00-Umuhimu Wa Tawhiyd Na Fadhila Zake: Utangulizi

 

 

Umuhimu Na Fadhila Za Tawhiyd

 

00-Utangulizi:

 

 

بِسْمِ الله الرَّحْمنِ الرَّحِيم

الْحمْدُ لِلَّه وَالصَّلاةُ وَالسِّلامُ عَلى خَاتم الأنْبِيَاء وَالْمُرْسَلِين، الْمَبْعُوثُ رَحْمَةً لِلْعَالَمِين، مُحَمَّد وَعَلى آلِه وَأصْحابِه أجْمَعِين وَمَنْ تَبِعَهُمْ بِإِحْسَانٍ إِلَى يَوْمِ الدِّينِ.

Himdi Anastahiki Allaah, Swalaah na salaam zimfike Nabiy na Rasuli wa mwisho, aliyetumwa awe rahmah kwa walimwengu, Muhammad, pamoja na ahli zake na Maswahaba zake wote, na wanaowafuata kwa ihsaan mpaka Siku ya Malipo.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ

 Basi jua kwamba: laa ilaaha illa Allaah (hapana muabudiwa wa haki ila Allaah)  [Muhammad: 19]

 

 

Maana ya Tawhiyd kama alivyosema ‘Allaamah ‘Abdir-Rahmaan Naaswir As-Sa’dy katika Al-Qawlus-Sadiyd Fiy Maqaaswidit-Tawhiyd - Sharh Kitaab At-Tawhiyd: “Tambua kwamba maana ya Tawhiyd haina mipaka. Ni maarifa na kukiri kumpwekesha Ar-Rabb (Mola) kwa Sifa za ukamilifu, na kuthibitisha kwamba Anapwekeshwa katika Sifa Zake Adhimu na Tukufu, na kumpwekesha katika ‘ibaadah zote”.  

 

Kinyume cha Tawhiyd ni shirk ambayo ni kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika hayo yaliyotajwa yote yanayomuhusu Yeye Pekee.

 

‘Ulamaa wameigawanywa Tawhiyd katika sehemu tatu:

 

1-Tawhiyd Ar-Rubuwbiyyah

 

Nayo ni kumpwekesha Allaah katika Uumbaji, Uendeshaji wa mambo yote katika Ulimwengu, Utoaji rizki, Uletaji uhai na Ufishaji, kwa kuamini kwamba Yeye Ndiye Aliyeumba kila kitu, Anayeruzuku na kuendesha mambo yote ni Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Hana mshirika, na kuamini kwamba Ufalme wote ni wake. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قُلِ اللَّـهُ ۚ

Sema: “Ni nani Rabb wa mbingu na ardhi?” Sema: “Ni Allaah.” [Ar-Ra’d:16]

 

Na Anasema:

 

 قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ

Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini. Au nani anayemiliki kusikia na kuona; na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu, na anayemtoa mfu kutoka aliye uhai; na nani anayeendesha mambo (yote)?”  Watasema: “Ni Allaah”; basi sema: “Je basi hamuwi na taqwa?” [Yuwnus: 31]

 

 

2-Tawhiyd Al-Uluwhiyyah

 

Maana yake ni kumwepekesha Allaah katika 'ibaadah na kuzielekeza ‘ibaadah zote kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) bila ya kumshirikisha na chochote kama Anavyosema:

 

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾

Sema: “Hakika Swalaah yangu, na kuchinja kafara na ‘ibaadah zangu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu.”

 

لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ ﴿١٦٣﴾

 “Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza.”   [Al-An’aam: 162-163]

 

 

3-Tawhiyd Asmaa wasw-Swifaat

 

Kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa Sifa Zake Tukufu, na Majina Yake mazuri, bila kuzigeuza Sifa hizo maana zake, au kuzipinga, au kuzifananisha na viumbe au kuzipa unamna. Yeye Amejipa Majina mazuri mazuri na Sifa nzuri nzuri na Akawataka waja Wake wamuombe na kumtukuza kwa Majina na Sifa hizo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

 وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٨٠﴾

Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo. Na waacheni wale wanamili katika kukadhibisha Majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [Al-A’raaf: 180]

 

 

Qur-aan nzima imedhihirisha Tawhiyd ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa); mfano Suwratul-Faatihah ambayo tunaisoma kila siku mara kumi na saba katika Swalaah zetu za fardhi na pia katika Swalaah zote nyinginezo, imejumuisha aina tatu zote za Tawhiyd.

 

 بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴿١﴾

Kwa Jina la Allaah Ar-Rahmaan, Mwenye kurehemu.

 

 الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٢﴾

AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Rabb wa walimwengu.

 

الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴿٣﴾

Ar-Rahmaan, Mwenye kurehemu.

 

 مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ ﴿٤﴾

Mfalme wa siku ya malipo.

 

 إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ﴿٥﴾

Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.  [Al-Faatihah: 1-5]

 

Na pia kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 

 رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا فَاعْبُدْهُ وَاصْطَبِرْ لِعِبَادَتِهِ ۚ هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا ﴿٦٥﴾

 Rabb wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake; basi mwabudu Yeye tu na dumisha subira katika ‘ibaadah Yake. Je, unamjua yeyote anayefanana Naye (Allaah)?  [Maryam: 65]

 

 

 

 

Share