111-Lu-ulu-un-Manthuwrun : Wanaume Na Wanawake Wasio Maharimu Wasitazamane Uchi Wala Wasilale Pamoja

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 111

 

Wanaume Na Wanawake Wasio Maharimu Wasitazamane Uchi Wala Wasilale Pamoja

 

 

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((لاَ يَنْظُرُ الرَّجُلُ إِلَى عَوْرَةِ الرَّجُلِ، وَلاَ الْمَرْأَةُ إِلَى عَوْرَةِ الْمَرْأَةِ، ولاَ يُفْضِي الرَّجُلُ إِلَى الرَّجُلِ فِي ثَوْبٍ وَاحِدٍ، وَلاَ تُفْضِي الْمَرْأَةُ إِلَى الْمَرْأَةِ فِي الثَّوْبِ الْوَاحِدِ)) مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mwanamme asitazame uchi wa mwanamme, wala mwanamke asitazame uchi wa mwanamke, wala mwanamme asilale na mwanamme mwenzie katika nguo moja, wala mwanamke asilale na mwanamke mwenzie katika nguo moja)). [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Makatazo ya kutazamana uchi japokuwa ni kwa jinsi moja, seuze ikiwa ni baina ya mwanamme na mwanamke. Kwani hayo huenda yakapelekea katika maasi ya uliwati na usagaji.

 

Rejea An-Nuwr (24: 30, 31)]. 

 

 

2. Uislamu umehimiza kujisitiri na kusitiriana, na umefunga milango yote itakayopelekea kwenye zinaa na Allaah (سبحانه وتعالى) Akatahadharisha hilo Anaposema:

 

وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٣٢﴾

  Na wala msiikaribie zinaa. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya kabisa. [Al-Israa (17: 32)]

 

 

Na Allaah (سبحانه وتعالى) Amewaahidi Jannah ya Al-Firdaws wanaojisitiri sehemu zao za siri. Ametaja sifa hizo kadhaa zikiwemo: 

 

 وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾

Na ambao wanazihifadhi tupu zao.

 

إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٦﴾

Isipokuwa kwa wake zao, au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume basi hao hawalaumiwi. [Al-Muuminuwn: 5-6]

 

 

 

3. Haramisho la kutazama uchi wa mwanamume kutoka kitovuni hadi magotini.

 

 

4. Haramisho la kutazama uchi wa mwanamke. Na ambaye si mahram wake, ni mwili wote isipokuwa uso na viganja.

 

Rejea An-Nuwr (24: 31).

 

 

5. Zinaa huweza kuwa ni ya uhakika kujamiiana kwa haramu, au kutazama uchi wa mtu na machafu, au kwa kusikiliza yanayohusiana nayo kama ilivyothibiti katika  Hadiyth  kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)   kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Allaah Ameandika kila sehemu ya zinaa ambayo humuingiza mtu katika shauku. Hakutokuwa na kuikwepa. Zinaa ya macho ni kutazama, ya masikio ni kusikiliza, ulimi ni kunena maneno, mkono ni kuunyoosha, mguu ni hatua zake, na moyo hupata matamanio, na tupu husadikisha [hutenda] au hukadhibisha [huacha])). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

6. Makatazo kwa  wanawake kuvaa nguo zinazodhihirisha sehemu nyingi za mwili katika shughuli za furaha kama harusini n.k. kwa kisingizio kuwa wako na wanawake wenziwao. Wanavuka mipaka na hali mwanamke wa Kiislamu anatakiwa avae mavazi ya kumfunika vizuri abakie katika sitara na heshima na si kama mavazi ya wanawake makafiri. Itambulike kuwa sitara ya mwanamke katika mavazi mbele ya wanawake wenzao ni sawasawa na inavyopasa wanapokuwa mbele ya mahaarim zao kwamba wasionyeshe isipokuwa uso, nywele, shingo, mikono na miguu (kuanzia kifundoni na nyayo na si juu yake).

 

Rejea Hadiyth namba (114).

 

 

7. Jambo lolote linaloompelekea mtu katika maasiya, limekatazwa katika Uislamu.

 

 

Share