Zingatio: Je, Wewe Ni Miongoni Mwa Waumini?

Zingatio: Je, Wewe Ni Miongoni Mwa Waumini?

 

Raashid Husayn

 

Alhidaaya.com

 

 

Je, wewe ni miongoni mwa Waumin? Kama humo basi usikate tamaa, utakuwemo in shaa Allaah kwa kufanya bidii ili nawe uwe miongoni mwa hao waitwao Waumin kwa tawfiq ya Allaah na Rehma Zake.

 

Kwa kawaida kila mwanaadamu hupenda kufikiwa na mambo mazuri na habari nzuri bila ya kutafakari ya kwamba, je ametimiza sifa za kufikiwa na habari hiyo nzuri au sifa hizo au malipo yanayostahiki na huo uzuri au laa?

 

Waislamu wote hupenda kuwa na sifa ya kuwa Waumin. Hata hivyo, suali linabaki kuwa: Je, kila Muislamu anaingia kwenye sifa ya kuwa Muumin? Kwani ukiwa miongoni mwa Waumin basi utakuwa ni miongoni mwa watakaoingizwa kwenye Jannah ya Firdausi.

 

Muumin wa kweli ni yule mwenye sifa zitakazotajwa hapa chini. Hivyo, tujiangalieni tumetimiza sifa hizo ili kuwa miongoni mwa hao Waumin wa kweli? Kama bado, basi tujitahidini In shaa Allaah Allaah Atujaalie tuwe miongoni mwa hao wanaoitwa Waumin wa kweli na Allaah mwenyewe.

 

Zifuatazo Ni Sifa Za Muumin Wa Kweli:

 

1) Anapotajwa Allaah nyoyo zao hujaa hofu, iwapo hujai hofu basi umekosa sifa ya kwanza ya kuwa Muumin.

2) Inaposomwa Qur-aan imani zao huzidi, iwapo imani yako haizidi basi umekosa sifa ya pili ya Waumin.

3) Waumin haswa humtegemea Rabb wao, iwapo humtegemei Rabb wako basi umekosa sifa ya tatu ya kuwa Muumin.

4) Ambao wanashika Swalah na wanatoa katika yale wanayoruzukiwa, iwapo husimamishi Swalah na hutoi ulivyoruzukiwa basi si katika Waumin.

 

Hao ndio Waumin wa haki (kweli).

 

Ni nani atakaekupima ya kwamba umefikia sifa za kuwa wewe au mimi ni miongoni mwa Waumin?

Jibu: Kila mwanadaam huweza kujifahamu au kujipima yeye mwenyewe, kama Alivyosema Allaah ndani ya Qur-aan ya kwamba:

 بَلِ الْإِنسَانُ عَلَىٰ نَفْسِهِ بَصِيرَةٌ﴿١٤﴾وَلَوْ أَلْقَىٰ مَعَاذِيرَهُ﴿١٥﴾

Bali insani ni shahidi dhidi ya nafsi yake. Japo akitoa nyudhuru. [Al-Qiyaamah Al-Qiyaamah: 14-15]

 

 
Zifuatazo ni sifa za Muumin kama Allaah Alivyomsifu huyo Muumin ndani ya Qur-aan, sifa ambazo zipo hapo juu tulizozitaja:

 

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ﴿٢﴾الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ﴿٣﴾ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا ۚ لَّهُمْ دَرَجَاتٌ عِندَ رَبِّهِمْ وَمَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ﴿٤﴾

Hakika Waumini ni wale ambao Anapotajwa Allaah, nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayaat Zake huwazidishia iymaan, na kwa Rabb wao wanatawakali. Ambao wanasimamisha Swalaah na katika yale Tuliyowaruzuku hutoa. Hao ndio Waumini wa kweli!  Wana daraja (za Jannah) kwa Rabb wao na maghfirah na riziki karimu. [Al-Anfaal: 2-4]

 

Ikiwa umetimiza sifa hiyo hapo juu ya kuwa Muumin basi unaingia kwenye hatua ya pili, kama ambavyo Allaah Alivyomuamrisha Nabiy Wake kwa kumwambia:

 

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu. [Az-Zumar: 53]

 

Zifuatazo Ni Sifa Za Muumin Atakaefuzu

 

Zifuatazo ni sifa za Muumin aliyefuzu baada ya kutimiza sifa za kuwa Muumin. Basi jiangalie, je utakuwa miongoni mwa Muumin aliyefuzu?

 

1)    Muumni ambaye ananyenyekea kwenye Swalaah yake, iwapo mtu hunyenyekei basi hujafuzu.

2)  Ambae anajiepusha na mambo ya upuuzi, iwapo hujiepushi na mambo ya kipuuzi basi utakuwa hujafuzu. Labda mtu atajiuliza suali - mambo ya kipuuzi ni yepi? Tukipata wasaa in shaa Allaah tutakuja kuyaeleza mambo ya kipuuzi ni yepi kutokana na mtizamo wa Kiislamu.

3)  Ambaye anatoa Zakaah, iwapo upo kwenye kundi la wenye kuwajibika kutoa Zakaah na ukawa huitoi, basi utakuwa hujafuzu.

4)  Ambaye analinda tupu yake isipokuwa tu kwa wake zake, iwapo huilindi tupu yako basi utakuwa hujafuzu, na ndie yule anaeitwa mzinifu. Allaah Atuepushe na uzinifu.

5)   Ambaye hutimiza amana na ahadi, iwapo ukiwa unaifanyia khiyana amana na huna ahadi, basi hujafuzu.

6) Ambaye Swalaah zake anazihifadhi, iwapo huhifadhi Swalaah zako basi hujafuzu (hujafanikiwa).

 

Ikiwa basi unatimiza sifa hizi, basi utakuwa umefuzu (umefanikiwa), na ndio utarithi Jannah iitwayo Firdaws kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Mnapomuomba Allaah Jannah, Muombeni (Jannah) ya Firdaws kwani (jannah hiyo) ni ya kati na kati na ndani yake inatiririka mito, juu yake kuna Arshi ya Ar-Rahmaan.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Habari hii Allaah Ameizungumza kwenye Suwrah Al-Muuminuwn Aayah 1-11.

 

 قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾ وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ ﴿٣﴾ وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ ﴿٤﴾ وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾ إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٦﴾ فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿٧﴾ وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ ﴿٨﴾ وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ ﴿٩﴾ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾ الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾

Kwa yakini wamefaulu Waumini. Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea. Na ambao wanajiepusha na mambo ya upuuzi. Na ambao wanatoa Zakaah. Na ambao wanazihifadhi tupu zao. Isipokuwa kwa wake zao, au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume basi hao hawalaumiwi. Lakini atakayetaka kinyume ya hayo; basi hao ndio wapindukao mipaka. Na ambao amana zao na ahadi zao wanazichunga. Na ambao wanazihifadhi Swalaah zao. Hao ndio warithi. Ambao watarithi (Jannah) ya Al-Firdaws, wao humo ni wenye kudumu.

  

Hitimisho

 

La muhimu ni kuwa, maadam tuko hai tusikate tamaa, tujitahidi. Yule ambae anahisi yuko miongoni mwa Waumin aongeze bidii, asije akatoka humo na yule aliyekuwa bado hajatimiza sifa za Muumin. Basi na azidishe bidii ili aingie humo Firdaws na akabidhi roho yake huku akiwa Muumin wa kweli.

Share