120-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Malaika Hawaingii Nyumba Yenye Mbwa Au Picha Za Viumbe

Lu-ulu-un-Manthuwrun:

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

 

Hadiyth Ya 120

 

Malaika Hawaingii Nyumba Yenye Mbwa Au Picha Za Viumbe

 

 

 

 

عَنْ أَبِي طَلْحَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((لاَ تَدْخُلُ الْملاَئِكَةُ بَيْتًا فِيهِ كَلْبٌ ولاَ صُورَةٌ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Twalhah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Malaika hawaingii nyumba ambayo yumo mbwa au picha [za viumbe vyenye roho])). [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

 Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Muislamu atahadhari kufuga mbwa bila ya sababu ya kufuga na kuweka picha, kwani kufanya hivyo anajikosesha kheri na baraka katika nyumba yake kwa kuwa Malaika hawatoingia.

 

 

2. Waislamu watahadhari kuzuia Malaika kutokuingia majumbani mwao kwa kuweka picha zenye viumbe, [Hadiyth: Imepokelewa kutoka kwa 'Aaishah (رضي الله عنها) amesema: "Nilifungua pazia la chumba cha hazina ambalo lilikuwa na picha (katika maelezo mengine: ambalo lilikuwa lina picha za farasi wenye mbawa). Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipoliona, alilichanilia mbali na uso wake ukabadilika kuwa mwekundu kisha akasema: ((Ee 'Aaishah, watu watakaopewa adhabu kali kabisa mbele ya Allaah siku ya Qiyaamah ni wale wanaoigiza maumbile ya Allaah)).

 

Kkatika riwaayah nyengine:

 

 ((Hakika wanaochora picha hizi wataadhibiwa na wataambiwa: Tieni uhai vile mlivyoviumba!))

 

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akaendelea kusema: ((Hakika Malaika hawaingii nyumba ambayo ina picha)). ‘Aaishah akasema: Tukalikata pazia na tukalitumia kufanyia mto au mito miwili. Nimemuona akiegemea mto mmojawapo uliokuwa na picha (zilizokatwa na kuharibiwa).

 

 

3. Malaika waliokusudiwa ni Malaika wa rahmah, kwani Malaika wengine kama wanaoandika matendo ya mwana Aadam, hao hakuna budi waweko kwa ajili ya kazi yao. Nao ni Malaika waliopewa sifa ya: raqiyb (mchungaji, shahidi) na: ‘atiyd (asiyekukosa kuweko), yu tayari kuandika, kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ﴿١٦﴾

Na kwa yakini Tumemuumba insani na Tunajua yale yanayowaza nafsi yake, na Sisi Tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo.

 

إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ﴿١٧﴾

Pale wanapopokea wapokeaji wawili (Malaika) wanaokaa kuliani na kushotoni. 

 

مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ﴿١٨﴾

Hatamki kauli yeyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha (kurekodi). [Qaaf: 16-18]

 

 

 

4. Picha zilokusudiwa ni za viumbe wa aina yoyote wenye roho. Pia chochote kilichochongwa kama vinyago vya watu, wanyama n.k.

 

 

 

5. Kufuga mbwa katika nyumba huwa ni kujikalifisha Muislamu na twahaara yake na mas-alah ya usafi kwa ujumla kama harufu mbaya, na kutosalimika vyombo, nguo, sehemu ya kuswalia na utwahara n.k.

 

 

6. Ni makosa katika jamii kwa wanaotundika picha zao ukumbini mwao wakiwa hawakuvaa mavazi ya hijaab. Mahali hapo huingia watu wasio mahaarim wa wanawake wa nyumba hiyo. Bali hata mtu akiwa na stara kamili, bado haijuzu kuweka picha kutokana na uharamu wake na pia kutoingia Malaika katika nyumba yenye picha.

 

 

7. Shariy’ah imekuja kuziba njia zote za kumpeleka mtu katika kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) katika uumbaji wake ambayo ni dhambi kubwa. Hivyo, Shariy’ah ikakataza kutundikwa picha zenye viumbe.

 

 

8. Shariy’ah imekuja kuondosha uzito na ugumu wa aina yoyote ile. Na kuweka mbwa ni njia moja inayompatia uzito mfugaji kwa kuiweka nyumba na yeye mwenyewe katika hali ya usafi na utwahaara.

 

 

 

Share