001-Lu-ulu-un-Manthuwrun :Allaah Hatazami Miili Wala Sura, Bali Anatazama Nyoyoni

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 1

Allaah Hatazami Miili Wala Sura, Bali Anatazama Nyoyoni

www.alhidaaya.com

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ  (صلى الله عليه و آله وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ لاَ يَنْظُرُ إِلى أجْسَامِكُمْ  وَلاَ إِلَى صُوَرِكُمْ وَلَكِنْ يَنْظُرُ إِلَى قُلُوبِكُمْ)) رواه مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hakika Allaah Hatazami viwiliwili vyenu wala sura zenu, lakini Anatazama nyoyo zenu)) [Muslim]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 

1. Umuhimu wa kuwa na niyyah safi na ikhlaasw katika kumuabudu Allaah (سبحانه وتعالى) kwani hivyo ndivyo tulivyoamrishwa:

 

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara. [Al-Bayinah 98:5

 

 

2. Hima ya kutenda ‘amali njema baada ya kuwa na  niyyah safi.  

 

 

3. ‘Amali na ‘Ibaadah hazipokelewi isipokuwa niyyah ikiwa ni safi kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى). Kwa hiyo ‘amali zinazomshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) haizipokelewi. Aliwatahadharisha Rusuli na Manabii Wake Aliposema:

 

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٦٥﴾

  Kwa yakini umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako (kwamba): “Ukifanya shirki bila shaka zitabatilika ‘amali zako na bila shaka utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” [Az-Zumar: 65]

 

 

Na pia:

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٨٨﴾

Na kama wangemshirikisha bila shaka yangebatilika yale waliyokuwa wakitenda. [Al-An’aam: 88]

 

Na ‘amali zenye kumshirikisha hazina thamani yoyote mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 وَقَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا ﴿٢٣﴾

Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya ‘amali yoyote ile, Tutayafanya   chembechembe za vumbi zinazoelea hewani zinazotawanyika. [Al-Furqaan: 23]

 

Pia rejea: Al-Kahf (18: 103-104, 110).    

 

 

 

4. Bin Aadam hawezi kuficha kitu kwa Allaah, Anatambua yaliyomo nyoyoni mwa waja Wake hataka kama ni khiyaana ndogo vipi basi Yeye Anaitambua. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَعْلَمُ خَائِنَةَ الْأَعْيُنِ وَمَا تُخْفِي الصُّدُورُ

(Allaah) Anajua khiyana za macho na yale yanayoficha vifua [Ghaafir : 19)

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

قُلْ إِن تُخْفُوا مَا فِي صُدُورِكُمْ أَوْ تُبْدُوهُ يَعْلَمْهُ اللَّـهُ ۗ  

Sema: “Mkificha yale yaliyomo katika vifua vyenu au mkiyafichua, Allaah Anayajua.  [Aal-‘Imraan (3:29)]

 

Rejea pia: Aal-‘Imraan  (3: 119, 154), Al-Mulk (67: 13), At-Taghaabun (64: 4), Huwd (11: 5),

 

Na na siri zote zitadhihirika Siku ya Qiyaamah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَوْمَ تُبْلَى السَّرَائِرُ ﴿٩﴾

Siku siri zitakapopekuliwa. [Atw-Twaariq (86: 9)]

 

 

Na Anasema pia:

وَحُصِّلَ مَا فِي الصُّدُورِ ﴿١٠﴾

Na yatapodhihirishwa yale yaliyomo vifuani? [Al-‘Aadiyaat (100: 10)]

 

 

Rejea pia: Al-An’aam (6: 60), Al-Jumu’ah (62: 8), Az-Zumar (39: 7), Luqmaan (31: 23).  

 

 

 

5. Siku ya Qiyaamah mali wala watoto hayatamfaa mtu isipokuwa atakayefika akiwa na moyo msafi uliosalimika na maovu kadhaa yakiwemo riyaa (kujionyesha). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾

 “Siku hayatofaa mali wa watoto.

 

إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾

“Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika. [Ash-Shu’araa (26: 88-89)]

 

 

 

6. Ni muhimu kwa Muislamu kuzitekeleza amri za Dini yake na si kwa mandhari pekee. Na mara nyingi watu huwa ni wenye kusema pindi anapotenda jambo ovu kuwa: “Lakini niyyah yangu ni nzuri”. Hapa Muislamu anatakiwa aizingatie Hadiyth nyengine inayosema: ((Hakika Allaah Hatazami viwiliwili vyenu wala sura zenu, lakini Anatazama nyoyo na ‘amali zenu)) [Muslim]

 

Hivyo,‘amali zinafaa ziende sambamba na Aliyoyateremsha Allaah na kuja nayo Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

 

 

7. Usimhukumu mtu kwa mandhari yake, pindi ukimuona mtu shakili yake na hakuvaa mavazi ya Muumin ukadhania ni mtu muovu, huenda akawa ni mwema. Hali kadhalika, pindi ukimuona mtu shakili yake na mavazi yake ni ya ki-Muumin ukadhani kuwa ni mtu mwema kabisa, lakini huenda akawa ni mtu muovu. Wala usimdharau au kumkejeli mtu kwa mandhari yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَوْمٌ مِّن قَوْمٍ عَسَىٰ أَن يَكُونُوا خَيْرًا مِّنْهُمْ وَلَا نِسَاءٌ مِّن نِّسَاءٍ عَسَىٰ أَن يَكُنَّ خَيْرًا مِّنْهُنَّ ۖ  

Enyi walioamini! Wanaume wasiwafanyie dhihaka na kudharau wanaume wengineo asaa wakawa bora kuliko wao, wala wanawake kwa wanawake wengineo, asaa wakawa bora kuliko wao. [Al-Hujuraat (49: 11)]

 

 

8. Kuzingatia yanayomridhisha Allaah (سبحانه وتعالى) daima.

 

 

9-Kukhofia riyaa kwani ni hatari mno huporomosha ‘amali zote: Hadiyth:

 

عنْ ابي هريرة رضي الله عنه أنَّه صلَّى الله عليه وسلَّم قال: ((قال الله تعالى: أنا أغْنى الشُّركاء عن الشِّرْك، فمَن عمل عملاً أشْرَك فيه معي غيري تركتُه وشِرْكه))    

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Allaah Ta’aalaa Anasema: "Mimi Ni Mwenye kujitosheleza kabisa, Sihitaji msaada wala mshirika. Kwa hiyo, yule afanyaye amali kwa kunishirikisha na mtu, Nitaikanusha pamoja na mshirika wake.”))  Yaani: hatopata ujira wowote kwa amali hiyo. [Muslim (2985), Ibn Maajah (4202)]

 

 

Pia:

 

 عَنْ أَبِي سَعِيدٍ مَرْفُوعًا: ((أَلا أُخْبِرُكُمْ مَا هُوَ أَخْوَفُ عَلَيْكُمْ عِنْدِي مِنَ الْمَسِيحِ الدَّجَّالِ؟)) قَالُوا بَلَى: قَالَ: ((الشِّرْكُ الْخَفِيُّ، يَقُومُ الرَّجُلُ فَيُصَلِّي فَيُزَيِّنُ صَلاتَهَ، لِمَا يَرَى مِنْ نَظَرِ رَجُلٍ إِلَيْه)) رَوَاهُ أَحْمَدُ

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd, Hadiyth Marfuw’: ((Je, niwajulisheni nikikhofiacho zaidi juu yenu kuliko hata Masiyh Ad-Dajjaal?)) Wakasema: Ndio. Akasema: ((Ni shirki iliyojfichikana kama vile mtu kuipamba Swalaah yake kwa kuwa anaangaliwa)) [Ahmad, Ibn Maajah]

 

 

Share