Ikiwa Hawaridhiani Katika Kitendo Cha Ndoa Wafanye Nini?

 

SWALI:

ENDAPO MWANAMKE ANASHINDWA KURIDHIKA KATIKA TENDO LA NDOA KWA SABABU YA MAUMBILE YAO; YAANI LABDA TUPU ZAO ZINA MATATIZO AMA MWANAUME; JE KUNA HALALI YA WAO KUISHI

 

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

Ikiwa mmoja wao ana matatizo, ama mume au mke inabidi wote wawili waende kwa daktari aliyebobea katika mas-ala hayo. Huenda ikawa ama mume au mke ana matatizo ya kutoweza kumtosheleza mwenziwe. Mara nyengine wote wawili au mmoja wao anaweza kutibiwa na kupona, hivyo kuwa sawa kabisa na hali yake kutulia. Mara nyengine hubidi upasuaji ili kuweza kurekebisha kasoro hiyo kati yao.

 

Ikiwa hali ya mmoja wao au wote wawili itarekebishika basi wataendelea kuishi kama mume na mke. Ikiwa tatizo hilo halikurekebishika basi zipo hali kadhaa ambazo zinaweza kujitokeza. Miongoni mwazo ni:

 

1. Wote wawili wana shida kwa sababu ya maumbile yao, hivyo kutoweza kutimiza mahitaji ya kimapenzi. Hapa itategemea, kwani kila mmoja anaweza kuridhika na hali hiyo bila kunung’unika. Katika uamuzi wao sheria haitawaingilia nao wanaweza kuishi pamoja bila ya shida yoyote.

 

2. Mmoja kati yao ndio mwenye tatizo, na hasa ikiwa ni mwanamume. Mume ambaye hawezi kumtosheleza mkewe kitandani ni sababu ya mke ama awe anatembea nje ili kujitosheleza kimwili. Lakini hili ni jambo ambalo limekatazwa na kupigwa vita na sheria. Hivyo, sheria ina kipengele cha kuwa mwanamke huyo anaweza kwenda kushitaki kwa Qadhi, na Qadhi ana uwezo wa kumuachisha na mumewe ili aweze akipata mume mwengine kuolewa na hivyo kuepukana na zinaa. Lakini ikiwa mke ataamua kukaa na mumewe kwa sababu ya kuwa tatizo hili likuja baadaye na kwa maslahi ya kuwatazama watoto, sheria haitamlazimisha kuachwa.

 

3. Mmoja kati yao ndio mwenye tatizo, na hasa ikiwa ni mwanamke. Kwa mwanamume itakuwa haina tatizo anaweza kukaa na mkewe hasa ikiwa wameishi kwa muda na wana watoto na tatizo limekuja baadaye. Na hapo mume atakuwa na thawabu kwa kumtazama mkewe katika hiyo. Mume huyo anaweza kuoa mke mwengine ili asitumbukie katika zinaa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share