04-Wasiya Wa Mwisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Thamani Ya Nasaha Za Mwisho

 

Thamani Ya Nasaha Za Mwisho

 

Tafakari hisia za mama mwenye moyo laini anaposema buriani kwa mwanaye mpenzi au msisimko wa baba kipenzi anapofarakana na mtoto wake kipenzi na ujue ya kwamba kuachana tunako kuzungumza hapa ni kukubwa na kunatia uchungu.

 

Kwa hakika Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema buriani kwa Maswahaba zake na kwa Taifa lake. Ni maelezo gani ya ibada aliyowambia? Je, aliwafafanulia hukumu za Shariah ya Kiislamu? Je, aliwafundisha mambo yenye uhusiano na imani, ambayo hakuwahi kuyataja kabla? Au aliwafundisha kanuni mpya zinazohusiana na mwenendo wa Kiislamu? Hali ilihusu jambo jingine, kwani Dini na “rehema” zilikamilika; kwa hiyo nasaha hizi zilikuwa kamilifu na hakuwahi kuzitoa – kama utapenda, mama wa nasaha. Inatakiwa kujumuisha mazuri yote na mema, na kuonya juu ya maovu yote.

 

Nasaha za mwisho zina kupa Uislamu, imani, na ihsani kwa ukamilifu, zinakutoa kwenye mkanganyiko na shauku na zinakuongoza kwenye mwongozo ulio sahihi.

 

Si ajabu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa uwezo wa kuelezea mambo mengi kwa maneno machache. Enyi wasaka mema: tunyweni kutoka chemchemi safi, haya ni maneno yake:

“Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa khutbah yenye ufasaha,” ambayo ilikuwa ni majibu kwa amri ya Allaah.

“…uwape mawaidha na uwaambie maneno ya kuathiri na kuingia katika nafsi zao.” (4:63).

 

Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. …. (16:125).

 

Mwandishi wa Jamii al-‘Ulum-wal-Hikam alisema ya kuwa mlinganiaji kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) lazima awe mbuji, kwani watu wako tayari (wamezoea) kupokea ujumbe unapowasilishwa kwa ufasaha.

 

Katika lugha ya Kiarabu, balaghah (umbuji) maana yake kufikisha maana iliyo kusudiwa kwenye mioyo ya wasikilizaji katika njia nzuri, kwa kutumia maneno muafaka na suala husika; maneno yenye mvuto kwa wasikilizaji na kupenya ndani ya moyo. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakurefusha khutbah zake; bali alizifupisha, hata hivyo yenye maana ya kina.

 

Jaabir Bin Samurah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisimulia, “Nilikuwa nikiswali na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Swalah yake ilikuwa ya kati na kati (yaani, haikuwa ndefu au fupi) na khutbah yake ilikuwa vivyo hivyo (haikuwa ndefu au fupi)”[1]

 

Katika hadithi nyingine, Abu Wail alisema, “Ammar alitoa khutbah iliyo kuwa fupi lakini yenye kina. Aliposhuka kwenye mimbari, tulisema, “Ewe Abu al-Yaqdhan! Ulisema mengi kwa kutumia maneno machache; bora ungepumua (ungerefusha khutbah yako). Aliwajibu kwa kusema, “Kwa hakika, Nilimsikia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema,

 

‘Kwa uhakika, mtu kurefusha Swalah na kufupisha khutbah ni dalili za kuelewa (Fiqh); kwa hiyo refusheni Swalah na fupisheni Khutbah, na bila shaka kuna ‘uchawi’ katika baadhi ya khutbah.”[2] 

 

Wakati mmoja mtu alisimama na akatoa khutbah ndefu, ‘Amr Bin Al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema, “Kama angetoa khutbah ya kiasi, ingelikuwa bora kwake. Nilimsikia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema,

 

“Niliona ya kuwa –au niliamrishwa – kutoa khutbah fupi kwa uhakika, ufupisho ni mzuri.”[3].

 

Leo hapa tulipo tuna khutbah iliyoandikwa sana kwa madoido, lakini  hali yetu iko vipi? Na hadhi yetu ikoje miongoni mwa mataifa? Tunaishi katika zama za wasemaji wengi, Wanachuoni wachache, wakati tuna maneno mengi na vitendo vichache.

 

“….Inayosababisha macho kutoa machozi na mioyo kutetema.”  Machozi na kutetema kunaashira kiwango cha juu cha Iman.

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanapo somewa Aya zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao Mlezi" (8:2)

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

“Na wanaposikia yaliyoteremshwa kwa Mtume utaona macho yao yanachururika machozi kwa sababu ya Haki waliyo itambua. Wanasema: Mola wetu! Tumeamini. Basi tuandike pamoja na wanao shuhudia.” (5:83).

 

Hii ndio sabili ya wachaji na waumini wa kweli;

“Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidisha unyenyekevu.” (17:109).

 

Hiyo ndio mioyo ya wale walionufaika na nasaha na mawaidha:

wanajua na kutumia, ni wa kweli katika imani zao, na wanatubia kwa Mola wao.

 

Kutokana na unyeti wake, uchaji wao, unyenyekevu wao, na machozi yao, wao wenyewe wanaomba nasaha, wakisema,

“Hii ni kama khutbah ya kuaga, hivyo tunasihi.”

Walihisi kuwa mtu aliyependwa zaidi na watu alikuwa akiwapa mkono wa buriani, ambalo si jambo la kushangaza, kwani walikuwa viongozi wa Fuqaha na wanazuoni walio wafuatia. Hawakuridhika kwa kile walichokijua kutokana na khutbah zilizopita au hukumu: walitaka ziada, kwani hawakuridhika na kutafuta elimu. Hata hivyo maonyo waliyo yasikia kabla, walitaraji kupata nasaha zilizotimia, ambazo wengeweza kuzitumia kuboresha amali zao na kushikamana na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).



[1] Muslim (866)

[2] Muslim (869)

[3] Ilisimuliwa na Abu Daawuud katika Swahiyh Sunan Abi Daawuud.

 

Share