08-Sifa Kumi Na Fadhila Zake: Wafungao Swawm Wanaume Na Wanawake

 

Sifa Kumi Na Fadhila Zake

 

08-Wafungao Swawm Wanaume Na Wanawake

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 

إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ وَالصَّابِرِينَ وَالصَّابِرَاتِ وَالْخَاشِعِينَ وَالْخَاشِعَاتِ وَالْمُتَصَدِّقِينَ وَالْمُتَصَدِّقَاتِ وَالصَّائِمِينَ وَالصَّائِمَاتِ

 

Hakika Waislamu wanaume na wanawake, na Waumini wanaume na wanawake, na watiifu wanaume na wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanaosubiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao swadaqah wanaume na wanawake, na wafungao Swawm wanaume na wanawake [Al-Ahzaab: 35]

 

 

Maana Ya Swawm Kilugha:

 

 

Swawm ni kufunga na kujizuilia. Huenda ikawa ni kujizua kula chakula, kinywaji au kitu chochote kingine hata kujizua kuongea kwa dalili ya kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alipomuamrisha Maryam mama yake Nabiy ‘Iysaa ‘('Alayhis-Salaam) afanye baada ya kumzaa mwanawe:

 

 

فَكُلِي وَاشْرَبِي وَقَرِّي عَيْنًا ۖ فَإِمَّا تَرَيِنَّ مِنَ الْبَشَرِ أَحَدًا فَقُولِي إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَـٰنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنسِيًّا ﴿٢٦﴾

 “Basi kula na kunywa na litue jicho lako. Na utakapokutana na mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri ya swawm kwa Ar-Rahmaan hivyo leo sitomsemesha mtu yeyote.”   [Maryam: 26]  

 

 

Maana ya Swawm ki-Shariy’ah:

 

 

Ni kuacha kula na kunywa pamoja na matamanio ya mwili na tumbo kuanzia kupambazuka kwa Alfajiri hadi linapozama jua yaani wakati wa Magharibi pamoja na niyyah ya kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

  

Hukmu ya Swawm ilikwishawatangulia walio kabla yetu kwa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa): 

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٨٣﴾

Enyi walioamini! Mmefaridhishwa Swiyaam kama ilivyofaridhishwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Al-Baqarah: 183]

 

 

Swawm ni aina mbili:

 

 

Swawm ya wajib: Ni Swawm ya mwezi wa Ramadhwaan, Swawm ya kafara, fidia na Swawm ya kuondosha nadhiri.

 

Swawm za Sunnah: Ni kama Swawm ya siku ya ‘Arafah, Swawm ya ‘Ashuraa, Jumatatu na Alkhamiys, Ayaamul-Biydhw (siku tatu katika mwezi wa Hijri 13, 14 na 15), na pia Swawm nyinginezo kama katika mwezi wa Muharram n.k.

 

Kuna aina mbili za watu wanaofunga:

 

a) Wanaofunga kwa kujizuia kula, kunywa na matamanio ya mwili, lakini hawazuii ndimi zao, wala macho na masikio yao, wala viungo vyao vinginevyo  kuzuia yale yaliyoharamishwa. Pia aina ya wafungaji wenye kupoteza muda wao katika upuuzi bila ya kutekeleza ‘ibaadah zipasazo kutekelezwa mtu anapokuwa katika Swawm.

 

 

b) Wanaofunga kwa kutekeleza ipasavyo swawm zao kwa ‘ibaadah na kutenda mema kwa wingi na kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa wingi.   Ni wenye taqwa na iymaan ya kutaraji malipo ya Swawm zao na ni wenye kuthamini fadhila za Swawm. 

 

 

Swawm ni ‘ibaadah tukufu kabisa na fadhila zake ni nyingi sana, chache miongoni mwazo ni:

 

 

Fadhila Za Swawm Kwa Ujumla Na Swawm Za Ramadhwan:

 

1. Swawm ni ‘Ibaadah mahsusi ya Allaah ('Azza wa Jalla):

 

 

عن أبي هريرة  رضي الله عنه  قال: قال رسول اللَّه  صلى الله عليه وسلم: (( قالَ اللَّهُ:  كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ لَهُ إِلاَّ الصِّيَامَ، فَإِنَّهُ لِي، وَأَنَا أَجْزِي بِهِ‏.‏ وَالصِّيَامُ جُنَّةٌ، وَإِذَا كَانَ يَوْمُ صَوْمِ أَحَدِكُمْ، فَلاَ يَرْفُثْ وَلاَ يَصْخَبْ، فَإِنْ سَابَّهُ أَحَدٌ، أَوْ قَاتَلَهُ فَلْيَقُلْ إِنِّي امْرُؤٌ صَائِمٌ‏.‏ وَالَّذِي نَفْسُ مُحَمَّدٍ بِيَدِهِ لَخُلُوفُ فَمِ الصَّائِمِ أَطْيَبُ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ رِيحِ الْمِسْكِ، لِلصَّائِمِ فَرْحَتَانِ يَفْرَحُهُمَا إِذَا أَفْطَرَ فَرِحَ، وَإِذَا لَقِيَ رَبَّهُ فَرِحَ بِصَوْمِهِ ‏)) رواه البخاري.

 

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema:

((Allaah ‘Azza wa Jalla Amesema: “Kila ‘amali ya bin Aadam inamhusu yeye isipokuwa Swiyaam, kwani hakika hiyo inanihusu Mimi, Nami Ndiye Ninayeilipia.  Na Swawm ni ngao, na itakapokuwa siku ya Swawm ya mmoja wenu, basi asitamke maneno yasiyolaiki, wala asifanye maasia, wala asipayuke ovyo. Ikiwa mtu atamvuta watukanane au wapigane, basi aseme: “Hakika mimi nimefunga”. Naapa kwa Ambaye Nafsi ya Muhammad iko Mkononi Mwake, hakika kutaghayari harufu ya kinywa cha mwenye Swawm kunanukia mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski. Mwenye Swawm ana furaha mbili anazozifurahikia; anapofungua hufurahika kwa Swawm yake, na atakapokutana na Mola wake atafurahi kwa Swawm yake)) [Al-Bukhaariy]

 

 

 

2.  Mwenye Swawm anaghufuriwa madhambi yake:

 

قال صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ صَامَ رَمَضَانَ إِيمَانًا وَاحْتِسَابًا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ))   أخرجه البخاري ومسلم

Amesema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Atakayefunga Ramadhwaan kwa iymaan na kutaraji malipo ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

3- Swawm ni ngao

 

عن عثمان بن عفان رضي الله عنه، قال: سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول:  الصِّيامُ جُنَّةٌ من النَّارِ ، كَجُنَّةِ أحدِكمْ من القِتالِ))

Imepokelewa toka kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu 'anhu)  akisema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Swiyaam ni ngao dhidi ya moto, kama ngao ya mmoja wenu katika mapigano)) [Ibn Maajah, amiesahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Ibn Maajah (1336),  Swahiyh Al-Jaami’  (3879)]

 

 

 

4. Kufunga (Swawm) ni kuepushwa na moto masafa ya miaka sabini.

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رضي الله عنه قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: مَنْ صَامَ يَوْماً فِي سَبِيلِ اللَّهِ بَعَّدَ اللَّهُ وَجْهَهُ عَنْ النَّارِ سَبْعِينَ خَرِيفًا .

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayefunga  Swawm siku moja kwa ajili ya Allaah, Allaah Atamweka mbali uso wake na moto masafa ya miaka sabini)) [Muslim 2/208]

 

Na katika Hadiyth nyingine pia:

 

عن جابر رضِي الله عنه عن النبيِّ  صلى الله عليه وسلم  قال: ((الصِّيام جُنَّة يَستَجِنُّ بها العبدُ من النار))   

Imepokelewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swiyaam ni kinga itamuokoa mja kutokana na moto [wa Siku ya Qiyaamah])) [Ahmad 2/402, Swahiyh At-Targhiyb 1/411 na Swahiyh Al-Jaami’ 3880]

 

 

5. Mwenye kufunga (Swawm) atafunguliwa mlango wa Rayyaan huko Jannah.

 

عَنْ سَهْلٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِنَّ فِي الْجَنَّةِ بَابًا يُقَالُ لَهُ الرَّيَّانُ يَدْخُلُ مِنْهُ الصَّائِمُونَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ لَا يَدْخُلُ مِنْهُ أَحَدٌ غَيْرُهُمْ يُقَالُ أَيْنَ الصَّائِمُونَ فَيَقُومُونَ لَا يَدْخُلُ مِنْهُ أَحَدٌ غَيْرُهُمْ فَإِذَا دَخَلُوا أُغْلِقَ فَلَمْ يَدْخُلْ مِنْهُ أَحَدٌ ))

Imepokelewa kutoka kwa Sahl (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika katika Jannah kuna mlango unaitwa Rayyaan, wataingia humo siku ya Qiyaamah wenye kufunga (Swawm), hatoingia yeyote mwingine. Itasemwa: “Wako wapi waliokuwa wakifunga? Watasimama kuingia hatoingia yeyote mwengine, watakapoingia, utafungwa, basi hatoingia mwengine)) [Al-Bukhaariy 1763, Muslim 1947]

 

 

6. Swawm ni kwa ajili ya Allaah Pekee na mwenye Swawm hupata furaha mbili; anapofuturu na atakapokutana na Rabb Wake. Na harufu ya mdomo wake ni nzuri mbele ya Allaah kuliko harufu ya misk.

 

 

عنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ يُضَاعَفُ الْحَسَنَةُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا إِلَى سَبْعمِائَة ضِعْفٍ قَالَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ إِلَّا الصَّوْمَ فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ يَدَعُ شَهْوَتَهُ وَطَعَامَهُ مِنْ أَجْلِي لِلصَّائِمِ فَرْحَتَانِ فَرْحَةٌ عِنْدَ فِطْرِهِ وَفَرْحَةٌ عِنْدَ لِقَاءِ رَبِّهِ وَلَخُلُوفُ فِيهِ أَطْيَبُ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ رِيحِ الْمِسْكِ))

Imepokewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu): ((Kila 'amali njema ya mwana Aadam inalipwa mara kumi na inaongezewa thawabu kutoka kumi hadi mia saba, na Allaah (‘Azza wa Jalla) Anasema: Isipokuwa Swawm, kwani hiyo ni kwa ajili Yangu na Mimi Ndiye Nitakayemlipa; ameacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili Yangu. Kwa anayefunga atapata furaha mbili; furaha anapofuturu na furaha atakapoonana na Rabb wake, harufu inayotoka kinywani mwa aliye na Swawm ni nzuri mbele ya Allaah kuliko harufu ya misk)) [Muslim na Ahmad]

 

 

7. Du’aa ya mwenye Swawm inakubaliwa.

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((ثَلاَثَةٌ لاَ تُرَدُّ دَعْوَتُهُمْ,  الإِمَامُ الْعَادِلُ, وَالصَّائِمُ حَتَّى يُفْطِرَ, وَدَعْوَةُ الْمَظْلُومِ ...))

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (([Watu] Watatu hazirudishwi du'aa zao; Imaam muadilifu, mwenye Swawm mpaka afuturu, na du'aa ya aliyedhulumiwa…)) [Ahmad na Ibn Maajah. Pia Al-Bayhaqiy 3/345 na As-Silsilah Asw-Swahiyhah 1797]

 

 

8. Swawm itakuombea Shafaa-‘ah Siku ya Qiyaamah.

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو رضي الله عنهما أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((الصِّيَامُ وَالْقُرْآنُ يَشْفَعَانِ لِلْعَبْدِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، يَقُولُ الصِّيَامُ:  أَيْ رَبِّ مَنَعْتُهُ الطَّعَامَ وَالشَّهَوَاتِ بِالنَّهَارِ فَشَفِّعْنِي فِيهِ.  وَيَقُولُ الْقُرْآنُ: مَنَعْتُهُ النَّوْمَ بِاللَّيْلِ فَشَفِّعْنِي فِيهِ.  قَالَ : فَيُشَفَّعَانِ))

Imepokelewa kutoka  kwa 'Abdullaah bin ‘Amr  (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa)  kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swiyaam na Qur-aan zitamuombea shafaa’ah mja siku ya Qiyaamah. Swiyaam itasema: “Ee ee Rabb!  Nimemzuia chakula chake na matamanio wakati wa mchana, basi nnamuombea shafaa-‘ah.” Na Qur-aan itasema: “Nimemzuia usingizi wake wakati wa usiku basi nnamuombea shafaa-‘ah.” Akasema: ((Basi [viwili hivyo] vinaombea shafaa-‘ah na kukubaliwa]. [Ahmad (174/2) Al-Haakim (1/554), Al-Bayhaqiy (3/181) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaamiy’ 7329]

 

 

9. Swawm hakuna mfano wake.

 

عَنْ أَبِي أُمَامَةَ  قَالَ: أَتَيْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، فَقُلْتُ: مُرْنِي بِأَمْرٍ آخُذُهُ عَنْكَ قَالَ: ((عَلَيْكَ بِالصَّوْمِ فَإِنَّهُ لَا مِثْلَ لَهُ))  

Kutoka kwa Abuu Umaamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Nilimwendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nikasema: “Niamrishe jambo [litakalonifaa Aakhirah] nilichukue kwako.” Akasema: ((Shikilia Swawm kwani hakika hakuna mfano wake)) [An-Nasaaiy]

 

 

10. Ukifariki ukiwa katika Swawm utaingia Jannah nayo ni Husnul-Khaatimah.

 

عن حذيفة  رضي الله عنه أن النبي صلى الله عليه وسلم قَال: ((مَن خُتِمَ له بصيام يومٍ دخل الجنة))

Imepokelewa kutoka kwa Hudhayfah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayekuwa 'amali yake ya mwisho kabla ya kufariki ni Swiyaam ataingia Jannah)) [Ahmad 5/391. Swahiyh At-Targhiyb 1/412, Swahiyh Al-Jaami’ 6224]

 

 

 

11. Swawm hufuta madhambi yatokanayo na mtu kufitinika na mkewe na mali yake:

 

سأل عمر رضي الله عنه قال: من يحفظ حديثًا عن النبي صلى الله عليه وسلم في الفتنة؟  قال حذيفة: أنا سمعته يقول: ((فِتْنَةُ الرَّجُلِ فِي أَهْلِهِ وَمَالِهِ وَجَارِهِ تُكَفِّرُهَا الصَّلَاةُ وَالصِّيَامُ وَالصَّدَقَةُ)).

‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu)  aliuliza: “Nani anahifadhi Hadiyth toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu fitnah?” Hudhayfah akasema: Mimi nimemsikia akisema: ((Kufitinika mtu kutokana na mke wake, mali yake na jirani yake, (dhambi yake) hufutwa na Swalaah na Swawm na swadaqah..)) [Al-Bukhaariy]

 

 

12. Fadhila Za Swawm Jumatatu Na Alkhamiys:

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه: تُعرَضُ الأعمالُ يومَ الاثنينِ والخميسِ فأحبُّ أن يُعرَضَ عملي وأنا صائمٌ

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Amali zinapandishwa siku ya Jumatatu na Alkhamiys, basi napenda kwamba zipandishwe 'amali zangu nikiwa mimi nina Swawm.” [Swahiyh At-Tirmidhiy 747, Swahiyh At-Targhiyb 1041]

 

Na kuhusu Swiyaam ya Jumatatu:

 

عَنْ أَبِي قَتَادَةَ الْأَنْصَارِيِّ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ سُئِلَ عَنْ صَوْمِ الِاثْنَيْنِ فَقَالَ: ((فِيهِ وُلِدْتُ وَفِيهِ أُنْزِلَ عَلَيَّ)).

Kutoka kwa Abuu Qataadah Al-Answaariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu Swawm ya Jumatatu akasema: “Nimezaliwa siku hiyo na siku hiyo nimeteremshiwa (Qur-aan).” [Muslim]

 

 

13-Fadhila Za Swiyaam Ayyaam Al-Biydhw:

 

 

عَنْ أَبي ذَرٍّ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيهِ وَسَلَّمَ (مَنْ صَامَ مِنْ كُلِّ شَهْرٍ ثَلاثَةَ أَيَّامٍ فَذَلِكَ صِيَامُ الدَّهْرِ)) فَأَنْزَلَ اللهُ تُصْدِيقَ ذَلِكَ في كِتَابِهِ الْكَرِيمِ: ((مَنْ جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا))، الْيَوْمُ بِعَشَرَةِ أَيّامٍ. أخرجه أحمد والترمذي وقال حديث حسن ، والنسائي وابن ماجه وابن خزيمة

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Dharr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote atakayefunga (Swawm) kila mwezi siku tatu, ni sawa na Swawm ya milele)) Kisha Allaah Akateremsha Aayah ithibitishayo hayo: “Atakayekuja kwa ‘amali nzuri basi atapata (thawabu) kumi mfano wa hiyo.” Siku moja kwa malipo ya siku kumi. [Imepokewa na At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan, An Nasaaiy na Ibn Maajah, Ibn Khuzaymah na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Al-Irwaa (4/102)]. Aayah: Suwrat Al-An’aam (160)]

 

Maana Ya Al-Biydhw:  Masiku hayo yameitwa ‘Al-Biydhw’ (meupe) sababu usiku wa siku hizo hung’aa kutokana na mwanga wa mwezi. Ayyaam Al-Biydhw (Masiku Meupe) tarehe zake ni 13, 14 na 15 katika kila mwezi wa kalenda ya Kiislamu.

 

عَنْ جريرٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ عَن النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((صِيَامُ ثَلاثَةِ أَيَّامٍ مِنْ كُلِّ شَهْرٍ صِيَامُ الدَّهْرِ، أَيَّامُ الْبِيضِ صَبِيحَةَ ثَلاثَ عَشَرَةَ وَأَرْبَعَ عَشَرَةَ وَخَمْسَ عشَرَةَ))   

Imepokelewa kutoka kwa Jariyr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swiyaam siku tatu kila mwezi ni sawa na swiyaam ya milele; na masiku meupe ni tarehe kumi na tatu, kumi ay a na kumi na tano [13, 14, 15])) [An-Nasaaiy (2420) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Targhiyb (1040)]

 

عن أبي ذر رضي الله عنه: قال لي رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((يَا أَبَا ذَرٍّ، إِذَا صُمْتَ مِنَ الشَّهْرِ ثَلاثَةَ أَيَّامٍ فَصُمْ ثَلاثَةَ عَشَرَ وَأَرْبَعَةَ عَشَرَ وَخَمْسَةَ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Dharr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia: ((Ee Abuu Dharr! Endapo utafunga (Swawm) siku tatu za kila mwezi, basi funga siku ya 13, ya 14, ay a 15)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy na kasema Al-Albaaniy kuwa ni Swahiyh]

 

قال صلى الله عليه وسلم: ((أَلا أُخْبِرُكُمْ بِمَا يُذْهِبُ وَحَرَ الصَّدْرِ صَوْمُ ثَلاثَةِ أَيَّامٍ مِنْ كُلِّ شَهْر))

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Je, nikujulisheni jambo litakaloondosha uovu wa moyo? Ni kufunga (Swawm) siku tatu kila mwezi)) [An-Nasaaiy (2/2386) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh An-Nasaaiy (2249)]

 

Asw-Suyuutwiy (Rahimahu Allaah) amesema katika An-Nihaayah: Uovu wa moyo ni; udanganyifu, wasiwasi, na imesemwa pia ni uhasidi, chuki, na imesemwa pia uadui na imesemwa ghadhabu”

 

 

14-Fadhila Za Swawm ya ‘Arafah

 

عَنْ أَبِي قَتَادَةَ رضي الله عنه أن النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ :  ((صِيَامُ يَوْمِ عَرَفَةَ أَحْتَسِبُ عَلَى اللَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ السَّنَةَ الَّتِي قَبْلَهُ وَالسَّنَةَ الَّتِي بَعْدَهُ )) أخرجه مسلم

Abuu Qataadah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swawm ya 'Arafah nataraji (kwa Allaah) kufuta madhambi ya mwaka uliopita na wa baada yake)) [Muslim]

 

 

15-Fadhila Za Swawm ya ‘Ashuraa na mwezi wa Muharaam:

 

عَنْ أَبِي قَتَادَةَ اَلْأَنْصَارِيِّ  رضى الله عنه {أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ‏ صلى الله عليه وسلم ‏سُئِلَ عَنْ صَوْمِ يَوْمِ عَرَفَةَ.‏ قَالَ: " يُكَفِّرُ اَلسَّنَةَ اَلْمَاضِيَةَ وَالْبَاقِيَةَ "، وَسُئِلَ عَنْ صِيَامِ يَوْمِ عَاشُورَاءَ.‏ قَالَ: " يُكَفِّرُ اَلسَّنَةَ اَلْمَاضِيَةَ " وَسُئِلَ عَنْ صَوْمِ يَوْمِ اَلِاثْنَيْنِ، قَالَ: " ذَاكَ يَوْمٌ وُلِدْتُ فِيهِ، وَبُعِثْتُ فِيهِ، أَوْ أُنْزِلَ عَلَيَّ فِيهِ "} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Abuu Qataadah Al-Answaariy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliulizwa kuhusu Swawm ya siku ya ‘Arafah akasema: “Hufuta madhambi ya mwaka uliopita na unaobakia.” Akaulizwa kuhusu Swawm ya siku ya ‘Aashuwraa akasema: “Inafuta madhambi ya mwaka uliopita.”  Akaulizwa kuhusu Swawm ya siku za Jumatatu, akasema: “Hiyo ni siku niliyozaliwa na siku niliyopewa Unabiy na ni siku niliyoteremshiwa Qur-aan.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

16-Fadhila za Swawm Za Sitta Shawwaal:

 

وَعَنْ أَبِي أَيُّوبَ اَلْأَنْصَارِيِّ رضى الله عنه‏ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {مَنْ صَامَ رَمَضَانَ، ثُمَّ أَتْبَعَهُ سِتًّا مِنْ شَوَّالٍ كَانَ كَصِيَامِ اَلدَّهْرِ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Abuu Ayyuwb Al-Answaariyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwenye kufunga Ramadhwaan, kisha akafuatishia siku sita za mwezi Shawwaal. huwa kama Swiyaam ya  mwaka mzima.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

18-Fadhila Za Swawm ya Nabiy Daawuwd:

 

Amesema ‘Abdullaah bin ‘Amr bin Al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia: “Funga inayopendeza zaidi kwa Allaah ni funga ya Nabii Daawuwd … alikuwa anafunga siku moja na anakula siku moja” [Al-Bukhaariy, Muslim na an-Nasaaiy].

 

 

Swahaabiyaah aliyekuwa akipenda kufunga sana:  Hafswah bint ‘Umar ibnil-Khatwaab  (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa)

 

 

Ni mtoto wa ‘Umar ibnil-Khatwaab Khaliyfah wa pili wa Waislamu. Aliolewa na Khunis ibn Hudhaafa bin Qays As-Sahaamiy ambaye alikuwa katika kabila ya Quraysh. Mumewe alihajiri mara mbili; kwenda Abyssinia na kwenda Madiynah. Alipigana vita vya Badr kisha Uhud akariki akimuacha Hafswah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akiwa na miaka kumi na nane.

 

‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alihuzunika kwa msiba ya binti yake. Kila alipokwenda nyumbani kwake akimtazama hali yake huwa anahuzunika. 

 

 

Baada ya muda akaamua kumtafutia mume binti yake akaanza kwa Abuu Bakar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye ni rafiki mpenzi wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alipomuomba amuoe, Abuu Bakar hakumjibu kitu. ‘Umar akarudi akiwa amevunjika moyo na wala hakuamini Abuu Bakar kumkatalia ombi lake.

 

Kisha akaenda kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye mkewe ni Ruqayyah mtoto wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).  Alipomuomba, alimjibu kuwa: “Sipendi kuoa kwa hivi sasa.”

 

Umar akazidi kusikitika. Akaenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumlalamikia kuhusu Abuu Bakar na ‘Uthmaan, Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: ((Hafswah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ataolewa na mtu aliye bora kuliko ‘Uthmaan na ‘Uthmaan ataoa aliye bora kuliko Hafswah)) [Al-Bukhaariy]

 

‘Umar Alifurahi akawa anamuambia kila aliyemuona. Abuu Bakar alipomuona, alitambua furaha yake akampa hongera kisha akamuomba msamaha na kumuambia: “Usikasirike na mimi kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimtaja Hafswah (Radhwiya Allahu ‘anhaa) kabla na sikuweza kutaja siri yake. Ingelikuwa hakumtaja ningelimuoa”.

 

Watu wote Madiynah walifurahiwa na ndoa ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Hafswah bint ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) hivyo akaungana na mama waumini wengine kwa furaha.

 

Hafswah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa alikuwa rafiki mkubwa wa ‘Aishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) hivyo walipatana sana. Imesemekana kwamba Rasuli wa Allaah alimpa talaka Hafswah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) mara moja kutokana na makosa aliyoyafanya ya kutoa siri,  lakini alimrudia kutokana na amri kutoka kwa Jibryil (‘alayhis-salaam) alipomuambia: “Mrudie Hafswah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwani yeye anafunga (Swawm) na kuswali usiku kucha.”

 

Hafswah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alitambua makosa yake akajirudi na kuwa mke mtiifu na mwema. 

 

Alipofariki Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Abuu Bakar alipokuwa Khaliyfah, Hafswah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alichaguliwa kuwa msimamizi   wa nuskha ya kwanza ya Qur-aan. Aliendelea kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kufunga (Swawm) na kutunza Qur-aan. Kabla ya kuuawa baba yake, Hafswah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) aliachiwa kuwa msimamizi wa mirathi yake.

 

Hafswah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alifariki katika uongozi wa Mu’aawiyah ibn Abu Sufyaan. Alimuamrisha kaka yake ‘Abdullah bin 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) yale aliyoamrishwa na baba yake.  

 

 

 

 

 

 

Share