Kumlipa Ubaya Aliyekutendea Maovu Au Kumsamehe?

Kumlipa Ubaya Aliyekutendea Maovu Au Kumsamehe?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Kumrudishia mtu mabaya aliyokufanyia unalipwa dhambi? Sina zaidi ni mwana funzi wenu.            

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Si vizuri kwa mtu kumrudishia mabaya mwenziwe bali Muislaam anatakiwa asamehe na kwa hilo linampatia sifa nyingi ambazo hazifikiwi na wengine. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuachia mifano chungu nzima kwa kuwasamehe wapinzani wake pamoja na kuwa walimtesa sana. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَلَا تَسْتَوِي الْحَسَنَةُ وَلَا السَّيِّئَةُ ۚ ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِي بَيْنَكَ وَبَيْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِيٌّ حَمِيمٌ﴿٣٤﴾ وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ﴿٣٥﴾

 

Na wala haulingani sawa wema na uovu. Lipiza (uovu) kwa ambalo ni zuri zaidi; tahamaki yule ambaye baina yako na baina yake kuna uadui, atakuwa kama ni rafiki mwandani.  Na hapewi hayo isipokuwa wale waliovuta subira, na hapewi hayo isipokuwa mwenye fungu adhimu. [Fusw-Swilat: 41: 34 – 35].

 

 

Na kusamehe ni katika sifa za Muhsin ambaye anapendwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyosema:

 

 

الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاءِ وَالضَّرَّاءِ وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ ۗ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٣٤﴾ 

Ambao wanatoa (kwa ajili ya Allaah) katika hali ya wasaa na katika hali ya shida, na wanazuia ghadhabu, na wenye kusamehe watu. Na Allaah Anapenda wafanyao ihsaan. [Aal-‘Imraan: 134]

 

Na kisa cha Abu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipogoma kumpatia Swadaqah Swahaba aliyekuwa jamaa yake ambaye alikuwa mmoja wa waliohusika na kisa cha Ifk, kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akateremsha Kauli Yake ifuatayo na hapo Abu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) akaitikia Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na akamsamehe:

 

وَلَا يَأْتَلِ أُولُو الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ وَلْيَعْفُوا وَلْيَصْفَحُوا ۗ أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٢﴾

Na wala wasiape wale wenye fadhila miongoni mwenu na wenye wasaa wa mali kuwa hawatowapa (swadaqah) jamaa wa karibu, na masikini, na Muhaajiriyn katika njia ya Allaah. Na wasamehe na waachilie mbali. Je, hampendi Allaah Akughufurieni? Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.   [An-Nuwr: 22]

 

 

Na Allaah Anajua Zaidi

 

Share