Kuswali Kwa Kukaa

 

SWALI:

Swala ni kitu cha lazima tulichoamrishwa na Allah, lakini wakati mwengine huwa unajisikia kama umechoka lakini ni lazima uswali kwa sababu unajuwa kama hujaswali utapata dhambi. Je, kama utaswali huku umekaa inakubalika Swalah hiyo?

 



 

JIBU:

Twamshukuru Allaah Ambaye pekee Anastahiki sifa na utukufu na Swalah na Salamu zimfikie kipenzi chetu, Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), familia yake, Maswahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Malipo.

Tunamshukuru ndugu yetu ambaye ana thiqah na sisi kwa kuuliza swali hili na tunaomba tawfiki ya Allaah katika kulijibu swali hili ili lipate kueleweka.

Mwanzo inatakiwa ieleweke kwa Swalah ni amali kubwa sana kwa Muislamu na fadhila zake ni nyingi na ndiyo amali ya kwanza itakayo hesabiwa Siku ya Qiyaama. Hivyo, tumetakiwa tudumu katika Swalah kama Alivyosema Aliyetukuka:

}}فَأَقِيمُواْ الصَّلاَةَ إِنَّ الصَّلاَةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا{{

{{“Na simamisheni Swalah hakika Swalah imekuwa kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati maalumu”}} (Q 4: 103).

Na ameifanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nguzo ya pili katika nguzo za Uislamu tano (Imepokewa na Al-Bukhariy na Muslim kutoka kwa Ibn ‘Umar).

Swalah ina hekima kubwa kwa mwenye kuswali vilivyo, hivyo kumtengezea tabia na maadili mema na kumuondoshea mambo machafu.  

Allaah Anasema:

}}وَأَقِمِ الصَّلَاةَ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَى عَنِ الْفَحْشَاء وَالْمُنكَرِ وَلَذِكْرُ اللَّهِ أَكْبَرُ وَاللَّهُ يَعْلَمُ مَا تَصْنَعُونَ{{

{{“Na simamisha Swalah hakika Swalah inakataza machafu na maovu”}} (29: 45).

Swalah ina ubora mkubwa sana kwa Muislamu na inatosha kuweka wazi ubora wa Swalah na ukubwa wa jambo lake.

((Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: “Msingi wa mambo ni Uislamu, na nguzo yake ni Swalah na kilele cha nundu yake ni kupigana katika njia ya Allaah”)) (Imepokewa na at-Tirmidhiy).

Kwa ajili hii Allaah hakutuamru tuswali tu bali inatakiwa tusimamishe Swalah. Kuswali tu bila kutekeleza mambo ya msingi hakuna maana kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amesema:

}}وَيْلٌ لِّلْمُصَلِّينَ{{

}}الَّذِينَ هُمْ عَن صَلاَتِهِمْ سَاهُون{{

}}الَّذِينَ هُمْ يُرَآؤُونَ{{

{{Ole wao wanaoswali. Ambao wanapuuza Swalah zao; Ambao wanajionyesha”}} (107: 4 – 6)

Hivyo tutahadhari sana tunaposwali tusiwe ni wenye kuipuuza au kufanya riyaa, na lau tutafanya hivyo itakuwa hatuna thawabu yoyote na tutakuwa na adhabu kali.

Kusimamisha Swalah ambayo imetajwa katika Aayah nyingi ni kutekeleza masharti ya kupasa kwake (mfano ni Uislamu, kuwa na akili timamu, kubaleghe, kuingia wakati na kuwa twahara). Na masharti ya kuswihi kwake ni kutwahirika, kusitiri tupu, na kuelekea Qiblah. Ili Swalah iwe itakubaliwa ni lazima nguzo zake zitekelezwe na hapa ndipo tunapokuja katika swali letu.

Je, nguzo za Swalah maana yake ni nini? Nguzo za Swalah ni yale mambo yanayofanywa ili kukubaliwa Swalah na lau moja ya nguzo itaachwa basi Swalah itakuwa haijakamilika. Miongoni mwa nguzo za Swalah ni kusimama kwa mwenye kuweza katika Swalah ya Faradhi. Swalah haitosihi kwa kukaa mwenye kuweza kusimama. Haya tunayapata kwa maneno ya Allaah Mtukufu:

}}حَافِظُواْ عَلَى الصَّلَوَاتِ والصَّلاَةِ الْوُسْطَى وَقُومُواْ لِلّهِ قَانِتِينَ{{

{{“Zihifadhini Swalah na hasa Swalah ya kati na kati na simameni kwa ajili ya Allah hali ya kuwa watiifu”}} (2: 238).

Na pia maneno ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akimwambia Imran bin Huswayn (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye alikuwa na ugonjwa wa bawasili na akawa hawezi kuswali kwa kusimama,

((“Swali hali ya kuwa umesimama, ikiwa hutoweza kusimama basi swali katika hali ya kukaa, ikiwa hutoweza kukaa basi swali kwa kulala kwa ubavu”)) (Imepokewa kwa al-Bukhaariy, at-Tirmidhiy na Abu Dawud).

Kwa sababu Uislamu ni Dini ya kimaumbile ya mwanadamu haimkalifishi mtu jambo ambalo haliwezi. Allah anatuelezea:

}}لاَ يُكَلِّفُ اللّهُ نَفْسًا إِلاَّ وُسْعَهَا لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ{{

{{“Allaah haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo. Faida ya iliyoyachuma ni yake, na hasara ya iliyoyachuma ni juu yake pia”}} (2: 286).

Ayah na Hadiyth tuliyoitaja juu ni dalili ya kuwa ni wajibu kuswali Swalah ya Faradhi kwa kusimama kwa yule mwenye kuweza. Ikiwa hataweza hilo katika Swalah ya Faradhi ataswali kwa ile hali anayoweza. Hivyo, ikiwa mtu ni mgonjwa au kiwete au ana matatizo mengine ambayo yanamfanya asiweze kusimama ataswali kwa kukaa au kulala ubavu kama Hadithi ilivyoeleza hapo juu. Na ikiwa hawezi kwa njia hizi basi hata kwa ishara, kwani swalah haina udhuru wa kuachwa isipokuwa kwa wanawake katika damu ya mwezi au ya uzazi, mtu ambaye ni mwendawazimu, au mtu ambaye yupo katika coma (amezirai kabisa).

Mtu anayeswali nyuma ya Imaam anafaa amfuate Imaam anavyoswali na ikiwa atashindwa kusimama, hivyo akiswali kwa kukaa na maamuma wataswali kwa kukaa.

((Wakati Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa mgonjwa aliswali kwa kukaa na akawaamuru wanaoswali nyuma yake pia kukaa)) (Imepokewa na al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Anas bin Maalik [Radhiya Allaahu 'anhu]).

((Imepokewa kwa Jaabir bin Abdillaah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipanda farasi Madinah. Farasi huyo alimwangusha kwenye mzizi wa mtende, hivyo mguu wake kuumia. Tulimzuru ili kujua hali yake na tukamkuta akiswali kwa kukaa katika chumba cha mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha). nasi tulisimama kuswali nyuma yake. Alinyamaza kimya. Tulimtembelea tena ili kumjulia hali tukamkuta anaswali Swalah ya faradhi kwa kukaa. Tulisimama nyuma yake naye akatuashiria tukae nyuma yake, nasi tukakaa. Alipomaliza Swalah alisema: “Imaam anaposwali kwa kukaa, nanyi swalini kwa kukaa na Imaam akiswali kwa kusimama swalini hivyo pia. Musiwe kama watu wa Fursi walipokuwa wakiamiliana na watemi (viongozi) wao (yaani watu walikuwa wanasimama nao walikuwa wanaketi))” (Abu Dawud).

Hadiyth hizi za kuonyesha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaagizia Masahaba wawe ni wenye kumfuata Imaam ni nyingi, hivyo Imaam akipiga takbiyr maamuma pia wafanye hivyo. Imaam akiswali kwa kukaa watu pia nao waswali kwa kukaa (al-Bukhaariy na Abu Dawud, Maalik).

Mtu anaweza kuswali Swalah ya Nafli kwa kukaa au kwa kusimama, kwani si wajibu kusimama kwayo. Hili limethibiti kutoka kwa

((Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alikuwa akiswali kwa kukaa na kusimama bila udhuru wowote)) (Imepokewa na Muslim kutoka kwa mama wa waumini ‘Aaishah na pia Abu Hurayrah [Radhiya Allaahu 'anhu]).

Watangu wema (Salafu Swaalih) pia walikuwa wakifuata mwendo huo, Yahya anasema, Maalik anasema alisikia kuwa Urwa ibn az-Zubayr na Said ibn al-Musayyab walikuwa wakiswali Swalah za Sunnah kwa kukaa.

Hivyo, ikiwa mtu ameshindwa kuswali kwa kusimama ataswali kwa njia ambayo anaiweza.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share