06-Sifa Kumi Na Fadhila Zake: Wanyenyekevu Wanaume Na Wanawake

 

Sifa Kumi Na Fadhila Zake

 

06 - Wanyenyekevu Wanaume Na Wanawake  

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ وَالصَّابِرِينَ وَالصَّابِرَاتِ وَالْخَاشِعِينَ وَالْخَاشِعَاتِ

Hakika Waislamu wanaume na wanawake, na Waumini wanaume na wanawake, na watiifu wanaume na wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanaosubiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake [Al-Ahzaab: 35]

 

 

Khushuw' ina maana nyingi, miongoni mwazo ni:

 

Utulivu, ushwari, udhalili kama Anvosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَخَشَعَتِ الْأَصْوَاتُ لِلرَّحْمَـٰنِ

na sauti zitafifia kwa Ar-Rahmaan [Twaahaa: 108] 

 

 

Pia khushuw’ ina maana ni khofu kwa dalili Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pindi alipowauliza Maswahaba:

 

((أَيُّكُمْ يُحِبُّ أَنْ يُعْرِضَ اللَّهُ عَنْهُ))‏ قَالَ:  فَخَشَعْنَا

((Nani miongoni mwenu anayependa Allaah Amgeuzie Uso Wake?)) akasema: “Tukakhofu.” [Muslim]

 

Na pia ni ulaini na kutahadhari, kuogopa; mfano pindi mtu anaposikia kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) nyoyo zikaingia khofu na unyenyekevu.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

أَلَمْ يَأْنِ لِلَّذِينَ آمَنُوا أَن تَخْشَعَ قُلُوبُهُمْ لِذِكْرِ اللَّـهِ وَمَا نَزَلَ مِنَ الْحَقِّ وَلَا يَكُونُوا كَالَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلُ فَطَالَ عَلَيْهِمُ الْأَمَدُ فَقَسَتْ قُلُوبُهُمْ ۖ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ فَاسِقُونَ ﴿١٦﴾

Je, haujafika wakati kwa walioamini kwamba zinyenyekee nyoyo zao kwa kumdhukuru Allaah na yale yaliyoteremka ya haki, na wala wasiwe kama wale waliopewa Kitabu kabla, ukawatawilikia muda, kisha zikawa ngumu nyoyo zao? Na wengi miongoni mwao ni mafasiki.  [Al-Hadiyd: 16]

 

 

Na khushu’w mahali pake ni moyoni kisha inaathiri viungo vinginevyo:   Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ﴿٢﴾

Hakika Waumini ni wale ambao Anapotajwa Allaah, nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayaat Zake huwazidishia iymaan, na kwa Rabb wao wanatawakali. [Al-Anfaa; 2]

 

 

Kinyume chake ni ugumu; yaani nyoyo kuwa ngumu na kutokuwa na khofu mtu anaposikia kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Aayah ya juu hapo ya Suwrah Al-Hadiyd ilivyomalizik:

 

وَلَا يَكُونُوا كَالَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلُ فَطَالَ عَلَيْهِمُ الْأَمَدُ فَقَسَتْ قُلُوبُهُمْ ۖ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ فَاسِقُونَ ﴿١٦﴾

wala wasiwe kama wale waliopewa Kitabu kabla, ukawatawilikia muda, kisha zikawa ngumu nyoyo zao? Na wengi miongoni mwao ni mafasiki.  [Al-Hadiyd: 16]

 

 

Na pia kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

اللَّـهُ نَزَّلَ أَحْسَنَ الْحَدِيثِ كِتَابًا مُّتَشَابِهًا مَّثَانِيَ تَقْشَعِرُّ مِنْهُ جُلُودُ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ ثُمَّ تَلِينُ جُلُودُهُمْ وَقُلُوبُهُمْ إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ هُدَى اللَّـهِ يَهْدِي بِهِ مَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ ﴿٢٣﴾

Allaah Ameteremsha kauli nzuri kabisa, Kitabu; zinazoshabihiana ibara zake, zenye kukaririwa kila mara, zinasisimua kwazo ngozi za wale wanaomkhofu Rabb wao, kisha zinalainisha ngozi zao na nyoyo zao katika kumdhukuru Allaah. Huo ndio mwongozo wa Allaah Humwongoza kwao Amtakaye. Na ambaye Allaah Amempotoa basi hana wa kumuongoa. [Az-Zumar: 23]

 

 

Khushuw’ pia ina maana kuzungumza kwa utaratibu kwa uangalifu, hadhi, raghba, khofu na unyenyekevu kama hali za Manabii. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَوَهَبْنَا لَهُ يَحْيَىٰ وَأَصْلَحْنَا لَهُ زَوْجَهُ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ ﴿٩٠﴾

Basi Tukamuitikia na Tukamtunukia Yahyaa, na Tukamtengenezea mke wake. Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya kheri na wakituomba kwa raghba na khofu, na walikuwa wenye kutunyenyekea. [Al-Anbiyaa: 90]

 

 

Linalomtia mtu hamasa kuwa katika hali hiyo ni khofu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na utambuzi kuwa Allaah ('Azza wa Jalla) Anaona yote tunayoyatenda kama ilivyothibiti katika Hadiyth ndefu alipokuja Jibriyl ('Alayhis-salaam) kwa Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumuuliza maswali kadhaa:   

 

((...أنْ تَعْبُدَ الله كَأَنَّكَ تَرَاهُ فإنْ لَمْ تَكُنْ تَرَاهُ فإنَّهُ يَرَاك))

((….. na umuabudu Allah kama kwamba unamuona, na kama humuoni basi Yeye Anakuona))  

 

Khushuw' katika Swalaah:

 

Khushuu (unyenyekevu) ni jambo gumu na kubwa hakika hasa katika Swalaah kwani shaytwaan ndipo mahali anapopenda sana kumharibia mtu ‘amali yake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ ﴿٤٥﴾

Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalaah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu. [Al-Baqarah: 45]

 

 

Kwa hiyo kunahitajika du’aa na kinga ya kumwepuka shaytwaan katika Swalaah jambo ambalo pindi mja akiswali kwa khushuw’, atapata fadhila zake zikiwemo kupata Jannah ya Al-Firdaws kwa kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):  

 

 بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴿١﴾

 

 

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾

Kwa yakini wamefaulu Waumini.

 

الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾

Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea. [Al-Muuminuwn: 1]

 

Aayah zinaendelea mpaka kauli Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾

Hao ndio warithi.

 

الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾

Ambao watarithi (Jannah) ya Al-Firdaws, wao humo ni wenye kudumu.  [Al-Muuminuun: 10-11]

 

Vipi kupata khushuw’ katika Swalaah:

 

 

1-Kwenda msalani kukidhi haja kubwa na ndogo kabla ya Swalaah.

 

 

2-Kula kama una njaa kabla ya kuswali

 

 

3-Kutia vizuri wudhuu.  

 

 

4-Kuweka Sutrah (Kizuizi) mbele yako.

 

 

5-Kutokuvaa nguo za rangi au zenye maneno hasa kama unaswali Jamaa  ili isiwashughulishe wengineo. 

 

 

6-Kukumbuka mauti.  

 

 

7-Kwa wanawake wanaoswali nyumbani, kutokuswali mbele ya watu   wanaozungumza, watoto na kutokuweko sauti za televisheni, radio n.k.

 

 

8-Kuanza kwa du’aa za kufungulia Swalaah na kujikinga na shatywaan kama ilivyothibiti katika Sunnah.

 

 أَعـوذُ بِاللهِ مِنَ الشَّـيْطانِ مِنْ نَفْخِـهِ وَنَفْـثِهِ وَهَمْـزِه

 

 Najikinga na Allaah kutokana na shaytwaan, na kibri yake, na kupulizia kwake na kutia kwake wasiwasi (katika nyoyo za binaadamu) [Hadiyth ya Jubayr bin Mutw-‘im (رضي الله عنه) - Abu Daawuwd (1/203), Ibn Maajah (1/265), Ahmad (4/85), na Muslim kutoka kwa ibn ‘Umar (رضي الله عنهما) kama hivyo na mna kisa humo (1/420)]

 

 

9-Kujikinga na shaytwaan ndani ya Swalaah anapokupotezea khushuw’, nayo ni kutema mate kidogo kama kupuliza upande wa bega la kushoto mara tatu na kuomba kinga.  

 

 

10-Kuweka mkono wa kulia juu ya kushoto kwenye kifua vizuri.

 

 

11-Kutambua kwamba upo mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na unaposoma Al-Faatihah Anakujibu.

 

 

12-Kutazama sehemu ya kusujudu unaposimama.

 

 

13-Kuzingatia Quraan unapoisoma.

 

 

14-Kusoma Qur-aan kwa sauti nzuri katika katika Swalaah za jahriyyah (kisoma cha sauti).

 

 

15-Kunong'ona kwenye Swalaah za Sirriyah (Swalah za kimya) bila ya kutoa sauti sana au bila ya kuswali kimya sana.

 

 

16-Kuswali kwa twumaaninah: ni utulivu na kwa vituo na kutimiza kila kitendo bila ya kuharakisha kwa kupumzika kiasi hadi uhakikishe kila sehemu ya kiungo kimetulia mahala pake wakati wa kurukuu, kusimama baada rukuu, kusujudu, baina ya sijda mbili, ukitoka kusujudu kabla hujanyanyuka n.k.1-    

 

 

 

Share