Anataka Kuongeza Mke Mwengine Ingawa Mkewe Hana Matatizo Naye

 

SWALI:

ASAALAAM ALEYKOOM WA BAAD. MASHEIKH WANGU WAPENDWA SUALA LANGU NI KAMA IFUATAVYO:

1-Nikiwa Mume na nimeishi na mke wangu zaidi ya miaka saba na Alhamdulillah, tumejaaliwa kupata watoto watatu, na Mke wangu kwa tabia na akhlaaq ni njema kabisa. Na wala hana walakini wowote ule, lakini nimependana na Mwanamke mwengine, ambaye hayupo mbali na familia yetu, na yeye amekubali nimuowe, na kukhofia tusije kufanya maovu na kwenda kinyume na maadili yetu ya kiislaam, ambapo mimi nimeshindwa kabisa kuzizuia shahawa zangu, na uwezo
Alhamdulillah Mwenye Enzi Mungu amenijaalia kwa kiasi fulani-je! Kisheria itawezekana kumuoa?

2-Huyu Mke wangu ni mwenye wivu sana, Je! kama hatopenda niongeze mke mwengine, je! inawezekana kumuoa Kisiri? inshaallah natumai nimeeleweka. ahsantum

 


JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'Alayhi Wa Aalihi Wasallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'Anhum)   na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tunamuomba Allah (Subhaana Wa Ta'aalah) Awazidishie mapenzi baina yenu na mumwe ni wenye kutekeleza kwa pamoja majukumu yenu ya kuwalea watoto wenu kwa malezi mazuri ya Kiislamu. Kwa hakika, Uislamu tayari umempatia mume ruhusa ya kuongeza mke mwengine pindi anapoona kuwa amefikia haja hiyo na kumuepusha yeye na zinaa. Allah (Subhaana Wa Ta'aalah) Anasema:

((فَانكِحُواْ مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاء مَثْنَى وَثُلاَثَ وَرُبَاعَ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً ))

 ((Basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu)) (4: 3).

Hapa tungependa pia kutoa nasaha na kukumbusha kuwa mwanamme ambaye anataka kuoa zaidi ya mke mmoja ni lazima afanye juhudi ya kutekeleza uadilifu baina yao. Uadilifu si kuwa na hela peke yake bali pia ni kuwagawia siku sawa, kuwapatia makazi sawa, na mambo mengine. Isiwe kuwa kwa mke wa pili unaenda kisiri siku moja kwa wiki lakini kule kwengine unakuwa ndio unatumia muda wako mwingi. Ikiwa ndoa itakuwa hivi itakuwa hujafanya uadilifu kwa mke mdogo, hivyo kukufanya upate adhabu siku ya Kiyama.  

Kuhusu swali lako hili la pili,  hii ni kawaida kwa wanawake kwani hakuna hata mmoja ambaye anakubali mume wake amuolee mke wa pili. Japokuwa wakati mwengine huwa ni wenye kuwaambia waume zao ikiwa munataka kuoa oeni. Katika Uislamu hakuna ndoa ya siri kwani yapo masharti ya kusihi ndoa, miongoni mwazo ni: -

1.       Idhini ya baba au walii wa binti anayeolewa.

2.       Mashahidi wawili waadilifu.

Swali linakuja ni kuwa, je yule mke wa pili utampatia haki zake ambazo tumezieleza katika swali la kwanza? Ikiwa utatekeleza masharti haya mawili itakuwa ndoa hii haitakuwa siri tena, lile ambalo limebaki ni kuweza kumfanyia uadilifu kama kuwagawia siku au muda baina ya hao wake wawili. Na haki ya kupenda au kukataa ni ya mume si ya mke, lakini kwa ule uhusiano mwema baina wewe na mke wako wa kwanza unaweza kumueleza kuhusu nia yako ili yasije yakatokea matatizo kwa kusikia kutoka kwa watu wengine. Ikiwa atakataaa basi mpe muda na uendelee kuzungumza naye kwa njia ambayo ni  nzuri  au kuwatuma watu ambao wako karibu naye na kumueleza kuhusu hukumu ya kisheria kuhusu jambo hilo. Ni matumaini yetu kuwa kwa kufanya hivi huenda kukapatikana nusra na hivyo kuwepo maelewano mazuri.

Mara nyingi mume anapooa mke wa pili ambaye ni mdogo kuliko wa kwanza huwa anampenda zaidi. Na hili ni jambo ambalo halifai kabisa kufanywa na mume Muislamu. Tunamuomba Allah (Subhaana Wa Ta'aalah) Akufanikishie shughuli yako hii na ampatie mkeo uoni wa kukubali na kutofanya vurugu lolote, na pia akuwezeshe kufanya uadilifu na kujiepusha na zinaa.

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share