Nampenda Lakini Nashindwa Kumwambia Nifanyeje?

Nampenda Lakini Nashindwa Kumwambia Nifanyeje?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

 

Nimewahi kutuma swali langu illa kwa uwezo wa Allaah sijajibiwa: Nikwamba mimi ni mwana mama ambae nimempenda mwanaume ila nimeshindwa kumwambia nae amemtaliki mkewe na mi piya mume amenitaliki sasa ninamfaham kwa tabia njema bwana huyo na nimempenda sasa nifanyeje kwa ajili ya Allaah maa salam.

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Suala hili tayari tumelijibu kwa kitambo sasa au ikiwa si hilo basi limefanana. Tofauti ya hili na lile la awali ni kubadilishwa ibara tu. Hakika ni tatizo kubwa kuwa wavulana hawataki kuoa na wasichana nao siku hizi hawataki kuolewa. Hivyo, inakuwa ili kutekeleza uchu wa kimaumbile huwa wavulana na wasichana wanafanya urafiki na kutekeleza hilo kupitia kwa zinaa ambao ni haram.

 

 

Tufahamu kuwa ndoa ni jambo muhimu sana na ni njia ya kutekeleza tendo la kimapenzi kwa njia ya halali pamoja na kufuata kanuni za kimaumbile na zile za Shariy’ah. Ndipo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuambia: “Mimi naswali na ninalala, ninafunga na kula na nimeoa wanawake. Yeyote atakayekengeuka (kuipa mgongo) Sunnah yangu si katika mimi” [al-Bukhaariy na Muslim].

 

Wazazi wa binti wengi au wasichana wanaona hayaa sana kuweza kumposa mvulana ambaye anaona kuwa atamfaa. Hili si jambo geni na linakubalika katika Shariy’ah kwani tunapata dalili kadhaa katika Qur-aan na Sunnah.  Mojawapo ni kisa cha binti wa mzee Swaalihina alipomshauri babake kuhusiana na Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam). Ilikuwa ni baada ya Nabiy Muwsaa ('Alayhis-salaam) kumkimbia Fir-‘awn aliposikia anataka kumuua, akatembea masafa marefu ya safari hadi akafika katika bahari ya Madyan akakuta watu tele wanachota maji, miongoni mwao walikuwa ni binti wawili ambao walishindwa kuchota maji kwa sababu ya zahma za watu. Basi yeye Nabiy Muwsaa ('Alayhis-Salaam) akawachotea kisha akakaa kitako pembeni katika kivuli, basi mmojawapo wa bint hao akampenda Nabiy Muwsaa (‘Alayhis-salaam); alipofika kwa baba yake akamshauri kuwa amlipe malipo mema, ndipo  alipomuozesha binti yake. Aayah hizo zimo katika Suwrah Al-Qaswasw (28: 22 – 28). Kati ya hizo ni Kauli Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَجَاءَتْهُ إِحْدَاهُمَا تَمْشِي عَلَى اسْتِحْيَاءٍ قَالَتْ إِنَّ أَبِي يَدْعُوكَ لِيَجْزِيَكَ أَجْرَ مَا سَقَيْتَ لَنَا ۚ فَلَمَّا جَاءَهُ وَقَصَّ عَلَيْهِ الْقَصَصَ قَالَ لَا تَخَفْ ۖ نَجَوْتَ مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٢٥﴾ قَالَتْ إِحْدَاهُمَا يَا أَبَتِ اسْتَأْجِرْهُ ۖ إِنَّ خَيْرَ مَنِ اسْتَأْجَرْتَ الْقَوِيُّ الْأَمِينُ ﴿٢٦﴾ قَالَ إِنِّي أُرِيدُ أَنْ أُنكِحَكَ إِحْدَى ابْنَتَيَّ هَاتَيْنِ عَلَىٰ أَن تَأْجُرَنِي ثَمَانِيَ حِجَجٍ ۖ فَإِنْ أَتْمَمْتَ عَشْرًا فَمِنْ عِندِكَ ۖ وَمَا أُرِيدُ أَنْ أَشُقَّ عَلَيْكَ ۚ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٢٧﴾

 

Basi akamjia mmoja kati ya wanawake wawili akitembea kwa kuona hayaa; akasema: Baba yangu anakwita ili akulipe ujira wa kutunyweshea. Basi alipomfikia na akamsimulia visa vyake; alisema: Usikhofu, umeokoka na watu madhalimu. Mmoja wao akasema: Ee baba yangu, muajiri! Hakika mbora uwezaye kumwajiri ni mwenye nguvu mwaminifu. Akasema: Mimi nataka nikuozeshe mmojawapo wa binti zangu hawa wawili kwa sharti kuwa unitumikie miaka minane; ukitimiza kumi, basi ni kutoka kwako. Na wala sitaki kukutia mashakani; utanikuta In Shaa Allaah miongoni mwa Swalihina. [Al-Qaswasw: 25 – 27]

 

 

Si mfano huo tu bali Siyrah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inatupatia mwongozo mzuri katika hilo. Hapa tunampata mama wa Waumini Khadiyjah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ambaye alimtuma rafiki yake wa kike amuulize Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaonaje ikiwa atamuoa yeye kwani yeye yuko tayari. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye hakusita bali alikubali kufunga naye Nikaah.

 

 

Pia tunapata kisa cha ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye baada ya binti yake, Hafswa (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kumaliza eda alianza kumtafutia mume kwa kwenda kwa Abu Bakr na ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) ili wamuoe binti yake.

 

 

Kwa hiyo, hilo ni jambo ambalo lipo.

 

Ama kuhusu kadhiya yako pia unaweza kufanya hivyo hivyo kwa kumtuma mtu mwaminifu aende amuelezee ile raghba yako ya kuwa unataka akuoe. Lakini chukua tahadhari kwa kutazama zile sifa za mume wa Kiislamu anazo ili usije ukajiingiza katika shimo. Chukua wakati kwa kuulizia kuhusu tabia zake, Dini yake, maadili yake na matendo yake. Tumia watu mbali mbali wakuletee maalumati hayo kuhusu huyo kijana. Ikiwa utaridhika na Dini na maadili yake basi swali Swalaah ya Istikhaarah kumtaka Allaah ('Azza wa Jalla)  mwongozo kuhusu hilo. Ikiwa mambo yote yapo sawa wakati huo utamtuma mtu ili amuulize kama atakuwa tayari kumuoa. Ikiwa atajibu ndio aje nyumbani kwenu kukuposa rasmi na hapo ndoa ifungwe.

 

 

Soma kuhusu Swalaah ya Istikhaarah katika viungo vifuatavyo:

 

 

Muda Wa Swalaah ya Istikhaarah

Swalaah Ya Istikhaarah Iswaliwe Kwa Ajili Ya Nini Na Ipi Du'aa Yake?

 

Tunakutakia tawfiyq  katika hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share