038-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Allaah Anamuunga Anayeunga Kizazi Na Anamkata Anayekata Kizazi

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 38

 

Allaah Anamuunga Anayeunga Kizazi Na Anamkata Anayekata Kizazi

 

Alhidaaya.com

 

 

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((الرَّحِمُ مُعَلَّقَةٌ بِالْعَرْشِ،  تَقُولُ مَنْ وَصَلَنِي وَصَلَهُ اللَّهُ وَمَنْ قَطَعَنِي قَطَعَهُ اللَّهُ)) متفق عليه

 

Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaisha (رضي الله عنها) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ((Uterasi [fuko la uzazi] limetundikwa katika ‘Arshi, linasema: Anayeniunga Allaah Atamuunga, na anayenikata Allaah Atamkata)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

1. Jina la Allaah (سبحانه وتعالى) Ar-Rahmaan linahusiana na ‘rahm’ yenye maana ya: Uterasi (fuko la uzazi).

 

2. Allaah (سبحانه وتعالى) Amesisitiza sana kuunga kizazi kinachohusiana kwa damu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَالَّذِينَ يَصِلُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ وَيَخَافُونَ سُوءَ الْحِسَابِ ﴿٢١﴾

Na ambao wanaunga yale Aliyoamrisha Allaah kuungwa na wanamkhofu Rabb wao, na wanakhofu hesabu mbaya.  [Ar-Ra’d (13: 21)]

 

 

3. Mwenye kutaka radhi za Allaah (سبحانه وتعالى)  basi aunge kizazi.

 

4. Hatari ya kukata kizazi; undugu na ujamaa wa uhusiano wa damu ni kukatwa na kulaaniwa na Allaah (سبحانه وتعالى) kama Anavyosema:

 

فَهَلْ عَسَيْتُمْ إِن تَوَلَّيْتُمْ أَن تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَتُقَطِّعُوا أَرْحَامَكُمْ﴿٢٢﴾

Basi huenda nyinyi mkigeuka ndio mfanye ufisadi katika ardhi na kukata jamaa zenu wa uhusiano wa damu?

 

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَعَنَهُمُ اللَّـهُ فَأَصَمَّهُمْ وَأَعْمَىٰ أَبْصَارَهُمْ﴿٢٣﴾

Hao ndio ambao Allaah Amewalaani; Akawafanya viziwi na Akawapofua macho yao. [Muhammad: 22-23]

 

Rejea pia Al-Baqarah (2: 27).   

 

 

5. Kukata uzazi; undugu na ujamaa wa uhusiano wa damu, ni miongoni mwa dhambi kubwa kwa vile zinasababisha mtu kupata laana ya Allaah (سبحانه وتعالى).   

 

6. Mwenye kukata kizazi; undugu na ujamaa wa uhusiano wa damu, haingii Jannah kutokana na kauli ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  ((Haingii Jannah mwenye kukata udugu)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

6. Fadhila kadhaa kwa wenye kuunga undugu zimetajwa katika Hadiyth za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) mojawapo ni sababu ya kuongezewa umri mrefu na kuzidishiwa riziki na baraka:  ((Mwenye kupenda kutanuliwa rizki yake, na azidishiwe baraka katika umri wake aunge undugu wake)) [Al-Bukhaariy]  

 

Pia Hadiyth zifuatazo zimetaja fadhila nyinginezo: 

 

((Mwenye kumuamini Allaah na siku ya mwisho amkirimu mgeni wake, na mwenye kumuamini Allaah na Siku ya mwisho aunge undugu wake)) [Al-Bukhaariy] 

 

Kutoka kwa Abuu Ayuwb Al-Answaariy (رضي الله عنه) kwamba mtu alisema: “Ee Rasuli wa Allaah! Nifahamishe tendo litakaloniingiza Jannah na litakaloniepusha na Moto.” Akasema Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  ((Umwabudu Allaah wala usimshirikishe na chochote, usimamishe Swalaah utoe Zakaah na uunge undugu)) [Al-Bukhaariy]

 

7. Kuunga undugu kunahitajia azimio la nguvu ambalo lina faida kwa mwenye kutekeleza. Hadiyth: Alikwenda mtu kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)   akasema: “Ee Rasuli wa Allaah, mimi nina ndugu nawaunga wananikata, nawafanyia wema na wao wananifanyia maovu, nawa mpole kwao wananifanya mjinga. Akasema: ((ikiwa uko kama unavyosema kanakwamba unawalisha majivu ya moto, na hutoacha kuwa unaungwa mkono na Allaah, ukidumu kwa hilo)) [Muslim]

 

 

 

Share