Zingatio: Ulichoandikiwa Utapatiwa

 

Zingatio: Ulichoandikiwa Utapatiwa

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Wanaadamu wa leo wamejaaliwa kuwa na teknolojia, ujuzi, elimu na vifaa ambavyo hawakupatapo kuwa navyo wanaadamu waliopita. Vingi katika vifaa hivi ni vyenye kumsaidia katika maisha yake na zaidi ni katika kujipatia rizki zake. Lakini, wanaadamu wa leo ndio wameshtadi kwa kula haramu.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kwamba itafika wakati ambao kila Muislamu atakula ribaa, na yule ambaye atajitahidi kuikimbia ribaa, basi atalipata vumbi lake: “Wakati kwa hakika unakuja kwa mwanaadamu ambapo mtu anayepokea ribaa tu ndiye atakayebakia, na iwapo haipokei, baadhi ya vumbi litamfikia yeye.” [Imesimuliwa na Abu Hurayrah na Imepokewa na Abu-Daawuud]

 

Rabb wetu Atakuja kutuhukumu kwa neema na baraka Aliyotushushia hivi leo na bado hatuna wakati wa kumuabudu. Tuna zana za usafiri za kisasa zenye kwenda kwa kasi na zilizojaa anasa ndani yake. Lakini tunapofika kwenye kituo kusudio tu, hata shukrani tunashindwa kumpatia Rabb Mlezi Aliyetulinda na dharuba katika msafara huo.

 

Juu ya hivyo, aliyejaaliwa kupokea shilingi moja anafanya matumizi ya shilingi kumi. Ajabu zaidi hata kwa yule aliyejaaliwa kupokea milioni moja, basi naye afanya matumizi yake kwa shilingi milioni kumi. Matokea yake ni kipi kinachotokezea hapo? Madeni na wizi basi, wala hakuna chengine. Ee Muislamu, Rabb wako Ameshakupangia kikomo chako kwa kila mwezi, wataka kushindana naye na kuanza kujipangia mambo yanayokuzidi kimo chako?

 

Tukielekea upande wa mali ndio hayo hayo, migogoro na dhulma zilizojaa kwenye ardhi hazina mpaka. Yote ni kwa sababu ya kutotosheka na rizki aliyopangiwa mja. Aliyekuwa na ekari moja anataka kuwa na ekari kumi na mfano wa huo.

 

Waislamu ni vyema tukaelewa sera ya Uislamu pale Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipotufunza kwa kutupigia mfano wa ndege. Ambaye anatoka asubuhi akiwa tumbo tupu, hali ya kuwa anarudi jioni akiwa tumbo lake limejaa:

 

Imesimuliwa na ‘Umar bin al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu), kwamba alimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Ukiweka imani yako kikamilifu kwa Allaah, atakuandalia rizki yako kama vile Alivyowaandalia ndege. Ndege wanatoka asubuhi na hali hawana kitu matumboni mwao na jioni wanarudi hali yakuwa yamejaa.” [Imepokelewa na At-Tirmidhiy]

 

Ni wangapi wamepata rizki zao bila ya kutarajia? Wanaamka asubuhi wakiwa hawaelewi mbele wala nyuma, basi wakamtegemea Muumba, wakanyooshewa mambo yao bila ya kutarajia kabisa.

 

Naye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametuahidi kwamba, tunapomuamini Yeye Atatushushia rizki kutoka mbinguni na kutoka ardhini:

 

وَلَوْ أَنَّ أَهْلَ الْقُرَىٰ آمَنُوا وَاتَّقَوْا لَفَتَحْنَا عَلَيْهِم بَرَكَاتٍ مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ وَلَـٰكِن كَذَّبُوا فَأَخَذْنَاهُم بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٩٦﴾

Na lau kama watu wa miji wangeliamimi na wakawa na taqwa, bila ya shaka Tungeliwafungulia baraka kutoka mbinguni na ardhini, lakini walikadhibisha, basi Tukawachukua kwa yale waliyokuwa wakiyachuma. [Al-A’araaf: 96]

 

Hivyo, tunazinasihi nyoyo zetu na za Waislamu wenzetu kuelewa kwamba, hata kama rizki ipo maili alfu moja juu ya mbinguni au chini ya ardhi, kama umeandikiwa kuipata itakuja kwako na kwa wakati ule ule uliopangiwa, haichelewi wala haifiki mapema.

 

Kila mmoja kati yetu ana rizki yake, amepangiwa chakula na kinywaji chake, na halikadhalika kipato chake, haondoki duniani kiumbe yeyote isipokuwa tu pale anapomaliza salio lake lote katika rizki zake alizopangiwa duniani.

 

Twamuomba Allaah Atujaalie kuchuma rizki za halali tukaweza kuzitumia katika njia ya halali – Aamiyn.

 

 

 

Share