09-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: 'Uthmaan Bin 'Affaan (Radhiya Allaahu 'Anhu) - 2

 

Ukarimu Wake

 

Tumeona jinsi ambavyo ‘Uthmaan alivyokuwa tayari kutoa katika njia ya Allaah. ‘Uthmaan hakukoma hapa. Hakuwa kama mvua iliyonyesha katika muda mwafaka. Alifahamika kwa kusaidia masikini na yeyote aliyehitaji msaada wake. Imesimuliwa kwa mamlaka ya Ibn ‘Abbaas.

Ibn ‘‘Abbaas alisema:

 

Wafanya biashara walifika nyumbani kwa ‘Uthmaan na kubisha hodi. Alitoka nje na joho lake ametungika mabegani, aliwauliza, “Mna shida gani?” Walijibu. “Tumepata habari ya kuwa kuna msafara unakuja kwako, una ngano na vyakula.  Tuuzie ili tuweze kuwasaidia masikini wa Madiynah.” ‘Uthmaan aliwajibu. “Ingieni ndani nyote.” Waliingia na kushangaa. Kulikuwa na mizigo elfu moja iliyopakuliwa nyumbani kwa ‘Uthmaan. Aliwaambia,”Mtanilipa kiasi gani kama faida? Walijibu, “Kumi kwa kumi na mbili.“ Aliwambia, “Nimepewa zaidi.” Wakasema, ”Kumi kwa kumi na nne.” Akasema,”Nimepewa zaidi.”   Wakamwambia, “Kumi kwa kumi na tano.” Akasema, “Nimelipwa zaidi.” Wakamwambia, “Nani mwingine aliyekulipa zaidi? Wafanya biashara wote wa Madiynah tuko hapa?” Akasema. “Kila dirham nimelipwa, mara kumi. Je, mnanyongeza yoyote?” Wakajibu. “Hapana.” Akawaambia, ”Nyie ni mashahidi kuwa nimetoa sadaka kwa masikini wa Madiynah.”

 

 

Kujinyima Anasa za Dunia

 

‘Uthmaan alikuwa mfano wa mtu aliyejinyima anasa za dunia na mcha-Mungu. Aliishi maisha ya kawaida. Alikula chakula cha kawaida, na hakufanya israfu katika mavazi na kufuja mali. Alijua ya kuwa Allaah hakujishughulisha na umbile la nje la mtu bali umbile la ndani na nia yake.

 

‘Abdul-Malik bin Shaddad bin Al-Had alisema.       

“Nilimwona ‘Uthmaan Ijumaa moja juu ya mimbari amevaa nguo ya Aden isiyo na thamani zaidi ya dirham nne au tano na kilemba cha Kufi kitochotiwa dai.[1]

Pamoja na kuwa alikuwa Khalifa alilala mchana Msikitini juu ya changarawe.

 

Al-Hasan aliulizwa juu ya wale wanaolala mchana Msikitini. Alijibu, ”Nilimwona ‘Uthmaan bin ‘Affaan akilala mchana Msikitini. Alikuwa Khalifa wa Waislamu wakati huo. Alipoamka kutoka usigizini alikuwa na alama za kokoto kwenye ngozi yake. Watu walisema,”Huyu ni jemadari wa Waislamu. Huyu ni jemadari wa Waislamu.”

                                                                                             

Kwa hiyo, tunaona ya kuwa kujirahisisha na kuipa nyongo dunia ilikuwa hali yake ya kawaida. Aidha alipanda mnyama wa kawaida sio farasi dume.

Imeelezwa kwa mamlaka ya Maymuun bin Mahran:

“Al-Hamdaan aliniambia ya kuwa alimwona ‘Uthmaan akipanda farasi jike na mtumwa wake alipanda nyuma yake.”[2]

 

 

Kujitambua

 

Alikuwa mcha-Mungu na akiogopa Siku ya Malipo.

Kwa mamlaka ya Hani, mtumwa aliyemwacha huru:

“Kila ‘Uthmaan aliposimama mbele ya kaburi, alilia mpaka ndevu zake zikalowa. Aliiogopa Siku ya malipo kwa sababu ni siku ambayo hapana ‘amali zitakazofanywa na kumbukumbu zitakuwa zimefungwa.”

‘Uthmaan alikuwa akisema:

“Kama ningekuwa kati ya Pepo na Moto bila kujua nitaamuriwa kwenda wapi, ningechagua kufanywa jivu kabla ya kujua nitaamriwa kwenda wapi.[3]

 

Abul-Fusayt alisema:

“Siku moja, ‘Uthmaan alimwambia mtumwa wake, “Kwa hakika, mara moja nilikufinya sikio lako, hivyo lipiza kisasi.”Kisha akamwambia yule mtumwa, “Nifinye kwa nguvu kwa kulipiza hapa duniani kunavumilika ya Akhera hayavumiliki.”[4]

         

Kujitambua kwake kulimzuia kusimulia Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Japokuwa alikuwa mtu wa karibu sana. Alikuwa mume wa mabinti mawili wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Ruqayyah na Ummu Kulthum. ‘Amr bin Sa’ad bin Abi Waqqaas alisema ya kuwa alimsikia ‘Uthmaan akisema, “Kinachonizuia kusimulia Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kuogopa kuwa sikuwa msikivu. Nilisikia Hadiyth isemayo: “Yeyote anayezua neno, na akalihusisha nami, atapata makazi yake Motoni.”[5]

 

 

Ukhalifa

 

Baada ya ‘Umar kuchomwa kisu, aliambiwa: “Teua (mrithi) Ewe Jemadari wa Waumini!” ‘Umar alijibu. “Hapana wanaostahiki zaidi katika suala hili kundi hili la watu aliowafia. Aliwataja majina; ‘Aliy,

‘Uthmaan, Az-Zubayr, Twalhah, Sa’ad na ‘Abdu-Rahman.”

Aliendelea kusema: ‘Abdullaah bin ‘Umar (mwanae) awe shahidi (katika uchaguzi) nazingatia ya kuwa hahusiki na kadhia hii.”

 

Lile kundi lililochaguliwa walimchagua ‘Uthmaan kuwa Jemadari wa Waumini na mrithi wa ‘Umar.

 

 

Ushindi Katika Utawala Wake

 

Vita nyingi zilipiganwa na kupatikana ushindi katika sehemu zote, baharini na nchi kavu. Ushindi huo ulidumu kwa miaka kumi mpaka uliposimamishwa na Al-Fitnah (zahama).

 

Maadui wa Uislamu kwa makusudi kabisa waliendelea kufanya fujo na kusita kutekwa na mipaka yao kuingizwa katika ardhi ya Waislamu na majaribio mengi yalisitishwa.

 

Kabla ya kipindi cha ‘Uthmaan, Waislamu waliteka majimbo mengi na kuongeza maeneo mazuri katika dola ya Kiislamu. Waislamu hawakuweza kuacha idadi kubwa ya wanajeshi katika miji na sehemu walizozifungua kwani Waislamu wakati huo walikuwa ni wachache.

 

‘Umar alipouawa, wakazi wa majimbo ya jirani walidhani Waislamu wamekuwa dhaifu. Walidhani sasa ulikuwa muda mwafaka kuanzisha mashambulizi. Walivunja mikataba waliokubaliana na Waislamu, na ‘Uthmaan kama Khalifa, alipambana nao kwa nguvu. Alikusanya majeshi chini ya makamanda wazoefu, na jeshi lilimudu kuleta utulivu kwa mara ya pili huko Persia (Iran), Khurasan, Babul Al-Abwaab, Afrika na Armenia.

 

‘Uthmaan hakufanikiwa kuwashinda maadui tu bali aliongeza ardhi mpya katika dola ya Kiislamu baada ya kushinda vita nyingi.

 

Nchi zifuatazo ziliongezwa katika dola ya Kiislamu.

1.     Katika Afrika, eneo la kuanzia Tripoli mpaka Algeria.

2.     Cyprus (Kuprus) katika Maditerranean.

3.     Mashariki ya Uturuki.

4.     Armenia, na kaskazini mwa Daghustan.

5.     Kapol, na Sind.

 

Vita hivi havikuwa rahisi. Vilikuwa vikali kama ilikuwa baharini au nchi kavu. Inatosha kutaja mfano mmoja tu.

Vita inaitwa Dhatus-Sawari (vita ya mlingoti uliosimikwa). Constantina, mtoto wa Hercules akiwa kamanda katika mwaka wa 31 wa Hijriyah, akitarajia kulipiza kisasi kwa Waislamu, walimshinda katika Afrika. Waislamu wengi waliuawa. Makafiri wasio na idadi pia waliuawa, lakini siku hiyo Waislamu walikuwa na uvumilivu usio na kikomo, na Allaah Aliteremsha ushindi kwa Waislamu.         

 

 

Ustawi wa Jamii Wakati wa Utawala Wake

 

Dola ya Kiislamu ilipanuka sana enzi za Ukhalifa wa ‘Uthmaan Zama zake zilikuwa za ustawi wa jamii na wingi na mali; watu wake walifurahia maisha mazuri na anasa. Muhammad bin Sina alisema”

“Utajiri (mali) uliongezeka wakati wa utawala wa ‘Uthmaan. Mjakazi aliweza kuuzwa kwa kupimwa kwa fedha, farasi kwa dirhamu laki moja na mtende kwa dirham elfu moja.

Al-Hasan alisema: “Chakula kilikuwa kingi wakati wa Ukhalifa wa ‘Uthmaan.”[6]

 

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Akimsifu Wakati Wote.

 

‘Uthmaan alikuwa mwenza wa kudumu wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ingekuwaje kinyume chake? Alikuwa mume wa Ruqayyah na kisha Umm Kulthum baada ya kifo cha Ruqayyah. Alikuwa Swahaba mcha-Mungu na mwenye soni na alipendwa sana na kuwavutia watu wengi. Vipi isingekuwa hivyo, ambapo alitumia mali zake nyingi katika njia ya Allaahambapo hapana aliyekuwa sawa naye katika hili.

 

Kama uthibitisho wa mapenzi hayo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimwombea sana ‘Uthmaan kwa Allaah kwa du’aa:

”Allaah Akusamehe Ewe ‘Uthmaan kwa yale uliyoyatenda, utakayoyatenda na utakayoyaficha, uliyoyadhihirisha, na yale yatakayokuwepo mpaka Siku ya Hukumu.”

 

Anas alisimulia ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema,

“Mtu mkarimu zaidi katika ummah wangu kwa ummah wangu ni ‘Abu Bakr, Mkali zaidi katika Dini ya Allaah ni ‘Umar na mwenye soni ya kweli ni ‘Uthmaan.”

 

Aidha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimzungumzia kwa ‘Aaishah.

“Hutaki nione haya mbele ya mtu anayeonewa haya na malaika?”

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliendelea kusema: “Ewe Allaah!  Nimeridhishwa na ‘Uthmaan na nakusihi uwe radhi naye pia.”[7]

Na pia alisema,

“‘Uthmaan ni mwenye soni zaidi na mkarimu zaidi katika ummah wangu.”[8]

Na pia alisema:

“Mwenye haya zaidi katika ummah wangu ni ‘Uthmaan.”[9]

 

 

Rai za Maswahaba Kuhusiana Naye

 

Kuna masimulizi sahihi kuwa wakati ‘Abu Bakr akimsomea wasia wake ‘Uthmaan kuhusu mrithi wake, alitaja jina la ‘Umar kuwa khalifa wa kumrithi, kisha Abu Bakr alipoteza fahamu.

‘Uthmaan aliandika: “Umar”. Abu Bakr alipozinduka, aliuliza: “Kumeandikwa nini?” ‘Uthmaan alisema: “Umar” Abu Bakr alisema,”Utukufu kwa Allaah ambaye ameutawala mja wake.”

 

Mutarrifu alimsifu ya kuwa alikutana na ‘Aliy ambaye alimwambia: “Ewe Abu ‘Abdullaah!  Kitu gani kilichokuchelewesha? Ni mapenzi kwa ‘Uthmaan? Iwapo unakubali niliyosema (kuhusu kumpenda ‘Uthmaan), utakuwa sahihi kwa sababu alikuwa na shauku ya kuwaunganisha jamaa zake, na anamwogopa sana Allaah[10]

 

Ibn ‘Umar aliripoti, “Wakati wa uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tuliwataka watu wachague kati ya Abu Bakr, ‘Umar na ‘Uthmaan, na watu walimchagua Abu Bakr, ‘Umar na kisha ‘Uthmaan.[11]

 

Ibn Sirin alisema:

“Aliyekuwa na elimu zaidi juu ya ibada za Hijjah alikuwa ‘Uthmaan na kisha Ibn ‘Umar.[12]

 

‘Uthmaan alipochaguliwa kuwa Khalifa, Ibn Mas’uud alisema”

“Tumemchagua mbora wa wote walio hai, na hatukufanya hiyana.”

 

‘Abdullaah bin ‘Umar alisema:

“Wanaume watatu wa Kiquraysh ni wenye sura nzuri zaidi, wenye mwenendo mwema na wenye soni zaidi (sana) Wanapokuambia kitu, basi ni kweli Na ukizungumza nao, hawatokudanganya. Watu hao ni: Abu Bakr, ‘Uthmaan bin ‘Affaan na Abu ‘Ubaydah bin Al-Jarraah.”[13]

 

Masruuq alikutana na Al-Ashtar na kumwambia, “Umemwua ‘Uthmaan?”  Alijibu, “Ndiyo” “WaLlaahi, umemuua na wakati wote alikuwa anafunga na kuswali.”

 

 

Kufa Shahidi

 

Maadui wa ‘Uthmaan walieneza uvumi wa uongo ili watu wawe dhidi yake. Walimshutumu kwa kuwapendelea jamaa zake na kuwa aliwapa vyeo katika ofisi za dola badala ya Maswahaba wengine wa Mjumbe wa Allaah. Walitumia fursa ya hali ya uvumilivu wa ‘Uthmaan na kufululiza kujaribu kuwaridhisha raia wake badala ya kuwa mkali kwao.

‘Abdullaah bin Saba alikuwa mstari wa mbele katika hujuma hii.

 

Kikundi kilitoka Misri kilikwenda kwa ‘Uthmaan huko Madiynah wakimlalamikia Amir wao, ‘Abdullaah bin Sa’da bin Abi Sarh. Aliwapokea na akakubaliana nao kuwa Amir atauzuliwa. Alipofikisha ushauri wao wakamteua Muhammad bin Abi Bakr na akatoa agizo kuhusiana na hilo. Walianza safari ya kurejea kwao Misri. Njiani walimwona kijana aliyepanda farasi huku akimpiga sana. Walimwuliza, kulikoni? Yule kijana aliwajibu:

“Mimi ni tarishi wa Kamanda wa Waumini, amenituma niende kwa Amir wa Misri.”

 

Walipofika walikuta barua (iliyoghushiwa) kutoka kwa ‘Uthmaan kwenda kwa ‘Abdullaah bin Sa’d bin Abi Sarh ikisema:

“ Iwapo fulani na fulani watakuja kwako,  waue kwa kughushi,  puuza barua yao, na endelea na madaraka yako mpaka taarifa nyingine itakapokufikia.”

 

Lile kundi lilihamanika na kurejea Madiynah walipomhoji ‘Uthmaan aliapa kwa jina la Allaah kuwa hakuandika barua ile. Baadaye ilithibitika kuwa Marwaan ndiye aliyeghushi barua ile. Walipomtaka ‘Uthmaan awakabidhi Marwaan, alikataa kwa kuchelea kuwa wangemuua.

Lile kundi likasema”

“Ama tupatie Marwaan au jiuzulu Ukhalifa.”

 

‘Uthmaan alikataa, hivyo walimzingira na kutaka kumuua. ‘Aliy aliwatuma watoto wake wawili Hasan na Husayn ili wamlinde. Az-Zubayr alimtuma mtoto wake ‘Abdullaah, Twalhah na Maswahaba wengine wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia walituma watoto wao kwa lengo hilo hilo, lakini maasi walipanda ukuta wa nyumba. ‘Uthmaan alikuwa akisoma Qur-aan aliyoipenda sana. Alipokuwa akisoma kimya na unyenyekevu, walimuua. Alikufa na Mus-haf mikononi.

 

Aliuawa tarehe 18 Dhul –Hijjah, mwaka wa 35 H, na alizikwa Al-Baqi’i. Alikuwa na umri wa miaka 82.

 

 



[1] Hilyat Awliya’ 1/60

[2] Hilyat Awliya’

[3] Hilyat Awliya’

[4] Ar-Riyaadh An-Naadirah.

[5] At-Taariykh Al-Kabiyr 2191

[6] Ar-Riyaadh An-Naadirah

[7] Muslim

[8] Muslim

[9] Hilyat Awliyaa’

[10] Swifatus-Safwah.

[11] Al-Bukhaariy 2655

[12] Imeripotiwa na Ibn ‘Asakir

[13] Hilyat Awliyaa’ 1/57

Share