Shaykh Ahmad Bin Yahyaa An-Najmiy

 

Jina Lake:

 

Alikuwa Mwanachuoni mkubwa, bingwa katika Hadiyth na Fiqh, Muftiy maeneo ya Jaazaan kusini mwa Saudi Arabia. Shaykh Ahmad bin Yahyaa bin Muhammad bin Shabiyr An-Najmiy, kutoka kabila la Banuu Hummad moja ya kabila maarufu katika maeneo ya Jaazaan.

 

 

Kuzaliwa Kwake Na Mwanzo Wa Masomo Yake:

 

Shaykh alizaliwa katika kijiji cha an-Najaamiyyah tarehe 22 Shawwaal 1346 H katika familia ya wazazi wawili wema ambao hawakupenda afanye kazi kama mtoto kwa sababu apate muda wa kusoma. Alianza kujifunza kusoma, kuandika na kuhifadhi Qur-aan alipokuwa mtoto. Baada ya hapo kukaja Shaykh mkubwa 'Abdullaah al-Qar'aawiy na kujadili na mwanachuoni wa Ash'ariy katika maeneo yao mpaka hapo haki ikadhihiri na watu wakafahamu kuwa Sunnah ndiyo njia sahihi. Baada ya hapo akawa Shaykh Ahmad mwanafunzi wa karibu wa Shaykh al-Qar'aawiy ambaye alikuwa ameanzisha madrasah ya Salafi katika mji wa Samitah. Shaykh alisoma 'Aqiydah, Fiqh, Hadiyth, Urithi wa Kiislamu, Mustwalah na masomo mengine ya Kiislamu pamoja naye.

 

 

Waalimu Wake:

 

1) Shaykh 'Abdullaah Al-Qar'aawiy aliyekuwa mhuishaji wa Sunnah kusini mwa Saudi Arabia na kuanzisha maelfu ya madrasah za kidini nchini Saudi Arabia na Yemen.

 

2) Shaykh Al-Haafidhw Al-Hakamiy, bingwa wa Mwanachuoni ambaye alifariki umri wa miaka 35 na aliandika vitabu vya aina yake katika mambo mbalimbali ya Kiislamu.

 

3) Shaykh Muhammad bin Ibraahiym. Muftiy wa Saudi Arabia wa zamani. Alisoma sehemu ya Tafsiyr Atw-Twabariy pamoja naye.

 

 

Wanafunzi Wake:

 

Shaykh alifundisha takriban miaka 50 na idadi kubwa ya wanafunzi walisoma kwake, katika hao baadhi yao ni Maulamaa wetu wakubwa leo. Miongoni mwao ni:

 

1) Shaykh Rabiy´ bin Al-Haadiy Al-Madkhaliy.

 

2) Shaykh Zayd bin Muhammad Al-Madkhaliy, Mwanachuoni mkubwa kusini mwa Saudi Arabia aliyeandika vitabu vya kina juu ya ´Aqiydah, Fiqh na Uswuwl-ul-Fiqh.

 

3) Shaykh 'Aliy bin Naaswir Al-Faqiyhiy ambaye ni mwalimu katika Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na huchukuliwa ni mmoja katika Wanachuoni wakubwa wa Madiynah.

 

 

Vitabu Vyake:

 

Shaykh ameandika vitabu maarufu vingi, miongoni mwavyo ni:

 

1) Ta'siys Al-Ahkaam Sharh 'Umdat-il-Ahkaam ambacho ni mjaladi tano tafsiri ya kitabu cha ´Umdat-ul-Ahkaam. Mjaladi wa kwanza alieleza Shaykh Al-Albaaniy kuthibitisha kiwango chake katika elimu.

 

2) Al-Mawrid Al-Adh’b Az-Zilaal Fiymaa Intaqada 'alaa Ba'adhwil-Manaahij Ad-Da'wiyyah min Al-'Aqaa'id wal-A'amaal.  Kitabu muhimu sana ambapo Shaykh anaelezea Da´wah ya Salafiyyah wakati huo huo anapiga radd makundi mawili; Jamaa'at-ut-Tabliygh na Al-Ikhwaan Al-Muslimuwn.

 

3) Awdhwaah Al-Ishaarah fiyr-Radd ´alaa Man Abaahal Mamnuw’ minaz-Ziyaarah. Kitabu muhimu kinachohusu kutembelea makaburi.

 

4) Tanziyh Ash-Shariy'ah 'an Ibaahatil-Aghaaniy Al-Khaliy'ah.

 

5) Risaalah fiy Hukmil-Jahr bil-Basmalah.

6) Fat-h Ar-Rabb Al-Waduwd fiyl-Fataawaa war-Ruduwd.

 

7) Risaalah Al-Irshaad ilaa Bayaanil-Haqq fiy Hukmil-Jihaad.

 

 

Kifo Chake:

 

Shaykh kafariki katika 23, Julai, 2008 baada ya kuwa mgonjwa kwa muda mrefu na alikuwa mmoja katika Wanachuoni wakubwa wa zama hizi.

 

Mukhtasari wa wasifu wake ambao mwanafunzi wake Shaykh Muhammad bin Al-Haadiy Al-Madkhaliy aliandika kama utangulizi wa kitabu cha Al-Mawrid Al-Adh’b Az-Zilaal (uk. 5-12) na baadhi ya nyongeza.

 

Share