Niko Kwenye Eda Ya Talaka Naweza kurudiana Na Mume Wangu?

 

SWALI:

Assalam alaikum,

Shukran kwa jawabu lenu, mashallah nimepata faida nyingi, jazakumullah kheir. Naelewa situation yenu, yaani kupata maswali mengi.Nina swali jengine hapa na naweza kusubiri jawabu mutakapo kuweza kunijibu.

Mume wangu ashanipatia talaka sasa kwa hivyo niko kwenye Iddah. Jambo hili halikuwafurahisha familia zote zetu mbili khususan babake. Ndugu zake wanajaribu kuzungumza nae na Jee ikiwa mume wangu atarijekebisha tabia yake mbovu, twaweza kurudiana? Na muna nasaha gani ya kunipatia? Wajazakumullah Alf Kheiran

 


JIBU:

 Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake, Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum)  na walio wafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa dada yetu aliyeuliza swali hili. Haya mas-ala ya ndoa na talaka ni mas-ala nyeti na kama tunavyokariri mara nyingi ndio chanzo chetu sisi kudidimia pindi tunapokosa kuelewana katika unyumba wetu. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatufahamisha ya kwamba mke anapopatiwa talaka anafaa asitoke katika nyumba yake hata kama nyumba ni miliki ya mume.

Hebu tutazame aayah hiyo: “Ee Nabii! Mtakapowapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao. Na fanyeni hisabu ya eda. Na mcheni Allaah Mola wenu i. Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Allaah, msiikiuke” (65: 1).

 

Mke anapopatiwa talaka ni lazima akae eda nyumba ya mumewe na wakati huo ni jukumu la mume kumlisha, kumvisha, kumtibu na kumpatia malazi mtalaka wake mpaka eda inapomalizika kama ambavyo ni mume na mke. Hekima ya hili ni kuwa inawapatia fursa ya watu hao wawili kuweza kujirudi na kufanya suluhu na kurudiana kabla ya eda haijamalizika. Mume anakuwa ni mwenye kutekeleza yote hayo lakini hana ruhusa ya kulala na mkewe na siku ambayo ataamua kufanya hivyo basi tayari watakuwa wamerudiana. Ikiwa eda itamalizika kabla ya kurudiana wakati wataamua kurudiana itabidi mume apeleke posa na atoe mahari mapya kwa mke.

 

Uislamu umeweka njia ya wanandoa kurudiana pindi inapotokea talaka. Kwa hakika ndugu zake mume wanafanya vizuri na tunawaombea kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) awajazi na awalipe kwa juhudi zao. Na ikiwa mume wako ana matatizo na anaweza kujirekebisha hizo tabia zake mbovu, mnaweza kurudiana tena ikiwa hiyo si talaka ya tatu. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

Talaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa vizuri” (2: 229).

 

Talaka ya pili inapotoka kwa mume inabidi wanandoa hao wakae kwa wema na vizuri kwani inapotoka talaka ya tatu huwa mume na mke hawawezi kurudiana mpaka mke aolewe na mume mwengine na wakutane kimwili. Akiachwa na mume huyo ndiyo mume wa kwanza anaweza kumrudia.

 

Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Na kama amempa talaka (ya tatu) basi si halali kwake baada ya hayo mpaka aolewe na mume mwengine. Na akiachwa basi hapana ubaya kwao kurejeana wakiona kuwa watashikamana na mipaka ya Allaah,  Na hii ni mipaka ya Allaah Anayoibainisha kwa watu wanaojua” (2: 230).

Sasa hii ikiwa si talaka ya tatu mnaweza kurudiana na lau ikiwa hii ni talaka ya tatu basi hamuwezi kurudiana tena mpaka uolewe na mume mwengine kisha uachwe.

 

Nasaha ambayo tunaweza kukupatia ni kuwa ikiwa matatizo ya mumeo ni madogo basi kurudiana ni kheri kwani yanaweza kurekebishwa. Lakini yakiwa ni makubwa kama kumshirikisha Allah (Subhaanahu wa Ta'ala), kutoswali, kunywa pombe na mengineyo inafaa apatiwe muda ili ajirekebishe ikiwa atajirekebisha itakuwa ni vyema kurudiana lau hatajirekebisha basi ni bora kukaa mbali ili kuweza kuilinda Dini yako. Na ni vyema mumeo apelekwe kwa wataalamu wanazuoni kwa ushauri na nasaha ili aweze kumsaidia kujirekebisha.

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share