08-Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake: Hukmu Ya Taarikus-Swalah (Asiyeswali)

Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

08- Hukmu Ya Taarikus-Swalaah (Asiyeswali)

 

Alhidaaya.com

 

 

‘Ulamaa wamekubaliana kuwa mwenye kuiacha Swalaah kusudi kwa jeuri na kwa kuikanusha, huyo anakuwa kafiri aliyekwisha toka katika Dini ya Kiislam.

 

Wakakhitalifiana juu ya yule mwenye kuiacha kwa uvivu tu au kwa kujishughulisha na dunia lakini haikanushi na anaamini kuwa ni fardhi juu yake. Wapo wanaosema hata huyu naye pia anakuwa kafiri aliyekwishatoka katika Dini ya Kiislam, na dalili walizoziegemea ni baadhi ya Hadiyth zifuatazo za Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عن جَابِر بن عبد الله عن النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهم عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قال: ((إِنَّ بَيْنَ الرَّجُلِ وَبَيْنَ الشِّرْكِ وَالْكُفْرِ تَرْكَ الصَّلَاةِ))   رواه مسلم  

Kutoka kwa Jaabir bin 'Abdillaah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Baina ya mtu na shirki, na kufru, ni kuacha Swalaah)) [Muslim]

 

 Na pia:

 

عَنْ بُرَيْدَةَ بن الحصيب  قال: سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول: ((إِنَّ الْعَهْدَ الَّذِي بَيْنَنَا وَبَيْنَهُمُ الصَّلاَةُ فَمَنْ تَرَكَهَا فَقَدْ كَفَرَ))  رواه أحمد وأبو داود والترمذي والنسائي وابن ماجه  

 

Kutoka kwa Buraydah bin Al-Haswiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu ambaye amesema: "Nimemsikia Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Ahadi (mafungamano) baina yetu na baina yao (wasio Waislam) ni Swalaah, atakayeiacha atakuwa amekufuru)) [Ahmad, Abu Daawuwd, An-Nasaaiy na Ibn Maajah]

 

 

Vile vile:

 

عن عَبْدِ اللَّهِ بْنِ شَقِيقٍ الْعُقَيْلِيِّ قال: " كَانَ أَصْحَابُ مُحَمَّدٍ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لَا يَرَوْنَ شَيْئًا مِنْ الْأَعْمَالِ تَرْكُهُ كُفْرٌ غَيْرَ الصَّلَاةِ"    رواه الترمذي (2622) وصححه الألباني في صحيح الترمذي

 

Kutoka kwa Abdillaah bin Shaqiyq ambaye amesema: “Maswahaba wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hawakuwa wakiona amali yoyote nyingine mtu akiiacha anakuwa kafiri isipokuwa Swalaah.” [At-Tirmidhiy na ameisahihisha Al-Albaaniy  katika Swahiyh At-Tirmidhiy (2622), Swahiyh At-Targhiyb (565)]

 

 

Anasema Ibn Hazm: “Imepokelewa kutoka kwa 'Umar bin Khatwtwaab na 'Abdur-Rahmaan bin 'Awf na Mu'aadh bin Jabal na Abuu Hurayrah na Maswahaba wengi (Radhwiya Allaahu 'anhum) kuwa: “Atakayeacha kuswali (Swalaah moja tu ya) fardhi kusudi (bila ya udhuru wowote) mpaka wakati wake (Swalaah hiyo) ukatoka, anakuwa kafiri.”

 

Hadiyth zifuatazo zinaelezea juu ya hukmu ya kuuliwa kwa Taarikus-Swalaah (Asiyeswali):

 

عن أُمِّ سَلَمَةَ  رضي الله عنها أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم قَالَ: ((سَتَكُونُ أُمَرَاءُ فَتَعْرِفُونَ وَتُنْكِرُونَ فَمَنْ عَرَفَ بَرِئَ وَمَنْ أَنْكَرَ سَلِمَ وَلَكِنْ مَنْ رَضِيَ وَتَابَعَ)) قَالُوا : أَفَلَا نُقَاتِلُهُمْ ؟ قَالَ: ((لَا مَا صَلَّوْا)) صحيح مسلم

Kutoka kwa Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu 'anha) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watakuweko viongozi kwenu watakaoamrisha mema na maovu. Atakayechukia hivi vitendo (viovu) hatakuwa na hatia. Atakayevipinga atakuwa salama, lakini (siye) atakayevikubali na kufuata)). Wakauliza: "Je tuwaue?" Akasema: ((Hapana madamu  wanaswali)) [Muslim]

 

 

 عن ابنِ عُمَرَ رضي الله عنهما أنَّ رسُوَل الله صلى الله عليه وسلم قال: ((أُمِرْتُ أَنْ أُقاتِلَ النَّاسَ حتَّى يَشْهَدُوا أنْ لا إلَهَ إلاَّ اللهُ وأنَّ محمداً رسوُل اللهِ، ويُقِيمُوا الصَّلاَةَ، ويُؤتُوا الزَّكاةَ، فإذا فَعَلوا ذَلِكَ عَصَموا منِّي دِماءَهُمْ وأمْوَالَهُمْ إلا بِحَقِّ الإِسْلامِ، وحِسابُهُم على اللهِ تعالى)) رَوَاهُ الْبُخَارِيُّ وَ مُسْلِمٌ   

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhuma) ambaye alisema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Nimeamrishwa nipigane vita na watu mpaka washuhudie kuwa hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na Muhammad ni Rasuli wa Allaah na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa Zakaah, na wakifanya hivyo, watakuwa wamepata himaya kwangu ya damu yao, na mali yao kwa haki ya Uislamu.  Na hesabu yao itakuwa kwa Allaah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kauli Za Baadhi Ya Wanavyuoni Kuhusu Taarikus-Swalaah:

 

 

Imaam An-Nawawy katika Sharh Muslim amesema:

 

“Anakatwa kichwa chake kwa upanga.”

 

Imaam Abu Haniyfah:

 

Anaona kuwa aliyertadi na akastahiki kuhukumiwa kuuliwa ni yule tu anayeikanusha ‘ibaadah hiyo ya Swalaah, lakini yule anayeacha kuswali kwa uvivu tu au kwa kujishughulisha na dunia, huyo si kafiri bali ni faasiq na hukmu yake ni kuhamishwa mbali na mji wake, wakiegemea dalili zinazobeba maana kwa ujumla kama vile kauli Yake Subhaanahu wa Ta’aalaa Anaposema:

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. [An-Nisaa: 116]

 

Na Hadiyth iliyosimuliwa na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((لكلِّ نبيٍّ دعوةٌ مستجابةٌ . فتعَجَّلَ كلُّ نبيٍّ دعوتَه . وإنِّي اخْتَبأْتُ دَعوتي شفاعةً لأُمَّتي يومَ القيامةِ . فهي نائلةٌ ، إن شاءَ اللهُ ، من مات من أُمَّتي لا يُشركُ باللهِ شيئًا)) ‏مسلم

 

((Kila Rasuli wa Allaah  ana du'aa yake inayokubaliwa. Kila Rasuli wa Allaah anafanya haraka kuiomba du'aa yake hiyo. Ama mimi nimeiweka du'aa yangu kwa ajili ya kuwaombea shafaa’ah ummati wangu siku ya Qiyaamah. Ataipata In Shaa Allaah kila aliyekufa na hali hajamshirikisha Allaah na chochote)) [Muslim]

 

Na Hadiyth nyingine za mfano huo.

 

 

Sayyid Saabiq:

 

"Kutokana na Ayaah pamoja na Hadiyth zilizotangulia, inatubainikia kuwa asiyeswali ni kafiri na kwamba damu yake ni halali. Hata hivyo baadhi ya ‘Ulamaa waliotangulia na wa siku hizi wakiwemo Imaam Abuu Haniyfah na Imaam Shaafi'y na Imaam Ahmad wanasema kuwa hawi kafiri moja kwa moja, bali anahesabiwa kuwa ni mtu faasiq (muovu) na anakamatwa na kutubishwa na akikataa kutubu basi ‘Ulamaa wote hao wanasema kuwa mtu huyo anahukumiwa kuuliwa.”

 

 

‘Ulamaa wengine wakasema kuwa hauliwi mtu kwa ajili ya kutoswali, na hawa wameegemeza hoja zao kutokana na Hadiyth:

  

عن ابْنِ مَسْعُودٍ رضي اللهُ عنه قالَ: قالَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم: ((لاَ يَحِلُّ دَمُ امْرِئٍ مُسْلِمٍ إلاّ بإحْدَى ثَلاَثٍ: الثَّيِّبُ الزَّاني، وَالنَّفْسُ بالنّفْسِ، وَالتَّارِكُ لِدِيِنِهِ الْمُفَارِقُ لِلْجَماعَةِ)).  رَوَاهُ الْبُخَارِيّ وَمُسْلِمٌ    

Kutoka kwa Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allahu 'anhu) ambaye alisema: Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Damu ya Muislamu haiwezi kwa haki kumwagwa isipokuwa katika hali tatu:  Mzinzi aliyeoaolewa, uhai kwa uhai, na kwa yule anayeacha Dini na akajifarikisha na  jamaa’ah (amejitenga na watu wa Dini yake))  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Wanasema kuwa hapa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakumtaja asiyeswali kuwa ni miongoni wa waliohalalishwa damu yao.

 

Imaam Ash-Shawkaaniy amesema: 

 

"Kwa hakika asiyeswali ni kafiri, kwa sababu Hadiyth zote zilizopokelewa katika maudhui haya zinamwita hivyo (kuwa ni kafiri), na mpaka uliowekwa baina ya mtu anayestahiki kuitwa kafiri na yule asiyestahiki kuitwa kafiri ni Swalaah."

 

Kwa hiyo waliohukumiwa kuwa ni makafiri kwa sababu ya kutokuswali wanapofariki huwa haipasi kuoshwa, wala kukafiniwa wala haswaliwi wala hazikwi katika makaburi ya Waislamu wala watu wake hawamrithi bali mali yake inapelekwa Baytul-Maal ya Waislamu.

 

Ama ‘Ulamaa wengi rai  zao ni kwamba: Ikiwa Muislamu anakanusha Swalaah kwamba sio fardhi kwake, basi yeye ni kafiri na anatoka katika Uislamu, na hukmu yake ni kama iliyotajwa hapo juu hukumu ya kafiri. Ama ikiwa hakanushi Swalaah bali ni kudharau kwake, au uvivu basi atahesabika ni mtenda dhambi kubwa, lakini hatoki katika Uislamu. Anatakiwa kupewa siku tatu atubu. Atakapotubu ni kheri yake, na asipotubu anatakiwa kuuawa na hii inakuwa ni adhabu yake sio kwa sababu ya kuwa kafiri bali kwa kukataa kuswali. Hivyo huoshwa na kukafiniwa, na kuswaliwa na Waislamu na kuombewa maghfirah na kuzikwa katika makaburi ya Waislamu na pia anaweza kurithiwa. Kwa ujumla hukmu zote zinazomhusu Muislamu anayetenda madhambi zinakuwa sawa na yake anapokuwa hai na anapofariki.  [Fataawa Al-Lajnah Ad-Daaimah (6/49)]  

 

 

Share