089-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Watu Waovu Kabisa Ni Wenye Nyuso Mbili Za Unafiki

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya  89

 

Watu Waovu Kabisa Ni Wenye Nyuso Mbili Za Unafiki

 

 

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَال: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  ((تَجِدُونَ النَّاسَ مَعَادِنَ، خِيَارُهُمْ فِي الْجَاهِلِيَّةِ خِيَارُهُمْ فِي الإِسْلامِ إِذَا فَقِهُوا، وَتَجِدُونَ خَيْرَ النَّاسِ فِي هَذَا الشَّأْنِ أَشَدَّهُمْ لَهُ كَرَاهِيَةً، وَتَجِدُونَ شَرَّ النَّاسِ ذَا الْوَجْهَيْنِ الَّذِي يَأْتِي هَؤُلاَءِ بِوَجْهٍ وَيَأْتِي هَؤُلاَءِ بِوَجْهٍ)) متفق عليه

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) ambaye amesema: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mtawakuta watu wana asili wanaonasibika nazo; wabora wao katika ujaahiliya ndio wabora wao katika Uislamu watakapofahamu Dini [hukmu za Shariy’ah]. Na mtamkuta mbora wa watu katika jambo hili [la uongozi] ni mwenye kulichukia mno, na mtamkuta muovu wa watu ni mwenye nyuso mbili, ambaye anawaendea hawa kwa uso huu, na anawaendea wale kwa uso mwingine)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Mwenye nyuso mbili ni miongoni mwa sifa za wanafiki, nao ni watu waovu kabisa kama mfano wa wanafiki wa zama za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ambao walikuwa wakificha unafiki wao lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Akawadhihirisha kwa kauli Zake kadhaa miongoni mwazo ni:

 

 

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّـهَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿١٤٢﴾

Hakika wanafiki (wanadhani) wanamhadaa Allaah, na hali Yeye (Allaah) Ndiye Mwenye kuwahadaa. Na wanaposimama kuswali husimama kwa uvivu, wakijionyesha kwa watu na wala hawamdhukuru Allaah isipokuwa kidogo tu.

 

 

مُّذَبْذَبِينَ بَيْنَ ذَٰلِكَ لَا إِلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ وَلَا إِلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ ۚ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَلَن تَجِدَ لَهُ سَبِيلًا ﴿١٤٣﴾

 

Madhabidhabina baina ya hayo (iymaan na kufru), huku hawako wala huko hawako. Na ambaye Allaah Amempotoa huwezi kumpatia njia (ya kumwongoa). [An-Nisaa (4: 142-143)].

 

Kisha Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ وَلَن تَجِدَ لَهُمْ نَصِيرًا ﴿١٤٥﴾

Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa katika moto; na wala hutompata kwa ajili yao mwenye kunusuru. [An-Nisaa (4: 145)].

 

 

 

2. Wenye nyuso mbili huwa na hulka ya kusema ya mdomoni yasiyokuweko moyoni. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu wanafiki wa zama za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

 

 وَلِيَعْلَمَ الَّذِينَ نَافَقُوا ۚ وَقِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا قَاتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَوِ ادْفَعُوا ۖ قَالُوا لَوْ نَعْلَمُ قِتَالًا لَّاتَّبَعْنَاكُمْ ۗ هُمْ لِلْكُفْرِ يَوْمَئِذٍ أَقْرَبُ مِنْهُمْ لِلْإِيمَانِ ۚ يَقُولُونَ بِأَفْوَاهِهِم مَّا لَيْسَ فِي قُلُوبِهِمْ ۗ وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا يَكْتُمُونَ ﴿١٦٧﴾

Na ili Adhihirishe wale waliofanya unafiki na wakaambiwa: “Njooni mpigane katika njia ya Allaah au (angalau) lindeni.” Wakasema: “Lau tungelijua kuwa kuna kupigana bila shaka tungelikufuateni.” Wao siku hiyo walikuwa karibu zaidi ya ukafiri kuliko iymaan. Wanasema kwa midomo yao, yale yasiyokuwemo katika nyoyo zao. Na Allaah Anajua zaidi wanayoyaficha. [Aal-‘Imraan (3: 167)]

 

Rejea pia: At-Tawbah (9: 8), Al-Fat-h (48: 11).

 

 

 

3. Mwenye sifa hiyo mbaya ya kuwa na nyuso mbili anafananishwa na kinyonga anayejibadilisha rangi kwa hali anayojipendelea nafsi yake. Ni hatari zaidi kuliko mtu muovu anayejulikana wazi. Na mtu kama huyu ni mwenye kusababisha ufisadi baina ya ndugu na jamii.

 

 

 

Rejea pia Hadiyth namba (21), (22), (88), (94) ambazo zimetaja matahadharisho ya maovu kama haya pamoja na mwongozo wa kuweka usalama baina ya ndugu katika jamii.  

 

 

 

4. Hapa tunafahamishwa ubora na umuhimu wa kufahamu mambo haswa ya Dini, kwani bila kufahamu tutapotea na kupoteza watu.

 

 

 

5. Walio bora katika nyakati za ujinga ni wale walioweza kufanya mambo mema na mazuri. Watu hao wanaposilimu ubora wao unaendelea, kwani Uislamu umehimiza sana kufanya mema. Waliotajwa hapa haswa ni Maswahaba na wale watakaokuja baada yao mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

 

 

6. Muislamu haifai kupigania uongozi, akichanguliwa na Waislamu ni vyema. Na hapo atakuwa ni mwenye kusaidiwa na Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

Share