na kumlaki Mtume pamoja na Mwenzake chini ya kivuli cha mtende. Watu wengi wa Madiynah hawakumfahamu Mjumbe wa Allaah hivyo walijumuika ili wamfahamu. Kivuli kiliposogea, Abu Bakr alisimama kutengeneza kivuli kwa nguo yake. Kwa kitendo hicho walimfahamu Mjumbe wa Allaah Muhammad

 

 

Share