09-Madhara Ya Ghiybah: Hali Zinazoruhusu Ghiybah

 

  Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) Na An-Namiymah (Kufitinisha)

 

09- Hali Zinazoruhusu Ghiybah

 

 

 

Tumebainishiwa katika Shariy’ah yetu ya Kiislamu kuwa ziko hali zinazojuzu  Ghiybah kwa sababu ya maslaha yanayopatikana. Nazo ni kama ifuatavyo:

 

 

 

1-Kupinga dhulma ya Qadhi au Kiongozi au kuzuia dhulma isitendeke:

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 لَّا يُحِبُّ اللَّـهُ الْجَهْرَ بِالسُّوءِ مِنَ الْقَوْلِ إِلَّا مَن ظُلِمَ

Allaah Hapendi uovu utajwe hadharani isipokuwa kwa yule aliyedhulumiwa. [An-Nisaa: 148].  

 

 

2-Katika kushitaki anapodhulumiwa mtu haki yake:

 

Kutoa aibu ya mtu inapohitajika mfano kushtaki kwa mhusika (mkuu atakayeweza kutatua matatizo) mfano kulalamika: “Fulani kanidhulumu kadhaa na kadhaa, au kanifanyia kadhaa na kadhaa, au fulani hanipi haki yangu kadhaa na kadhaa."  Hii ni kutokana na dalili ifuatayo:

 

 

عَنْ عَائِشَةَ، أَنَّ هِنْدَ بِنْتَ عُتْبَةَ، قَالَتْ : يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّ أَبَا سُفْيَانَ رَجُلٌ شَحِيحٌ وَلَيْسَ يُعْطِينِي مَا يَكْفِينِي وَوَلَدِي، إِلَّا مَا أَخَذْتُ مِنْهُ وَهُوَ لاَ يَعْلَمُ، فَقَالَ: ((خُذِي مَا يَكْفِيكِ وَوَلَدَكِ ، بِالْمَعْرُوفِ )) متفق عليه

Kutoka kwa 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Hind mke wa Abuu Sufyaan alisema: "Ee Rasuli wa Allaah , Hakika Abuu Sufyaan ni mtu bakhili, wala hanipi kinachonitosha mimi na mwanangu ila ninachokichukua ilihali hajui." (ni sawa hivi nifanyavyo?) Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Chukua kwa wema kinachokutosha wewe na mwanao)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

3-Katika hali ya kubadilisha maovu:

 

Huenda Muislamu akaona maovu yanatendeka na hatoweza kuyaondosha ila aulizie sababu, na huenda atakayeulizwa amseme aliyetenda maovu mfano kusema: “Fulani ndiye aliyefanya ovu hili kadhaa na kadhaa."

 

 

4-Kujikinga na shari, na kunapotolewa nasiha kwa Waislamu:

 

عنْ فاطِمَة بِنْت قَيْس رضي الله عنها قالت أتَيْت النبي صلى الله عليه وسلم فَقُلْتُ إنَّ أبا الجهم ومعاوية خطباني فقال رسول الله صلى الله عليه وسلم ( أَمَّا مُعَاوِيَةُ فَصُعْلُوكٌ لَا مَالَ لَهُ، وَأَمَّا أَبُو جَهْمٍ فَلَا يَضَعُ عَصَاهُ عَنْ عَاتِقِهِ)) ))  متفق

وفي رواية لمسلم ((وأما أبو الجهم فضراب للنساء)) وهو تفسير لرواية لا يضع العصا عن عاتقه وقيل معناه كثير الأسفار

Faatwimah binti Qays (Radhwiya Allaahu 'anhaa) amesimulia: "Nilimuendea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nikamuambia: "Abul-Jahmi na Mu'aawiyah wameniposa." Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia: ((Ama Mu'aawiyah ni mtu fukara hanamali. Ama Abul-Jahmi haondoi fimbo juu ya shingo yake)) [Al-Bukhaaariy na Muslim]

 

Katika Riwaayah nyingine ya Muslim imesema: ((Na ama Abul-Jahmi anawapiga mno wanawake))

 

Riwaayah hii ni tafsiyr ya riwaayah isemayo: ((…haondoi fimbo juu ya shingo yake)) Na pia imesemekana kuwa maana ya kutoondosha fimbo juu ya shingo yake ni kuwa, anasafiri mno.

 

Ibn Taymiyyah amesema: Huenda anapotajwa kwa ubaya mtu kukawa ni kwa ajili ya nasiha kwa Waislamu kwa usalama au manufaa ya Dini yao na dunia yao.

 

 

5-Kuwasengenya mafisadi na watu wenye shaka:

 

Kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo ambayo Al-Bukhaairy ametoa hoja kuwa Hadiyth hii yafaa kuwasengenya mafisadi na watu wenye shaka.

 

عن عَائِشَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا أن رَجُلاً اسْتَأْذَنَ عَلَى النبي صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: ((ائْذَنُوا لَهُ بِئْسَ أَخُو الْعَشِيرَةِ))  متفق

 

Kutoka kwa 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anha) amesimulia kuwa mtu mmoja aliomba idhini ya kuingia kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Mruhusuni, ni mtu mbaya katika kabila lake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

6-Kuihami Dini kutokana na wanafiki:

 

عن عائشة رضي الله عنها قالت قال رسول الله صلى الله عليه وسلم ((مَا أَظُنُّ فُلاَنًا وَفُلاَنًا يَعْرِفَانِ مِنْ دِينِنَا شَيْئًا))   رواه البخاري

قال الليث بن سعد أحد رواة هذا الحديث كَانَا رَجُلَيْنِ مِنَ المُنَافِقِينَ 

Kutoka kwa 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) amesema: Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Sidhani fulani na fulani wanajua chochote katika Dini yetu)) [Al-Bukhaariy]

 

Layth bin Sa'ad ambaye ni mmoja wa wapokezi wa Hadiyth hii amesema: "Watu hawa wawili walikuwa ni katika wanafiki."

 

 

 

 

Share