050-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kafiri Analipwa Duniani Aakhirah Hatopata Kitu, Na Muumin Analipwa Duniani Na Aakhirah

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 50

Kafiri Analipwa Duniani Aakhirah Hatopata Kitu,

Na Muumin Analipwa Duniani Na Aakhirah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

عَنْ أَنَسِ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَال: ((إِنَّ الْكَافِرَ إِذَا عَمِلَ حَسَنَةً أُطْعِمَ بِهَا طُعْمَةً مِنْ الدُّنْيَا، وَأَمَّا الْمُؤْمِنُ فَإِنَّ اللَّهَ يَدَّخِرُ لَهُ حَسَنَاتِهِ فِي الأَخِرَةِ وَيُعْقِبُهُ رِزْقًا فِي الدُّنْيَا عَلَى طَاعَتِهِ)) 

وفي رواية: ((إِنَّ اللَّهَ لاَ يَظْلِمُ مُؤْمِنًا حَسَنَةً يُعْطَى بِهَا فِي الدُّنْيَا وَيُجْزَى بِهَا فِي الأَخِرَةِ.  وَأَمَّا الْكَافِرُ فَيُطْعَمُ بِحَسَنَاتِ مَا عَمِلَ بِهَا لِلَّهِ فِي الدُّنْيَا حَتَّى إِذَا أَفْضَى إِلَى الأَخِرَةِ لَمْ يَكُنْ لَهُ حَسَنَةٌ يُجْزَى بِهَا)) مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hakika kafiri anapotenda ‘amali nzuri hulipwa mwonjo duniani. Ama Muumin, Allaah Humwekea mema yake Aakhirah na Anamlipa rizki duniani kwa utiifu wake)).

 

Na katika riwaayah: ((Hakika Allaah Hamdhulumu Muumin kwa mema yake, hupewa duniani [kheri zaidi] na hulipwa Aakhirah. Ama kafiri, huonjeshwa duniani kwa mema yake aliyoyatenda kwa ajili ya Allaah mpaka akifika Aakhirah hatakuwa na jema la kulipwa)). [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Tofauti kubwa baina ya malipo ya kafiri na Muumin, na Waumini daima ndio watakaofaulu kwa kulipwa mema zaidi.

 

 

2. Vipimo vya Allaah (سبحانه وتعالى) katika kulipa ‘amali kutokana na niyyah na ‘Aqiydah ya mtu.

 

 

3. Kafiri hulipwa mema yake duniani; ima kwa ziada ya mali yake au kukingwa na shari, lakini Aakhirah hana sehemu yoyote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 مَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الْآخِرَةِ نَزِدْ لَهُ فِي حَرْثِهِ ۖ وَمَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِن نَّصِيبٍ﴿٢٠﴾

Yeyote yule aliyekuwa anataka mavuno ya Aakhirah Tunamzidishia katika mavuno yake; na yeyote yule aliyekuwa anataka mavuno ya dunia, Tutampa humo, lakini Aakhirah hatokuwa na fungu lolote. [Ash-Shuwraa (42: 20)]

 

 [Rejea pia:  Al-Muuminuwn (23: 55-56)].

 

 

 4. Kafiri hata akitenda ‘amali nzuri zenye uzito mno, juhudi zake ni za bure hazina thamani mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

قُلْ هَلْ نُنَبِّئُكُم بِالْأَخْسَرِينَ أَعْمَالًا ﴿١٠٣﴾

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Je, Tukujulisheni wenye kukhasirika mno kwa ‘amali?”

 

الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا ﴿١٠٤﴾

Ni wale ambao wamepoteza juhudi zao katika uhai wa dunia, na huku wao wakidhani kwamba wanapata mazuri kwa matendo yao.

 

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ وَلِقَائِهِ فَحَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فَلَا نُقِيمُ لَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَزْنًا ﴿١٠٥﴾

Hao ni wale waliozikanusha Aayaat za Rabb wao na kukutana Naye basi zimeporomoka ‘amali zao; hivyo Hatutowasimamishia Siku ya Qiyaamah uzito wowote. 

 

ذَٰلِكَ جَزَاؤُهُمْ جَهَنَّمُ بِمَا كَفَرُوا وَاتَّخَذُوا آيَاتِي وَرُسُلِي هُزُوًا ﴿١٠٦﴾

Hivyo ndio jazaa yao Jahannam kwa yale waliyoyakufuru na kuchukulia mzaha Aayaat Zangu na Rusuli Wangu. [Al-Kahf (18: 103-106)]

 

[Rejea pia: Al-Israa (17: 18)].

 

 

5. Muumin juhudi zake zinathaminiwa na anapata faida ya kulipwa duniani na Aakhirah malipo mema zaidi. [Rejea: Al-Israa (17: 19-20)].

 

 

6. Allaah (سبحانه وتعالى) Hamdhulumu mja ‘amali yake hata ndogo vipi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا وَيُؤْتِ مِن لَّدُنْهُ أَجْرًا عَظِيمًا ﴿٤٠﴾

Hakika Allaah Hadhulumu hata uzito au chembe (au sisimizi). Na ikiwa ni ‘amali njema Huizidisha na Hutoa kutoka Kwake ujira adhimu.  [An-Nisaa (4: 40)]

 

[Rejea pia: Fusw-swilat (41: 46), Al-Zalzalah (99: 7), Yuwnus (10: 61), Al-Anbiyaa (21: 47)].

 

 

7. Allaah (سبحانه وتعالى) Anamlipa Muumin mara kumi zaidi kwa kitendo kimoja.

 

مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿١٦٠﴾

Atakayekuja kwa ‘amali njema basi atapata (thawabu) kumi mfano wa hiyo. Na Atakayekuja kwa ovu basi hatolipwa ila mfano wake, nao hawatodhulumiwa. [Al-An’aam (: 160)]

 

 

 

Share