057-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Dunia Ni Jela Kwa Muumin, Kafiri Kwake Ni Kama Jannah (Pepo)

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 57

Dunia Ni Jela Kwa Muumin, Kwa Kafiri Kwake Ni Kama Jannah (Pepo) 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((الدُّنْيَا سِجْنُ الْمُؤْمِنِ وَجَنَّةُ الْكَافِرِ)) مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Dunia ni jela ya Muumin, na ni Pepo Ya Kafiri)) [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Muumin ameharamishwa asivuke mipaka kwa ajili ya matamanio yasiyo ya halali ya kidunia, bali astarehe kwa mazuri aliyohalalishiwa, hivyo huwa kama yuko jela. Ama kafiri, yeye yuko huru kufanya lolote linalomshawishi katika matamanio yake kwa vile anapendelea zaidi maisha ya dunia.

 

 

[Al-A’raaf: 32, Huwd: 15-16, Ar-Ra’d: 26, An-Nahl: 107-109].

 

 

2. Muumin huko Jannah atakuwa huru kutembea atakako. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا سَلَامٌ عَلَيْكُمْ طِبْتُمْ فَادْخُلُوهَا خَالِدِينَ﴿٧٣﴾

Na wataendeshwa wale waliomcha Rabb wao kuelekea Jannah makundi-makundi, mpaka watakapoifikia na ikafunguliwa milango yake, na watasema walinzi wake: “Salaamun ‘Alaykum! Amani iwe juu yenu furahini na iingieni ni wenye kudumu.”

 

 

وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي صَدَقَنَا وَعْدَهُ وَأَوْرَثَنَا الْأَرْضَ نَتَبَوَّأُ مِنَ الْجَنَّةِ حَيْثُ نَشَاءُ ۖ فَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ﴿٧٤﴾

Watasema: “AlhamduliLLaahi, Himidi Anastahiki Allaah Ambaye Ametuhakikishia kweli ahadi Yake, na Ameturithisha ardhi tunakaa popote katika Jannah tutakapo”. Basi uzuri ulioje ujira wa watendao. [Az-Zumar: 73-74]

 

 Rejea pia: Al-Kahf (18: 107-108).

 

Ama kafiri, yeye atakuwa jela yaani motoni, na hatoweza kutoka wala kubadilisha hali yake ya adhabu.

 

Rejea: Ghaafir (40: 47-50), Az-Zukhruf 43: 74-78), Al-Muuminuwn (23: 103-108), Ash-Shuwraa (42: 44).

 

 

 3. Dunia ni jela kwa Muumin kulingana na Jannah ya neema za kudumu Aliyoahidi Allaah (سبحانه وتعالى).

 

وَأَمَّا الَّذِينَ سُعِدُوا فَفِي الْجَنَّةِ خَالِدِينَ فِيهَا مَا دَامَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ إِلَّا مَا شَاءَ رَبُّكَ ۖ عَطَاءً غَيْرَ مَجْذُوذٍ﴿١٠٨﴾

Na ama wale walio furahani, basi watakuwa katika Jannah, ni wenye kudumu humo zitakavyodumu mbingu na ardhi isipokuwa Atakavyo Rabb wako. Ni hiba isiyokatizwa. [Huwd (11: 108)]

 

Rejea pia: Aal-‘Imraan (3: 14-15), At-Tawbah (9: 20-22) (72), Az-Zukhruf (43: (33-35), Al-Bayyinah (98: 7-8).

 

Lakini dunia ni Jannah kwa kafiri kulingana na adhabu ya kudumu Aliyoahidi Allaah (سبحانه وتعالى) Aakhirah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

لَا يَغُرَّنَّكَ تَقَلُّبُ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي الْبِلَادِ ﴿١٩٦﴾

Isikudanganye kabisa kutangatanga kwa wale waliokufuru katika nchi.

 

مَتَاعٌ قَلِيلٌ ثُمَّ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۚ وَبِئْسَ الْمِهَادُ ﴿١٩٧﴾ 

Ni starehe ndogo, kisha makazi yao ni Jahannam. Na ni mahala pabaya mno pa kupumzikia. [Aal-‘Imraan (3196-197)]

 

 

Rejea pia: An-Nahl (16: 117), Luqmaan: (31:23-24).

 

 

4. Muumin anatakiwa asiwe mwenye mapenzi makubwa ya dunia na starehe zake, bali awe na shauku ya kupenda nyumba ya kudumu ya Aakhirah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَمَا أُوتِيتُم مِّن شَيْءٍ فَمَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَزِينَتُهَا ۚ وَمَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٦٠﴾

Na chochote mlichopewa katika vitu, basi ni starehe za uhai wa dunia na mapambo yake. Na yaliyoko kwa Allaah ni bora zaidi na yakubakia. Je, basi hamtii akilini? [Al-Qaswasw (28: 60)]

 

 

Rejea: Aal-‘Imraan (3: 14), Al-An’aam (6: 32), Al-Hadiyd (57: 20), Al-‘Ankabuwt (29: 64), Al-Kahf (18: 46), Ash-Shuwraa (42: 36), Ghaafir (40: 39), Az-Zukhruf (43: 33-35). 

 

 

Share