Nimekaa Eda Ya Uwongo Kwa Kuogopa Maneno Ya Watu

 

SWALI:

Asalam alykum,  samahani kwakuwaandikia maswali mengi lakini M/mungu atawalipa kwa msaada wenu na kutuelimisha zaid sasa mimi nauliza kuna jamaa yangu alikua ameolewa na mtu mzima na yeye alikua mdogo bado kuliko mume wake kwa kweli alikua mzee tena sasa ikawa wamekaa siku nyingi hawajabahatika kupata mtoto sasa yule mume akamwambia mkewe mimi nataka nikuache halafu utafute mume akuowe upate watoto wakakubaliana na kweli akamuacha lakini yule mzee hana mtu huko wanakoishi wa hana mtoto wakuweza hata wakumfanyia chakula ikabidi yule aliekua mkewe akamwambia mimi sitaki nikae mbali na wewe kwa sababu tumekaa kwa vizuri hatujawahi kugombana na unajitahidi na mimi pamoja na wazee wangu kwa hio nitabaki humu humu kwenye nyumba ili nikusaidie, lakini hakutaka watu wajue kama kaachwa kwa ajili wasije wakamfikiria vibaya  sasa wamekaa mpaka ilifika siku M/mungu akachukua amana yake kwa yule mzee sasa kwa kweli watu wanao kuja kumuhani wanasema akae eda mpaka atakapo maliza eda yake na mwenyewe akawa  anafanya vile kwa jili vile vile watu wasijue sasa vipi hafanyi makosa yeye au kupata dhambi kwa ajili ya kua watu wasipate kumsema kwa vibaya naomba jibu haraka sana ili    nipate kumfahamisha mwenzangu.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

Shukran kwa suala lako zuri na haya ni makosa ambayo yanafanyika katika ndoa. Hatujui hiyo ndoa ilikuwa ni namna gani, lakini inatakiwa mas-ala ya ndoa watu wawe wameelimishwa vizuri wasije wakapatwa na matatizo baadaye. Je, msichana mdogo alipoolewa aliridhia mwenyewe au alilazimishwa na wazazi?

Lakini tukiacha hayo na tukaja katika swali lenyewe ni kuwa haijaingia akilini kwa mume mkongwe kumuacha mkewe mdogo ili apate kuolewa na mume mwingine kisha ikawa mke huyo aliyeachwa abakie kwa mtalaka wake mpaka afe. Kitu ambacho kinaingia katika mantiki ni kuwa msichana alikuwa arudi kwao kwani mahusiano yao yamekwisha baina yao baada ya talaka hiyo. Ilikuwa ni afadhali basi msichana huyo angevumilia katika ndoa mpaka Allah Aliyetukuka kuleta hukumu yake.

Haifai katika Uislamu kutofanya kitu kwa kuogopea watu kuzungumza. Hata ukiwa namna gani katika kujitahidi watu wataendelea kusema. Eda kawaida inakaliwa kwa moja ya sababu mbili ama kufiwa na mume au kuachwa. Sasa huyu mwanamke tayari alikuwa ameachwa na hivyo atakuwa tayari ameshakaa eda yake ya kuachwa. Haifai kwake yeye baada ya kumaliza eda hiyo na hakurudiwa tena na mumewe kukaa eda nyingine ni makosa. Kwa hiyo ikiwa ameanza kukaa, avunje eda yake kwa kuwa hana eda kabisa.

Hili kosa linaweza kumueka vibaya mbele ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa kuwaogopa watu badala ya Allah. Inavyotakiwa ni apatiwe nasiha ili arudi katika njia ya sawa na atubie kwa Mola wake Mlezi. Inatakiwa mtu afikie daraja ya Ihsani ambayo Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ni kumuabudu Allaah kama kwamba wamuona, kwani ikiwa humuoni basi Yeye Anakuona” (Muslim kutoka kwa ‘Umar ibn al-Khatwtwaab).  

Na tufahamu kuwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anajua na Anaona kila kitu. Tunatakiwa tumche Allah popote tulipo na tufuatilize jambo baya kwa jema litalifuta hilo baya, kama anavyosema Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Mche Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) popote pale ulipo na fuatisha kitendo kibaya kwa kitendo kizuri  kitafuta (kitendo kibaya) na ishi na watu kwa uzuri.” (at-Tirmidhiy kutoka kwa Jundub ibn Junaadah na Mu‘aadh ibn Jabal).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share