Adabu za Kuchunga Katika Nyumba za Allaah (Misikiti)

Adabu Za Kuchunga Katika Nyumba Ya Allaah (Misikiti) 

 

Imefasiriwa Na: Abuu Nawwaaf

 

Alhidaaya.com

 

 

Bismillaahi Rahmaani Rahiim

 

Kila Muislamu anaujua utukufu wa nyumba za Allaah. Msikiti ulikuwa ni katika mambo ya mwanzo ambayo Rasuli Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyasimamia mara alipofika Madiynah. Ni pahala ambapo Waislamu (wanaume) hukutana kila siku ili kuitekeleza nguzo ya pili ya Dini ya Kiislamu. Ni pahala ambapo elimu na busara vinatolewa na kugawanywa kutoka humo. Ni pahala ambapo Waislamu hupokea ujumbe wa wiki (khutbah za Ijumaa), kuhusiana na wajibu wao kwa Allaah, kwao wao wenyewe, kwa familia zao, na kwa viumbe wengine waliobakia.

 

Nyumba za Allaah zina sifa tulizotaja hapo juu na nyingine nyingi. Kwa msingi huo basi, tumeona ipo haja ya kujikumbusha, sisi wenyewe, na ndugu zetu wengine katika Uislam, juu ya baadhi ya adabu na kanuni zinazohusiana na kuhudhuria (kukaa) katika Msikiti (Masjid). Yafaa kuzingatia kuwa, hizi ni nyumba za Allaah, na pamoja na kuwa Yeye (Azza wa Jalla) yuko juu (kwamba hawezi kuishi ndani yake), kiuhalisia, zimejengwa kwa lengo maalumu la kumuabudia Yeye, na kwa hiyo, zinapaswa kuheshimiwa na kuadhimishwa na wale wanaohudhuria (katika Misikiti hiyo).

 

Kwa kuzingatia lengo hili, tumekusanya Makala hii fupi, inayohusiana na adabu za kuhudhuria nyumba za Allaah. Tunaomba na ni matarajio yetu kuwa kazi hii itainufaisha jamii ya Kiislamu na itabakia kuwa ukumbusho kwa wale ambao inawezekana wamesahau utukufu wa Msikiti.[1]

 

 

 Faida Na Umuhimu Wa Msikiti (Nyumba Ya Allaah)

 

Nyumba za Allaah zina faida na Baraka ambazo hazipatikani katika jengo lingine lolote juu ya uso wa Dunia. Faida na Baraka hizi ni nyingi sana, na si tu kuwa zinapatikana kwa kuingia Msikitini, bali hata kabla ya mtu kuingia, kama ameweka niyyah ya kwenda Msikitini, anaanza kuchuma Baraka (hizo) punde tu anapotoka nyumbani kwake. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Atakayetoka (atakayekwenda) Msikitini, Allaah Atamuandalia sehemu (makazi) katika pepo, kila mara aendapo Msikitini.” [Swahiyh Al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim].

 

Amesema pia:

 

“Yeyote mwenye kuchukua wudhuu nyumbani kwake, kisha akatoka kuelekea Msikitini kwa niyyah ya kutekeleza Swalah ya faradhi, hatua zake zitakuwa njia ya yeye kufutiwa madhambi. Hatua moja itafuta dhambi moja, ilhali hatua nyingine (itakuwa sababu ya yeye kuongezewa) thawabu.” [Swahiyh Muslim].

 

Pia ilitokea katika kipindi cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kuwa:

 

“Mtu mmoja alikuwa akiishi mbali (na Msikiti), lakini alikuwa akijitahidi sana kuhudhuria Swalah za jamaa’ah katika Msikiti. Baadhi ya watu wakamshauri: “Kwa nini usinunue punda ili uwe unampanda (wakati wa kwenda Msikitini), hasa nyakati za usiku na (kunapokuwa na) joto kali? Akajibu: Sitaki kufanya hivyo. Ninatumai kuwa hatua zangu (ninazotembea) kuja Msikitini zinaandikwa (kama matendo mema), na pia hatua zangu wakati ninaporudi kwa familia yangu (baada ya Swalah) zinaandikwa (kama matendo mema). Baada ya kusikia haya, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Allaah Ameyaandika yote mawili kwa ajili yako.” [Swahiyh Muslim].

 

 Ama kuhusiana na faida zinazopatikana baada ya kuingia Msikitini, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Malaika huendelea kumuombea mtu ambaye anabakia katika Msikiti alioswalia, muda wa kuwa hajatokwa na upepo(kutenguka wudhuu). Malaika husema: Ee Allaah msamehe (mja) huyu! Ee Allaah mrehemu (mja) huyu.” [Swahiyh Al-Bukhaariy].

 

Umuhimu wa Msikiti unajulikana pia kwa makafiri. Kama mtu atafuatilia kiundani historia ya vita baina ya Waislamu na wakatoliki, atagundua kuwa, hata mpaka leo hii, pindi makafiri wanapotaka kuvamia au kupigana na nchi ya Waislamu, moja ya maeneo ya mwanzo kushambuliwa (kuharibiwa) ni Msikiti. Hii ni kwa sababu makafiri wanautambua umuhimu wa Misikiti katika kuiunganisha na kuifundisha jamii ya kiislamu.

 

 

Kabla Ya Kuingia Msikitini

 

 

1. Muislamu anapaswa kutambua kuwa lengo kuu la Misikiti ni kwa ajili ya kuabudiwa Allaah (ndani yake). Kwa kuzingatia hili, inafaa kwa mtu kuweka niyyah sahihi kabla ya kuingia katika nyumba hii ya ‘ibaadah. 

 

Allaah (Azza wa Jalla) amesema katika Qur-aan kuhusiana na Misikiti:

 

 

فِي بُيُوتٍ أَذِنَ اللَّـهُ أَن تُرْفَعَ وَيُذْكَرَ فِيهَا اسْمُهُ يُسَبِّحُ لَهُ فِيهَا بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ

 

Katika nyumba ambazo Allaah Ameidhinisha litukuzwe na litajwe humo Jina Lake; wanamsabihi humo asubuhi na jioni. [An-Nuwr: 36].

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuhusiana na Misikiti:

 

"Kwa hakika nyumba za Allaah zimejengwa kwa ajili ya kumkumbuka (kumtaja) Allaah, kuswalia, na kusomea Qur-aan." [Swahiyh Muslim].

 

 

Kwa hiyo ni wajibu kwa Muislamu kutambua kuwa lengo la Misikiti si kwa ajili ya mikusanyiko ya kijamii na mazungumzo (yasiyohusiana na Msikiti), bali ni eneo lililoteuliwa na Allaah (Azza wa Jalla) kwa ajili ya kuabudiwa Yeye, kutajwa jina Lake, na kusomwa kitabu Chake. Mtu anyeingia Msikitini na akatoka, anatakiwa kujihisi ongezeko hasa la kiimani. Baada ya kuondoka Msikitini, kiwango chake cha imani na taqwa (Uchaji Allaah) kinatakiwa kuwa juu kuliko mwanzoni alipoingia Msikitini. Allaah (Azza wa Jalla) Amesema katika Kitabu Chake kitukufu:

 

إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ

 

Hakika Swalaah inazuia machafu na munkari.  [Al-‘Ankabuwt: 45].

 

2.  Ni lazima kwa mtu anayetaka kwenda Msikitini kuhakikisha kuwa hana (hatoi) harufu mbaya. Hii ni kutokana na kauli ya Allaah katika Qur-aan:

 

يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ

 

“Enyi wana-Aadam! Chukueni mapambo yenu katika kila Masjid (mnapokwenda Misikitini kwa ajili ya ‘ibaadah)” [Al-A‘raaf: 31].

 

 

Pia, maneno ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Yeyote aliyekula vitunguu vyeupe (vitunguu thaumu) au vitunguu vya kawaida (vitunguu maji) asihudhurie Msikitini." [Swahiyh Al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim].

 

 

Ushahidi tulioutoa hapo juu unatudhihirishia kuwa ni wajibu kwa Muislamu kuhakikisha kuwa hatowaudhi watu wengine kutokana na harufu (mbaya) ya mwili (wake) anapohudhuria Msikitini, na kwa hiyo, anapaswa kujitahidi kadiri awezavyo kujisafisha kabla ya kuhudhuria Swalah katika nyumba ya Allaah. Wanachuoni wa Kiislamu wanasisitiza juu ya katazo hilo tulilolitaja na kwamba linaenea zaidi pia kwa uvutaji sigara, kutokana na harufu mbaya ya sigara anayobaki nayo mvuta sigara mara tu amalizapo kuvuta sigara. Harufu hii (ya sigara), bila shaka, ina madhara na huwasumbua wanaoswali katika Msikiti, na pia huwasumbua (huwaumiza) Malaika. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 

Kwa hakika Malaika huumia kwa kile ambacho huwaumiza bin Aadam.” [Swahiyh Muslim].

 

 

3.  Wakati wa kwenda Msikitini, haifai kwa mtu kuharakisha na kukimbia, bali aende kwa mwendo wa kawaida. Hii ni kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Utakaposikia adhana (mwito wa Swalah) utembee kuelekea Msikitini katika hali ya utulivu, kwa amani, na usiharakishe. Utakachodiriki (katika Swalah), basi swali, na kile ambacho utakikosa, kimalizie.” [Swahiyh Al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim].

 

 

Wakati Wa Kuingia Msikitini

 

 

Ukiingia Msikitini anapaswa kuzingatia taratibu (adabu) zifuatazo:

 

 

i.  Kutanguliza Mguu Wa Kulia Kwanza

 

Swahaba maarufu wa Nabiy, Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

“Ni katika Sunnah, kuwa mtu anapoingia Msikitini basi atangulize mguu wake wa kulia, na (anapotoka), atoke kwa kutanguliza mguu wake wa kushoto.” [Mustadrak Al-Haakim].

 

 

Na imenukuliwa pia, kuwa ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa na mtazamo huo huo. [Swahiyh Al-Bukhaariy].

 

 

ii.  Du’aa (Ya Kusoma) Unapoingia Msikitini

 

 

Hii inapatikana katika Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Mmoja wenu anapoingia Msikitini, basi aseme: Allaahumma iftah liy ab-waaba rahmatik (Ee Rabb! Nifungulie milango ya Rahmah Zako).” [Swahiyh Muslim]

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema pia:

 

“Atakapoingia mmoja wenu Msikitini, aniswalie mimi, na kisha aseme: Allaahumma iftah liy abwaaba rahmatik (Ee Allaah, nifungulie mimi milango ya Rahmah Zako).” [Sunan Abi Daawuwd].

 

 

iii.      Kuswali Rakaa 2 Kabla Ya Kukaa (Tahiyyatul Masjid)

 

 

Uthibitisho wa haya nimaneno ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

“Mmoja wenu atakapoingia Msikitini, aswali rakaa mbili kabla ya kukaa.” [Swahiyh Al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim].

 

 

iv.   Kuswali Nyuma Ya Sutrah (Kizuizi)

 

Sutra ni kizuizi kinachomsaidia mtu anayeswali kutomruhusu mtu mwingine kupita mbele yake. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Mmoja wenu anaposwali, basi asimame nyuma ya sutrah na aswali karibu na hiyo sutrah. Hii ni kwa ajili ya kumzuia shaytwaan asimsumbue katika Swalah yake. [Sunan Abi Daawuwd].

 

 

 

v.  Mtu Ajitahidi Kadiri Awezavyo Kupata Nafasi Katika Safu Ya Kwanza[2]

 

 

Hii ni kutokana na maneno ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Lau watu wangelijua malipo makubwa yapatikanayo kwa kuitikia mwito wa Swalah (adhana), na kuswali katika swafu ya kwanza, basi wangeshindania kupata nafasi katika swafu ya kwanza.” [Swahiyh Al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim].

 

Amesema pia:

 

“Bora ya swafu kwa wanaume ni swafu ya kwanza.” [Swahiyh Muslim].

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipata kuwaona baadhi ya Swahaba zake wakiwa wamekaa (swafu) ya nyuma ya Msikiti punde tu, kabla ya kuanza kwa Swalah. Alipoona hivyo, alisema:

 

“Watajivuta na kujichelewesha (kuendea swafu ya kwanza) mpaka Allaah Atawachelewesha (kuingia peponi).[3] [Swahiyh Muslim].

 

 

vi.   Kurudia (Maneno) Baada Ya Muadhini

 

Hii ni kutokana na maneno ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Utakapoisikia adhana, sema kama asemavyo Muadhini.” [Swahiyh Al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim].

 

 

vii.   Du’aa Baina Ya Adhana (Mwito Wa Swalah) Na Iqaamah

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameujulisha ummah wake nyakati tofauti ambazo du’aa zina uwezekano mkubwa wa kukubaliwa na Allaah. Moja ya nyakati hizo ni baina ya adhana na iqaamah. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Du’aa inayoombwa baina ya adhana na iqaamah haitokataliwa.” [Musnad Imaam Ahmad].

 

 

viii. Kusoma Qur-aan Na Kumtaja Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

 

Tumeshaonesha awali katika Makala hii, maneno ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa:

 

 

“Kwa hakika nyumba za Allaah zimejengwa kwa ajili ya kumtaja Allaah, Swalah, na kusomwa Qur-aan (ndani yake).” [Swahiyh Muslim].

 

 

ix. Kujitahidi Kuhudhuria Mikusanyiko Ya Kielimu (Duruus Za Misikitini)

 

 

Haya ni kutokana na maneno ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

“Hakikusanyiki kikundi cha watu katika nyumba ya Allaah, wakisoma Kitabu Chake na kufundishana wenyewe kwa wenyewe isipokuwa utulivu hushuka juu yao, Malaika huwazunguka, Rahmah huwateremkia, na Allaah Huwataja katika mjumuiko Wake (mbele ya Malaika).” [Swahiyh Muslim].

 

Pia maelezo ya ujumla ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa:

                                                                                                                                                      

“Yeyote mwenye kuifuata njia (kwa ajili ya) kutafuta elimu, Allaah Atamfanyia wepesi njia yake kuelekea peponi.” [Swahiyh Muslim].

 

Kutokana na Hadiyth hiyo hapo juu, ni sawa kusema kuwa, ikiwa mtu ataondoka nyumbani kwake akiwa na niyyah ya kuswali (Swalah kwa) Jamaa’ah na pia akiwa na niyyah ya kutafuta elimu Msikitini, kwa kupenda Kwake Allaah, atapata malipo makubwa sana kutokana na ukweli kuwa amekusanya mambo (matendo) mawili makubwa Ayapendayo Allaah (Azza wa Jalla).

 

 

x. Ni Wajibu Kwa Misikiti Kuwa Misafi, Na Muumini Anatakiwa Ajitahidi Kadiri Awezavyo Kusaidia Hili

 

 

Hii ni kutokana na maneno ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) aliyesema kuwa, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliagiza kuwa Misikiti inapaswa kusafishwa na kufukizwa (manukato mazuri). [Musnad Imaam Ahmad].

 

 

Mambo Ya Kuepuka Wakati Wa Kutembelea Masjid (Misikiti)

 

Matendo ya Muumini wakati anapotembelea nyumba za Allaah yanatakiwa kuwa tofauti na matendo yake ya kawaida nje ya Misikiti. Hii ni kutokana na uelewa wake juu ya utukufu wa nyumba hizi (Misikiti). (Mja) Huzingatia mara zote kuwa, anatembelea sehemu ambayo imewekwa kwa ajili ya kumuabudu Allaah, na kwa hiyo, kila kinachofanyika ndani yake kinatakiwa kimuwezeshe mja kuwa karibu zaidi na Allaah.

 

Baada ya hayo, matendo yafuatayo yamekatazwa (ni haraam kufanyika Misikitini)

 

 

a.   Kununua Na Kuuza Ndani Ya Msikiti[4]

 

Haya yametajwa katika kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Ukimuona mtu akinunua au akitafuta kununua ndani ya Msikiti, sema kumwambia: ‘(Namuomba) Allaah asiibariki biashara yako’.” [Swahiyh Muslim].

 

 

b. Kuongea Kwa Sauti Kubwa Au Kuongelea Masuala Yasiyo Na Umuhimu (Misikitini)[5]

 

Sa’iib bin Yaziyd amesema: “Nilikuwa nimesimama Msikitini siku moja niliposikia mtu akinishika. Nilipogeuka nikamuona kuwa alikuwa ni ‘Umar bin Al-Khatwaab. Alinielekeza nimpelekee watu wawili waliokuwa wamekaa Msikitini wakiongea kwa sauti kubwa. Nilipompelekea watu wale wawili, ‘Umar akawauliza: Mnatokea wapi? Wakajibu: Tunatokea Twaaif. ‘Umar akasema: Mngekuwa mnatokea katika mji huu, ningewapiga. Mlikuwa mnanyanyua sauti zenu (sana) katika Msikiti wa Nabiy!” [Swahiyh Al-Bukhaariy].

 

Sa’iyd bin Musayyib amesema:

 

“Pindi mtu anapokaa Msikitini, kwa hakika anakaa kwa ajili ya kumuabudu Rabb wake, kwa hiyo, aongee tu kwa lile ambalo ni jema.” [Tafsiyr Al-Qurtwubiy].

 

Yafaa pia kuwakumbusha wale ambao huenda na watoto katika nyumba za Allaah kuwa, wanawajibika kuwasimamia watoto wao na kuhakikisha kuwa tabia zao (watoto) haziwasumbui watu wengine wafanyao ‘ibaadah. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Kila mmoja wenu ni mchunga, na kila mmoja mmoja ataulizwa kuhusiana na wale walio chini ya uangalizi wake. [Swahiyh Al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim]

 

Ingawa Hadiyth hii ina maana ya ujumla, bila shaka, inatumika pia kwa wale ambao wanakwenda na watoto katika nyumba za Allaah. Mzazi (Mlezi) anatakiwa kuwafundisha wale walio chini yake, tabia (taratibu) njema za kutembelea nyumba ya ‘ibaadah. Asimruhusu mtoto wake kukimbia kimbia ovyo Msikitini (hali itakayopelekea) kuwasumbua wengine wenye kujikurubisha kwa Allaah. Kama mtoto ni mdogo sana na hawezi kuzielewa taratibu hizi (za kukaa Msikitini), basi ni bora kumuacha nyumbani kuliko kuwabughudhi wengine walioko Msikitni.

 

 

c. Kusoma Qur-aan Kwa Sauti Kiasi Ambacho Inawasumbua Wengine Wanaofanya ‘Ibaadah

 

Abu Sa’iyd Al-Khudriyy ameripoti kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwasikia baadhi ya watu wakisoma Qur-aan kwa sauti kubwa (wakiwa) Msikitini, kwa hili akawaambia:

 

“Kila mmoja wenu anakusudia kumuomba Rabb wake, kwa hiyo msikwazane, wala msinyanyue sana sauti zenu mnaposoma (Qur-aan)” [Sunan Abi Daawuwd].

 

Katika Hadiyth hii kuna katazo la wazi kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kuwabughudhi wengine Msikitini, sasa vipi kwa wale wanaowabughudhi wengine kwa mazungumzo yasiyo na maana (porojo), miziki kwenye simu zao za mkononi (rununu), vicheko na utani (mizaha), na kadhalika?! Hapana shaka kuwa kusoma Qur-aan ni moja katika matendo yenye kupendeza mbele ya Allaah, lakini pamoja hadhi yake kubwa katika Uislam, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu kuisoma kwa sauti ambayo itawabughudhi wengine wenye kufanya ‘ibaadah zao. Hii inatubainishia kuwa wale ambao huwabughudhi wengine kwa mambo (masuala) yenye hadhi ya chini ya Qur-aan watakuwa wamefanya makosa makubwa.[6]

 

 

d.     Kupita Mbele Ya Mtu Anayeswali[7]

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Lau mtu anayepita mbele ya mtu anayeswali angelijua uzito wa kosa lake hilo, ingelikuwa bora kwake kusubiri arobaini kabla ya kupita mbele ya mtu anayeswali.” [Swahiyh Al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim].

 

 

 Kutoka Msikitini

 

I.     Du’aa Ya Kusoma Wakati Wa Kutoka Msikitini

 

Hii ni kutokana na maneno ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Mmoja wenu anapotoka Msikitini aniswalie mimi na aseme: Allaahumma inniy as-aluka min fadhwlik. Ee Allaah! Ninakuomba fadhila Zako.” [Swahiyh Muslim].

 

 

II. Kuwa Unatoka (Unaondoka) Katika Nyumba Ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

 

Tumerejea mara kwa mara katika Makala haya kuwa mtu anayeingia Msikitini alenge zaidi kujikurubisha kwa Rabb wake. Muda wote wa kuwa kwake Msikitini anapaswa awe ameswali, kuomba du’aa, kumtaja Allaah, na ikiwezekana awe amesikiliza kitu katika elimu ya Dini ambacho kitamnufaisha katika maisha haya na yajayo (Aakhirah). Kwa hiyo, tabia yake wakati wa kutoka katika nyumba ya Allaah inatakiwa (inatarajiwa) kuwa bora zaidi na tofauti (yenye mfano mzuri). Watangu wetu wema (Salafus-Swaalih) wametujulisha kuwa ishara ya kuwa ‘ibaadah ya mtu imekubaliwa na Allaah ni kuwa matendo ya mja baada ya kutekeleza ‘ibaadah (inakuwa) ni bora na yenye kupendeza zaidi. Kama aliyefanya ‘ibaadah hajihisi kuongezeka iymaan (baada ya kutekeleza ‘ibaadah), inawezekana kuwa hazifanyi ‘ibaadah zake katika utaratibu unaokubalika (unaofaa) kishari’ah, kwa hiyo ajitathmini matendo yake kabla na wakati wa kuitenda (kuitekeleza) ‘ibaadah.

 

 

Kwa Kumalizia

 

Hizi ni adabu (taratibu) chache tu za kuchunga ambazo tumehisi kuna haja ya kujikumbusha, sisi wenyewe na ndugu zetu, kwani zinahusiana na (taratibu na adabu za) kuhudhuria katika nyumba za Allaah.

 

Allaah ni mjuzi zaidi. Swalah na Salaam za Allaah ziende juu ya Rasuli na Nabiy Wake wa mwisho, na juu ya familia yake na Swahaba zake.

 

 

[1] Hadiyth nyingi zilizopo katika Makala hii zimechukuliwa kutoka katika kitabu: Riyaadh Asw-Swaalihiyn cha Imaam An-Nawawiy.

[2] Hii ni kwa wanaume na wanawake kama kutakuwa na kizuizi (kitenganishi) chenye kutenganisha wanaume na wanawake. Kama hakuna kitenganishi, wanawake wanatakiwa waswali swafu za nyuma zaidi (ndiyo bora kwao).

[3] Hii imetajwa kama makameo kwa wale ambao mara nyingi hujivuta kuiendea swafu za kwanza.

[4] Hili linajuilisha pia uwekaji wa matangazo ya biashara (kutangaza bidhaa na huduma) katika Misikiti.

[5] Hili halihusishi kunyanyua sauti wakati wa khutbah na madarasani.

[6]  Kwa hakika inatuhuzunisha sana kusikia baadhi ya mambo yanayotokea ikiwemo kupigana, kuzozana, n ahata kutishana kwa silaha, katika baadhi ya Nyumba za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)!! Hili kwa hakika ni kos ana ni uhaini mkubwa na wale ambao huyafanya haya wanapaswa kutubia kwa Rabb wao na kumuomba msamaha.

 

[7]  Hili linamjuilisha Imaam (anayeongoza Swalah), au mtu anayeswali peke yake. Halimhusu mtu anayewali nyuma ya Imaam (Sutra ya Imaam inatosheleza).

 

 

Share